The House of Favourite Newspapers

Mbowe Afungukia CCTV Kamera Zilizonasa Tukio la Lissu, Aituhumu Tena Serikali – Video

0
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema afya ya Mbunge Tundu Lissu ambaye amelazwa hospitalini Nairobi, Kenya, baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa risasi mjini Dodoma zaidi ya mwezi mmoja uliopita, imeimarika na ametoka katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Hayo yalisemwa leo na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam.

“Afya ya Mheshimiwa Lissu imeendelea kuimarika… Mheshimiwa Lissu alihitaji upasuaji mwingi sana wa maeneo mbalimbali ya mwili wake ambao ulijeruhiwa na risasi nyingi zilizoingia na zingine kutoka,” alisema Mbowe na kuongeza kwamba kuimarika huko kumekuja kama miujiza na akawashukuru wote waliokuwa wakimwombea mbunge huyo na Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika kupona.

Aliendelea kuwa Lissu amefanyiwa upasuaji mbalimbali mara 17 na kwamba amepewa damu nyingi kuliko aliyowahi kupewa mgonjwa yeyote aliyeingia katika hospitali hiyo ya Nairobi kwa miaka 20 iliyopita.

“Amekaa ICU kwa muda wote tangu apelekwe huko, lakini wiki iliyopita ametoka ICU na mashine zote zilizokuwa zikimsaidia mwilini mwake zimeondolewa,” alisema Mbowe na kuongeza kwamba hatumii tena mashine ya hewa ya oksijeni na anakula mwenyewe chakula anachotaka.

“Wikiendi iliyopita, kwa mara ya kwanza ameliona jua,” alisema Mbowe akimaanisha Lissu alitolewa nje kwa mara ya kwanza na akasema tangu jana chama chake kingeanza kutoa picha za Lissu kuonyesha hali yake ilivyoimarika. “Mtamsikia kwa sauti yake na mtaiona video yake,” alisema.

Kiongozi huyo ambaye pia ndiye kiongozi wa upinzani bungeni, aliendeleza kauli za tuhuma za chama chake kwamba vyombo vya usalama na ulinzi vya serikali vilihusika katika shambulio hilo dhidi ya Lissu.

“Katika maeneo ambayo kuna kamera za kuchukua matukio yote yanayotokea (CCTV), katika maeneo ambayo yana askari na vyombo vya usalama vinapofanya kazi masaa ishirini na nne wakiwa na silaha haiwezekani mtu akashambuliwa kwa kiwango kile, mchana saa saba.

Mheshimiwa Lissu ni jirani wa waziri, kwenye nyumba ya waziri huyo kuna kamera ya CCVT. Taarifa zetu za uchunugizi zinasema ile CCTV imeondolewa. “Imeondolewa na nani? Kwa sababu gani?

Na ilipelekwa wapi? Kwa hiyo tunapenda kujua kabisa kwamba jambo hili limetendwa na vyombo vya serikali. Na hili hatumung’unyi maneno. Na waliotenda wanajulikana na mfumo ulioandaliwa na ujasusi huu,” alisema Mbowe. Aliongeza kwamba suala la usalama wa Lissu halikuwa jambo dogo kwani bado kuna watu wengine ambao walikuwa wamo katika orodha ya kufanyiwa vitendo kama alivyofanyiwa Lissu.

Kuhusu gharama zote za matibabu na huduma mbalimbali hospitali Nairobi, mwenyekiti huyo alisema hadi anaondoka Nairobi ilikuwa imefikia kiasi cha Sh. milioni 412 na kwamba bado matibabu yalikuwa yanaendelea ambapo aliwaomba watu wote kuendelea kusaidia kuchangia gharama hizo.

Awali ya hapo, Mbowe alikuwa amefafanua michango na gharama za matibabu tangu Lissu alipofikishwa hospitalini ambapo michango mingi ilitoka nchini na kwa Watanzania na watu wengine walio nchi za nje.

Akijibu moja ya maswali ya wanahabari, Mbowe alisisitiza kwamba kulikuwa na ulazima wa uchunguzi wa tukio hilo kufanywa na vyombo kutoka nje ya nchi hii kwa vile, alisisitiza, vyombo vya ndani ya nchi havionyeshi dhamira ya kulishughulikia suala hilo.

Alitoa mifano ya kupotea kwa msaidizi wake, Ben Saanane, na kuuawa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, ambapo hadi leo polisi hawajatoa jibu lolote la uchunguzi. Mbowe alimalizia kwa kusema kwamba kitendo cha kushambuliwa Lissu hakitakikwamisha chama chake katika kutafuta haki na kwamba hakitaogopa vitisho vyovyote.

VIDEO YA MBOWE AKIFUNGUKA

Leave A Reply