The House of Favourite Newspapers

Bossou Akili Yote Yanga, Amtwangia Simu Lwandamina

0
Vincent Bossou.

BEKI wa Yanga, raia wa Togo, Vincent Bossou, amempigia simu Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina, akimuomba kurejea kwenye klabu yake hiyo ya zamani.

 

Mtogo huyo, aliachana na Yanga kwenye msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara baada ya mkataba wake kumalizika huku akigoma kuongeza mwingine kutokana na maslahi madogo.

 

Yanga hivi sasa ipo kwenye mipango ya kumsajili beki mwingine wa kati wa kimataifa kwa ajili ya kuiimarisha safu hiyo ya ulinzi katika kuelekea Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumatatu limezipata, beki huyo yupo kwenye mazungumzo mazuri na viongozi wa Yanga kwa ajili ya kurejea kuichezea kwa mara pili.

 

Beki huyo alimpigia kocha huyo kumshawishi ili amrejeshe kikosini katika usajili huu wa dirisha dogo lililofunguliwa juzi Jumatano.

 

Aliongeza kuwa, upo uwezekano mkubwa wa beki huyo kurejea Jangwani kwani ni kati ya wachezaji waliopendekezwa na kocha na mabosi wa timu hiyo katika kuiimarisha safu hiyo ya ulinzi.

 

“Yeye mwenyewe ameonyesha nia kubwa ya kurejea tena kwa mara ya pili kuja kuichezea Yanga na alimpigia simu kocha mwenyewe kuomba arudi Jangwani,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Bossou kuzungumzia hilo, alisema: “Mimi Yanga ni nyumbani, muda wowote nitarejea kuichezea, kwani ni timu niliyoichezea kwa mafanikio makubwa.

 

“Hivi sasa ninaendelea na mawasiliano na baadhi ya viongozi wa Yanga kwa ajili ya kurejea katika dirisha dogo la usajili ambalo limefunguliwa, kama Mungu akipenda mazungumzo yakienda vizuri, basi utaniona tena Yanga.”

Stori: Wilbert Molandi | Championi Jumatatu

Leave A Reply