The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Ateua Wakuu wa Mikoa Wapya

0

RAIS Samia Suluhu Hassan amepangua wakuu wa mikoa na kuteua wapya akiwemo David Kafulila, Amos Makalla na Queen Sendiga ambaye aligombea urais katika uchaguzi mkuu mwaka 2020 kwa tiketi ya chama cha ADC.

 

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Mei 15, 2021 na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa wateule hao wataapishwa Ikulu, Dar es Salaam Mei 18, 2021.

 

Kafulila kada wa zamani wa NCCR-Mageuzi na Chadema ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha kuchukua nafasi ya Idd Kimanta aliyestaafu.

Katika uteuzi huo, Makalla ambaye amewahi kuwa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ameteuliwa tena kuwa mkuu wa mkoa huo kuchukua nafasi ya Aboubakar Kunenge aliyehamishiwa Pwani kuchukua nafasi ya Evarist Ndikilo ambaye amestaafu.

 

Queen ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Iringa kuchukua nafasi ya Ali Hapi aliyehamishiwa Tabora huku Rosemary Senyamule akiteuliwa kuuongoza Mkoa wa Geita akichukua nafasi ya Robert Gabriel aliyehamishiwa Mara kuendelea na wadhifa huo.

Brigedia Jenerali Charles Mbuge ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Kagera kuchukua nafasi ya Meja Jenerali Marco Gaguti na Mwanamvua Mrindoko yeye ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Katavi kuchukua nafasi ya Juma Homera aliyehamishiwa Mbeya.

 

Aliyekuwa katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kuchukua nafasi ya Anna Mghwira ambaye amestaafu.

 

Naye Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Ruvuma akichukua nafasi ya Christine Mndeme ambaye ameteuliwa kuwa naibu katibu mkuu wa CCM.

 

Omary Mgumba ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Songwe akichukua nafasi ya Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela aliyestaafu. Mgumba alikuwa mbunge wa Morogoro Kusini na naibu Waziri wa Kilimo hadi mwaka 2020.

 

Rais Samia pia amemteua Makongoro Nyerere kuwa mkuu wa Mkoa wa Manyara akichukua nafasi ya Joseph Mkirikiti aliyehamishiwa Rukwa kuchukua nafasi ya Joachim Wangabo aliyestaafu.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amehamishiwa Dodoma kuchukua nafasi ya Dk Binilith Mahenge aliyehamishiwa Mkoa wa Singida kuchukua nafasi ya Dk Rehema Nchimbi aliyestaafu.

 

Aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amehamishiwa Simiyu huku aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila akihamishiwa Mwanza.

 

“Amemteua Zainab Telack kuwa mkuu wa Mkoa wa Lindi. Kabla ya uteuzi huo, Telack alikuwa mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na anachukua nafasi ya Godfrey Zambi ambaye amestaafu.”

 

“Juma Homera aliyekuwa Mkoa wa Katavi kahamishiwa Mkoa wa Mbeya huku aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella akihamishiwa Mkoa wa Morogoro kuchukua nafasi ya Loata Erasto Ole Sanare ambaye amemaliza muda wake. Aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amehamishiwa Mkoa wa Tanga,” inaeleza taarifa hiyo.

 

Katika uteuzi huo, kiongozi mkuu huyo wa nchi amemteua aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Marco Gaguti kuwa mkuu wa Mkoa wa Mtwara akichukua nafasi ya Gelasius Byakanwa ambaye atapangiwa majukumu mengine.

 

Aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Philemon Sengati amehamishiwa Shinyanga na nafasi yake kuchukuliwa na Hapi.

Wakuu wa Mikoa waliobaki katika maeneo yao ni Thobias Andengenye (Kigoma) na Marwa Rubirya (Njombe).

Leave A Reply