The House of Favourite Newspapers

Breaking News: Rais Pierre Buyoya Afariki Dunia

0

RAIS wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya, ambaye aliiongoza  Burundi kwa mihula miwili kuanzia mwaka 1987 hadi 1993 kisha tena 1996 hadi 2003, amefariki dunia nchini Ufaransa akiwa na miaka 71, ambapo chanzo cha familia kimesema alifariki mjini Paris, Ufaransa siku ya Alhamisi kutokana na athari za ugonjwa wa Covid-19.

 

Jenerali huyo mstaafu alihudumu mara mbili madarakani kwa jumla ya miaka 13 baada ya kumpindua mtangulizi wake madarakani.

 

Mwezi Oktoba, alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani na mahakama ya Burundi kwa kosa la mauaji ya rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia nchini humo, Rais Melchior Ndadaye,  mwaka 1993 – ambayo yalisababisha mauaji ya karibu watu 300,000. Buyoya alikana kufanya makosa.

 

Mwezi uliyopita, alijiuzulu ujumbe wa Muungano wa Afrika wa eneo la Sahel, na kusema kuwa anataka kutumia muda wake zaidi kusafisha jina lake.

 

Maisha ya Buyoya katika siasa za Burundi

Marehemu Pierre Buyoya aliingia madarakani mara ya kwanza kama rais baada mapinduzi ya kijeshi dhidi ya utawala wa Rais Jean-Baptiste Bagaza mwaka 1987 ambaye pia aliingia madarakani kwa mapinduzi dhidi ya mtangulizi wake, Michel Micombero, mwaka 1976.

 

Utawala wake wa miaka sita uligubikwa na mambo mbalimbali ambayo yalibadili sura ya nchi kama vile mauaji ya kinyama yaliyofanyika katika kitongoji cha Ntega-Marangara mwaka 1988, makubaliano ya umoja wa Warundi yaliyoidhinishwa mwaka 1991, kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1993, na mengine mengi.

 

Aliondoka madarakani mwaka 1993 baada ya kushindwa katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi kuwahi kufanyika tangu mwaka 1960. Wakati huo, mtangulizi wake, Ndadaye, kutoka chama cha Frodebu ndiye aliyemshinda kwa asilimia zaidi ya 65% ya kura na Pierre Buyoya aliyekuwa wakati huo amegombea kwa tiketi ya chama cha Uprona aliibuka na 33% za kura.

 

Buyoya alirejea tema madarakani mwezi wa Julai 1996, baada ya kumpindua tena madarakani rais wa mpito, Sylvestre Ntibantunganya, ambaye wakati huo alichukua madaraka kufuatia kifo cha Cyprien Ntaryamira ambaye alikufa katika ajali ya ndege pamoja aliyekuwa rais wa Rwanda wakati huo, Juvenal Habyarimana.

 

Ntaryamira alikuwa ameshikilia kiti cha urais kwa miezi miwili pekee, baada ya kifo cha Rais Ndadaye. Kuuawa kinyama kwa  Ndadaye kulilitumbikiza taifa katika vita vya kikabila, kati ya Watusi na Wahutu nchini humo.

 

Hali hiyo ilimlazimu Rais Buyoya kufanya mazungumzo na wapinzani wa serikali waliokuwa wameanzisha vita, mazungumzo yaliyodumu kwa muda wa miaka miwili kuanzia mwaka 1998 hadi pande hizo mbili zilipoweza kusaini makubaliano ya amani mwezi Agosti mwaka 2000.

 

Tangu wakati huo, Rais Buyoya alikubaliwa kuhudumu kwa kipindi cha mpito cha kilichokubaliwa katika makubaliano ya kwanza kwa mujibu wa makubaliano ya amani yaliyoidhinishwa Arusha, na baadaye akaondoka madarakani mwaka 2003 na utawala wa nchi kuchukuliwa na Rais Domitien Ndayizeye.

 

Mwaka 2008, aliteuliwa kuwa mjumbe maalumu wa amani Umoja wa Mataifa katika nchi ya Mali na Sahel kufuatia mzozo wa kivita uliokuwa ukitokota kati ya Mali na nchi jirani ya Sudan.

 

Mwezi wa Januari mwaka 2013,  aliteuliwa tena na Umoja wa Afrika kama mjumbe maalumu katika nchi ya Mali na eneo la Sahel.

 

Mwaka 2014, alijaribu kugombea nafasi ya uongozi wa nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa na wakati huo serikali ya Burundi ilimuunga mkono kwani uhusiano baina yao ulikuwa bado ni mzuri.

 

Hata hivyo, mambo yalibadilika kuanzia mwaka 2015, wakati ulipoibuka mzozo wa kisiasa kuhusiana na aliyekuwa rais wa Burundi hayati Pierre Nkurunziza, kugombea muhula wa tatu wa urais.

 

Wakati huo wapinzani wa serikali walisema kuwa hatua ya Nkurunziza ni kinyume cha sheria, lakini chama chake cha CNDD-FDD, walisisitiza kuwa hatua hiyo ni kwa mujibu wa sheria.

 

Wakati huo, Buyoya hakukubaliana na hatua ya Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu akinukuu kuwa “makubaliano ya amani ya Arusha” yanabainisha wazi kwamba rais anapaswa kuongoza kwa mihula miwili pekee.

 

Kutokana na kauli hiyo, uhusiano wake na utawala wa Nkurunziza uliharibika na hakuweza tena kukanyaga katika ardhi ya Burundi.

 

Tunaendelea kukufahamisha kwa kina juu ya maisha ya kisiasa ya Pierre Nkurunziza …

Leave A Reply