The House of Favourite Newspapers

CCM Yaanika Namba Maalum Kushughulikia Rushwa -Video

0

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza namba maalum ya kushughulikia wanachama wake wasiokuwa waadilifu kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020.

 

Akiitangaza namba hiyo mapema leo  Juni 1, 2020 hii ambayo itatumika kwa ajili ya kutumia ushahidi wa video na sauti, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole alisema anafahamu tayari kuna watu wameshaanza kupita kutoatoa rushwa hivyo kupitia namba hiyo, watawashughulikia vilivyo.

 

Alisema, watakapojiridhisha kwamba mwana-CCM yeyote amefanya jambo lolote ambalo ni kinyume na maadili, hatapewa nafasi ya kugombea uongozi.

 

“Chama kimeamua kuweka utaratibu mpya wa kushughulikia viongozi wasiokuwa waadilifu. Tutatoa namba mahususi ya WhatsApp 0745 260364 tutumieni ushahidi video na sauti, tutawashughulia,” alisema Polepole.

 

Alisema kwa kipindi cha sasa filimbi rasmi ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu bado haijapulizwa hivyo ni marufuku kuanza kufanya vitendo vyovyote vyenye viashiria ya kampeni.

 

“Kuna watu bado wapo katika nafasi ya uongozi hivyo CCM inasisitiza wakati huu waachwe wamalizie kutumikia nafasi zao za uongozi,” alisema.

 

Polepole alisema wapo watu ambao wanazunguka mikoani wanachanganisha pesa kwa ajili ya fomu ya mgombea urais wa CCM ni matapeli na watu wanatakiwa kutolewa taarifa ili wachukuliwe hatua na vyombo husika.

 

“Kwa mila na desturi yetu mpaka sasa mgombea wa urais anajulikana. Ukiona mtu anazunguka kusema anasaka hela ya fomu kwa ajili ya mgombea urais mpuuzeni na mumtolee taarifa,” alisema Polepole na kuongeza:

 

“Wapo watu wanaojipitisha na kusema wametumwa na mwenyekiti kwenda kugombea sehemu yoyote niwaambie hakuna mwenyekiti aliyewatuma kwa upande wa Bara na Zanzibar.”

 

Polepole alisema, chama chao kina misingi thabiti ya ambayo inahakikisha mgombea ambaye anapitishwa kugombea nafasi yoyote ya uongozi anakuwa mwadilifu.

 

“Katiba ya CCM inaeleza kuhusu sifa za kiongozi wa CCM, ibara ya 17, kiongozi awe na sifa zifuatazo; awe ni mtu aliyetosheka na asiwe mbinafsi. Kurubuni wanachama kwa hongo na rushwa hairuhusiwi ndani ya chama chetu cha Mapinduzi.

 

“Ni marufuku kwa mwanachama au wakala wake kufanya vitendo vyovyote vinavyoashiria kurubuni watu. Ni marufuku kwa mgombea yeyote kuzunguka katika matawi kwa kisingizio cha kujitambulisha, jina lako litaondolewa tukikubaini,” alisema.

Stori: Erick Evarist | GPL

 

Leave A Reply