The House of Favourite Newspapers

CCM Yasambaratisha Ngome ya Upinzani Kibiti, Umati Warudisha Kadi Wakiwemo Viongozi

0
Mbunge wa Jimbo la Kibiti, Twaha Mpembenwe akizungumza kwenye mkutano huo.

 

 

23 Oktoba 2022: NGOME ya upinzani wilayani Kibiti imesambaratishwa. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia umati wa wanachama wa vyama mbalimbali vya upinzani wakiwemo viongozi kurudisha kadi kwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia Chama cha Mapinduzi ‘CCM’, Twaha Mpembenwe na Mwenyekiti wa Chama hicho wilayani humo, Juma Kassim Ndaruke.

Umati ukimshangilia Ngachoka baada ya kutangaza kurudi CCM kwenye mkutano huo.

 

Wanachama hao walirudisha kadi za vyama vyao kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge Mpembenwe na kufanyika kijiji cha Mbwera Magharibi Kata ya Mbuchi, Kibiti mkoani Pwani kwaajili ya uzinduzi wa ujenzi wa Sekondari ya Mbuchi jimboni hapo.

Ngachoka akirudisha kadi ya CUF kwa Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kibiti, Juma Kassim Ndaruke kulia ni Mbungte wa Kibiti, Twaha Mpembenwe.

 

Akizungumza kwa niaba ya wenzake walioamua kurudisha kadi na kujiunga na CCM aliyekuwa kiongozi wa CUF wilaya na Kibiti, Haji Juma Ngachoka amesema yeye na wenzake hawaoni sababu ya kuendelea kujiita wapinzani na kuacha kumuunga mkono Mbunge wa Jimbo hilo Twaha Mpembenue ambaye ameonesha jitihada kubwa sana za kujenga Kibiti huku akihamasisha kauli mbiu yake ya Kibiti Kwa Maendeleo.

Huyu naye akipewa kadi ya CCM baada ya kurudisha kadi ya upinzani.

 

Katika uzinduzi wa ujenzi wa shule hiyo mbunge Mpembenwe amejitolea mifuko 100 ya saruji na nondo 70 na kwenye kata zingine ameshasaidia mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule, zahanati, ofisi za chama na mengineyo.

Sehemu ya wananchi wakifuatilia matukio kiumakini kwenye mkutano huo uliofanyika Kijiji cha Mbwera Magharibi Kata ya Mbuchi mkoani Pwani.

 

Ngachoka amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi katika upinzani wa kupingana hata katika suala la kimaendeleo lakini kutokana na kasi anayoonesha Mbunge Mpembenwe ameona siasa za kupingana kwa jambo haziwezi kuleta maendeleo katika jimbo hilo.

Sehemu ya wanachama wa vyama vya upinzani wakionesha kadi za CCM baada ya kurudisha kadi za vyama vyao.

 

“Siku zote sisi kazi yetu ilikuwa kuleta upinzani kwa jambo lolote hata likiwa la maendeleo sasa tumeona mbunge huyu anafanya mambo ambayo ukimpinga utaonekana siyo bure una lako jambo, kama leo amekuja kuzindua mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari kwa gharama zake, sasa mpaka hapo umpinge tu kwakuwa wewe ni mpinzani.”

 

Kwa mpenda maendeleo ya kweli huwezi kuendelea kumpinga hivyo mimi na wenzangu tumeamua kwa pamoja kurudisha kadi na kujiunga na CCM ili tumuunge mkono mbunge kwa jitihada zake za kimaendeleo.” Alimaliza kusema Ngachoka kwa niaba ya wenzake.

 

Miongoni mwa waliorudisha kadi na kujiunga na CCM kwenye mkutano huo ni pamoja na Haji Juma Ngachoka, Haridi Maulid Abudu, Shabani Milala, Juma Muhenga, Bakari Likokotae, Maulid na Amagae.

 

Kundi la wananchi wengine waliokuwa kwenye  msururu wa kurudisha kadi za upinzani waliambiwa muda ulikuwa umekwisha hivyo walipangiwa utaratibu maalum wa kurudisha kadi hizo na kuwa wanachama wapya wa CCM.

 

Baada ya zoezi hilo, Mwenyekiti CCM Wilaya ya Kibiti, Juma Kassim Ndaruke akifunga mkutano huo aliwapongeza wanachama hao wapya kwa nia yao ya kuunga mkono maendeleo ya jimbo hilo na kuwakaribisha kwa ajili ya kuijenga Kibiti ya Maendeleo.  HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS NA ISSA MNALLY/ GLOBAL PUBLISHERS

Leave A Reply