The House of Favourite Newspapers

Bossou: Tambwe, Ngoma watatupa…

0

DONALD-NGOMA3.jpgDonald Ngoma

Said Ally na Omary Mdose
BEKI wa Yanga, Mtogo, Vincent Bossou, amesema tangu atue Bongo kucheza soka, hakuwahi kumuona straika hatari kwa kufunga mabao kama alivyo Mrundi, Amissi Tambwe.
Bossou ambaye amejiunga na Yanga msimu huu, tangu nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ awe majeruhi takriban miezi miwili sasa, amekuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara tofauti na hapo awali ambapo alikuwa akisugua benchi.
Bossou amesema kwa ushirikiano wa Tambwe na Donald Ngoma ni wazi wataifanikisha Yanga kuutetea ubingwa wao wa ligi msimu huu kutokana na kasi yao ya kufunga mabao ambapo Alhamisi iliyopita waliiwezesha timu yao kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Majimaji, huku Tambwe akifunga mabao matatu na kujichimbia kileleni kwa ufungaji akiwa na mabao 13.
“Kwa kweli sijawahi kuona mshambuliaji hatari zaidi ya Tambwe katika ligi hii kwani huyu jamaa anajua sana kufunga na huwa hana utani anapopata nafasi, naamini kwa kushirikiana na Ngoma (Donald) wataisaidia sana timu katika harakati zetu za kuwania ubingwa wa ligi,” alisema Bossou.
Ikumbukwe kuwa, mpaka mzunguko wa kwanza wa ligi unamalizika wiki iliyopita, Yanga imefunga mabao 36 huku 22 kati ya hayo yakiwa yamefungwa na Ngoma na Tambwe peke yao.
Wakati huohuo, Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime, amesema hivi sasa Tambwe ndiye mshambuliaji mwenye thamani kubwa kushinda wengine wote wanaoshiriki ligi kuu,
wakiwemo Kipre Tchetche wa Azam na Hamis Kiiza wa Simba.
“Kama wakiniambia kuwa ni mshambuliaji gani ambaye kwa sasa ningependa kuwa naye katika kikosi changu, basi nitasema ni Tambwe kwa sababu anajua majukumu yake uwanjani kuliko washambuliaji wengine.
“Siku zote kazi ya mshambuliaji ni kufunga, achana na mbwembwe nyingine, hivyo Tambwe ni namba moja kwangu kwa washambuliaji na kama ningekuwa naye katika kikosi changu, hakika tungetisha sana kwani nina viungo bora kabisa ambao angeshirikiana nao kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema Maxime.

Leave A Reply