CAF Yazuia Mkataba wa Okwi Simba

WAKATI uongozi na mashabiki wa Simba wakiendelea kutafakari hatma ya mshambuliaji wao, Mganda, Emmanuel Okwi kama atasalia hapo ama la, sasa mambo ni moto. Kwa taarifa yako tu ni kwamba, kuna uwezekano mkubwa msimu ujao Okwi asionekane katika kikosi hicho baada ya hivi karibuni kudaiwa kugoma kuongeza mkataba.

 

Kutokana na hali hiyo, inadaiwa Okwi ameamua kuiweka kando Simba na kutumia fursa nyingine ambayo ameipata kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf) atakapokuwa akitumikia timu ya taifa ya Uganda kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Juni, mwaka huu nchini Misri.

 

Okwi amepanga kuzitumia vilivyo fainali hizo kuhakikisha anazishawishi timu nyingine ambazo zinamuhitaji ili ziweze kumsajili. Habari za kuaminika ambazo Championi Ijumaa limezipata kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa Okwi amegoma kusaini mkataba mpya Simba kutokana na dau analotaka kupewa kuliona kuwa ni dogo.

 

“Okwi ameuomba uongozi usubiri kwanza mpaka atoke katika Afcon. Hata hivyo, ukweli ni kwamba anatarajia kuitumia michuano hiyo ili kupata timu nyingine ambayo itampatia fedha nyingi zaidi ya zile ambazo tunataka kumpa,” kilisema chanzo.

 

Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema: “Ni kweli Okwi tumeshafanya naye mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya lakini ametuambia tusubiri kwanza mpaka atoke Afcon ndipo kila kitu kitafahamika.”

Loading...

Toa comment