The House of Favourite Newspapers

Cedric Kaze Arudishwa Yanga

0

IMEFAHAMIKA kuwa Yanga ipo katika hatua za mwisho za kumrudisha aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mrundi, Cedric Kaze awe kocha msaidizi kikosini hapo.

Hiyo ni katika kuhakikisha wanaliboresha benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mtunisia, Nasreddine Nabi. Kabla ya kuvunjiwa mkataba msimu uliopita, Kaze aliipa Yanga Kombe la Mapinduzi.

Mmoja wa mabosi wa Yanga, ameliambia Spoti Xtra kuwa, wanamrudisha Kaze kutokana na kulifahamu aina ya soka la hapa nchini.

Bosi huyo alisema kuwa, wanaamini kuwa uwepo wa Kaze katika kikosi hicho kwa kushirikiana na Nabi kutatengeneza timu imara itakayobeba makombe msimu ujao, huku akiweka wazi kwamba, kocha huyo amekubali kurejea kuifundisha Yanga.

“Kaze hana tatizo lolote na viongozi, aliondoka kwa amani baada ya pande mbili kukaa pamoja na kukubaliana kufikia muafaka wa kuusitisha mkataba wake.

“Viongozi wapo katika hatua za mwisho na Kaze na kama mambo yakienda vizuri, basi ndani ya wiki hii huenda akatua nchini kujiunga na Yanga,” alisema bosi huyo.

Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema: “Kwa hivi sasa sipo katika nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo, wanaohusika na hilo ni Kamati ya Mashindano, lakini kama kweli anakuja basi tutaweka wazi.”

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabity Kandoro, alisema: “Lazima tupate kocha msaidizi kwa sababu mwalimu mkuu hana mtu huyo kwenye benchi la ufundi, wapo watu wengi ambao wameonesha nia.”

WILBERT MOLANDI, Dar

Leave A Reply