The House of Favourite Newspapers

Bilionea Laizer Awakataa Mastaa wa Kibongo

0

HII inaitwa sitaki shobo! Bilionea mpya Bongo, Saniniu Laizer ambaye wiki iliyopita alitangazwa kuwa bilionea mpya wa madini nchini, amewakataa ‘live’ mastaa wa Kibongo wanaomtajataja mitandaoni.

 

Laizer alitangazwa na Serikali kuwa bilionea mpya baada ya kuchimba madini ya Tanzanite yenye thamani ya shilingi bilioni 7.8 huko Mererani wilayani Simanjiro, Manyara.

 

Katika mahojiano maalum (exclusive) na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, Laizer ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini, amesema kuwa yeye siyo mtu wa mitandao kabisa, hivyo hata hao wasanii wanaosema wanamjua, yeye hawajui.

“Unajua mimi siyo mtu wa mitandao kabisa kwa sababu huwa siangalii sana, lakini kingine watu ambao wanasema najuana nao, siyo kweli. Mimi ninawajua zaidi watu wa Mererani tu,” anasema Bilionea Laizer.

 

Bilionea huyo ambaye kwa sasa ni gumzo Bongo alisema kuwa, anasikia pia watu wakimfananisha yeye na mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, jambo ambalo siyo sawa Anasema wanaofanya hivyo ni vijana tu.Kingine, Bilionea Laizer anasema kuna mwanamke anawekwa naye mitandaoni ambaye hamjui kama inavyooneshwa.

 

“Nasikia wananiweka na msichana mweupe, hapana, mimi sina mwanamke kama huyo wanayemuonesha, lakini hata wanaonifananisha na Diamond, wanakosea sana kwa sababu tuko kwenye vitu tofauti.

 

“Siwezi kumuita mtu sijui Whozu kwa sababu nimepata pesa, siyo sawa na siko hivyo kabisa,” anasema Bilionea Laizer ambaye maisha yake yote anaishi mkoani Arusha na Manyara na kusisitiza hamjui hata huyo Diamond wala Wema.

 

Baadhi ya mastaa ambao wamekuwa wakimzungumzia Bilionea Laizer na wengine kujiita jina lake ni pamoja na video vixen maarufu Bongo, Annastazia Sebastian ‘Tunda’.

 

Wengine ni msanii wa Bongo Fleva, Lulu Abbas ‘Lulu Diva’, mtangazaji Loveness Malinzi ‘Diva’ na waigizaji kibao wakiongozwa na Yobnesh Yusuf ‘Batuli’.

 

Bilionea Laizer ambaye ni mchimbaji madini mdogo, amepata madini hayo ya Tanzanite ambayo yana thamani ya bilioni 7.8 ambapo moja lina kilo 9.2 na thamani yake ni bilioni 4.5 na la pili lina kilo 5.8 lenye thamani ya shilingi bilioni 3.3.

Leave A Reply