Bodaboda afa kwa kugongwa na mjamzito!

STORI: Idd Mumba, Wikienda
Mwanza: Inauma sana! Mwendesha pikipiki almaarufu bodaboda, Galus Fabian (30), mkazi wa Ilemela jijini hapa amefariki dunia baada ya kugongwa na gari aina ya Toyota RAV4 lililokuwa likiendeshwa na mama aliyedaiwa ni mjamzito aliyetajwa kwa jina la Wankoye Wambura.

Akisimulia mkasa huo wa kusikitisha uliotokea eneo la Soko la Kiloleni jijini hapa uliojiri wikiendi iliyopita, Nicolaus Charles alisema kuwa, mama huyo alikuwa ‘analiovateki’ gari lingine na kujikuta akipata kashikashi baada ya kumgonga bodaboda huyo aliyekuwa akimshusha abiria.

“Ilikuwa saa 1:00 asubuhi, nikiwa jirani na eneo la tukio nilishuhudia gari la Wankoye likiovateki gari lililokuwa mbele ndipo akamgonga bodaboda huyo aliyekuwa anamshusha abiria.
“Baada ya kugongwa, pikipiki ilitupwa mtaroni na Galus kufariki dunia palepale.

“Cha ajabu gari lililomgonga Galus lilianza kuwaka moto ulioanzia chini ya uvungu wake ila bodaboda wengine na wakazi wa eneo hilo waliudhibiti. Wakati wakiendelea na zoezi hilo, yule mama alitaka kutoroka ndipo madereva bodaboda wakamdhibiti,” alisema shuhuda huyo.

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba majeruhi walipelekwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Seko-Toure huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa hospitalini hapo wakati ukisubiri taratibu za mazishi.


Loading...

Toa comment