The House of Favourite Newspapers

Bonga Yai Kamusi Kitaa: COMMON EXPRESSION IN ENGLISH

(Misemo ya kawaida ya kiingereza)

Kamusi Sanifu

NI siku nyingine tunapokutana katika ukurasa huu, leo nataka tujadiliane kuhusu misemo ya kawaida ya Kiingereza, common expressions.

Ni matumaini yangu kwamba kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa darasa hili, angalau sasa utakuwa na uwezo wa kuzungumza maneno mawili matatu, kwa hiyo lengo la somo hili ni kuzidi kukuongezea maujanja katika lugha hii iliyokuja na meli.

I’M…

Katika sentensi nyingi za Kiingereza, utakutana na neno I’m mwanzo au katikati ya sentensi. I’m ni kifupi cha I am (ayem) ambayo humaanisha mimi nina… ikifuatiwa na neno unalotaka kulielezea.

Kwa mfano:

I’m so tired (Nimechoka sana).

I’m happy (Nina furaha).

I’m twenty three years old (Nina umri wa miaka ishirini na tatu).

I’m hungry (Ninaumwa na njaa).

I’m from Mbozi (Natokea Mbozi).

Unaweza kuongeza maneno kama extremely, very, terribly, super na kadhalika, kuonesha msisitizo wa unachokisema. Kwa mfano:

I’m extremely tired. (Nimechoka kupita kawaida).

I’m very happy. (Nina furaha sana).

I’M GONNA

Yawezekana huwa unawasikiasikia sana watu wakilitumia neno hili. Wala usiogope, kwanza lazima ujue kwamba I’m gonna… siyo neno la kisarufi la Kiingereza bali limetoholewa kutoka katika I’m going to… likimaanisha ninakwenda kufanya jambo fulani. Ni maneno yanayotumika kumuelezea mtu umepanga kufanya nini katika muda mfupi ujao.

Kwa mfano:

I’m gonna have some coffee. (Ninakwenda kunywa kahawa!)

I’m gonna go to work. (Ninakwenda kazini).

I’m gonna eat some cake. (Nitakula keki).

I’m gonna ask her out for dinner. (Nitamuomba tutoke kwa chakula cha usiku).

I’m gonna stop smoking. (Nitaacha kuvuta sigara).

I’M SORRY

Kila mmoja huwa anafanya makosa. Lakini inapotokea umemkosea mtu, kiungwana unatakiwa kuomba radhi. Sasa utaombaje radhi kama hujui hata neno moja linalotumika kuomba radhi?

I’m sorry/I’m very sorry/I’m so sorry hutumika kuomba radhi pale unapokosea jambo fulani. Lakini pia, unaweza kutumia this is my fault ukimaanisha hili ni kosa langu, yaani unakubali kosa.

Kuonesha kwamba umekwiva kisawasawa, unaweza kutumia ‘please accept my sincere apologies’ ukimaanisha tafadhali pokea msamaha wangu wa dhati.

CAN I ASK A FAVOUR?

Maana yake ni naweza kukuomba msaada? Huu ni msemo unaotumika unapotaka kuomba msaada kwa mtu. Yawezekana upo sehemu na umekwama jambo, pengine unataka kuuliza jambo au kuna msaada unahitaji. Ukimuona mtu na humjui lakini unahitaji msaada wake, ukianza na msemo huu utamleta karibu na utamshawishi aache anachokifanya na kukusikiliza. Baada ya hapo, utaeleza unachotaka kuuliza.

I’D LIKE TO KNOW…

Maana yake ni ‘napenda kufahamu kuhusu…’. Unaweza kumuuliza mtu chochote unachotaka kukijua na ukianza na msemo huu, utaonekana ni mtu uliyestaarabika. Unaweza kutumia msemo wa kwanza wa can I ask a favour? Kisha ukaendelea… I’d like to know where is the washroom ukimaanisha unataka unayemuuliza akuoneshe mahali vyoo vilipo.

I CAN’T WAIT…

Huu ni msemo ambao hutumika kuonesha shauku uliyonayo kusikia au kuona jambo fulani. Yawezekana mtu amekupa taarifa nzuri ya kusisimua, ukiutumia msemo huu, ukaongeza na maneno mbele yake, utaonekana mjuzi wa lugha.

Kwa mfano, mpenzi wako alikuwa amesafiri, sasa anakutaarifu kwamba kesho anarudi na anataka muonane, basi unaweza kunogesha kwa kusema I can’t wait to see you! Ukimaanisha una shauku kubwa ya kumuona kabla hata ya hiyo siku aliyokwambia.

I’M LOOKING FOWARD TO…

Msemo huu hutumika kuonesha matarajio chanya uliyonayo kuhusu jambo fulani kutoka kwa mtu fulani. Yawezekana unaomba ‘appointment’ na mtu fulani muhimu, akakujibu kwamba atakuwa na nafasi labda wiki ijayo, basi ukitumia msemo huu unaonesha kwamba una matarajio makubwa kwamba wiki ijayo kweli mtaonana.

‘I’m looking foward to see you’ au ‘I’m looking foward to seeing you’, yote ni sawa na yana maana ileile ingawa kwa wajuzi wa lugha, watapendelea zaidi msemo wa pili, ukimaanisha unategemea au unaamini mtaonana tena.

HANG ON A MOMENT

Msemo huu, hutumika kumfikishia ujumbe kiungwana mtu unayezungumza naye kwamba kuna kitu kingine cha muhimu kimeingilia kwenye mazungumzo yenu kwa hiyo unamuomba akusubiri kidogo. Maana yake huwa ni ‘subiri kidogo’. Iwe mnazungumza ana kwa ana au kwa simu, ukisikia mtu amekwambia maneno hayo, unatakiwa kuwa na subira kidogo.

NO COMMENT

Yawezekana umeshakutana na msemo huu mara nyingi lakini ukawa huelewi maana yake na matumizi yake. Huu ni msemo ambao hutumika kuonesha kwamba mtu fulani hayupo tayari kuzungumzia chochote kuhusu alichoulizwa namara nyingu hutumiwa na wanasiasa au watu maarufu wanapohojiwa na vyombo vya habari.

Hata wewe unaweza kuutumia pale mtu anapokuuliza swali ambalo haupo tayari kulijibu, ukimaanisha ‘sina maoni au sina cha kuzungumza’.

MIND YOUR OWN BUSINESS

Japokuwa msemo huu huonesha ‘ujeuri’ kwa anayeutoa, mara nyingi humaanisha mtu hataki uendelee kumuuliza au kushughulika na mambo yake binafsi. Maana yake huwa ni ‘shughulika na mambo yako’. Maneno haya mara nyingi hutamkwa na mtu aliyekasirishwa au kukerwa na jambo unalomsemesha na busara ni kwamba mtu akikwambia maneno haya, unaachana naye na kuendelea na mambo yako binafsi kama alivyokwambia.

MASURUPWETE:

Hizi ni nguo ambazo zimechakaa na kuchanikachanika.

NA MWALIMU HASHIM AZIZ

Comments are closed.