The House of Favourite Newspapers

CHADEMA Yatoa Tamko Kesi ya Mbowe

0

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema uamuzi wa jana na Jaji Kiongozi Mustapha Siyani, pamoja na kuitwa uamuzi mdogo kwenye shauri dogo madhara yake hayapo tu kwenye haki ya Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na wenzake, bali katika mustakabali wa haki wa Taifa la Tanzania.

 

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Oktoba 21, 2021 na Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kufuatia Mahakama Kuu Division ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kutupilia mbali mapingamizi mawili ya Mbowe na wenzake mahakamani hapo jana na kuamua kesi ya msingi ya tuhuma za ugaidi iendelee.

 

“Naviomba Vyombo vya Habari siku ya leo,siku ya haki,utawala wa awamu ya sita Rais Samia Suluhu alipoapishwa kuna wakati alizungumza kuhusu haki na uhuru wa Vyombo vya Habari, hapa ninapozungumza mkiwa wawazi mnaweza kueleza kwa uwazi kwamba uhuru na haki zenu zimeanza kuingiliwa.

 

“Natoa wito kwenu Vyombo vya Habari bila kujali vitisho, vishawishi vya fedha na matangazo ni vyema mkaurusha mkutano huu na Waandishi wa Habari moja kwa moja na wale watakaoenda kurusha baada ya hapa na wale watakaoandika baada ya hapa mkaandike kwa uhuru na haki.

 

“Uvunjaji wa haki ukihamia mahakamani ni hatari sana kwa mustakhabali wa watu na nchi. Hili tukio la uamuzi uliofanywa jana na Jaji Siyani kwa kila anayetafakari kuhusiana na haki za binadamu na haki za watu ni vema akasikiliza na akaitafakari katika muktadha mpana wa haki.

 

“Mara ya mwisho nilizungumza nanyi kuhusu kesi ya Mwenyekiti tarehe 31/07/2021 wakati ule niliwaambia kauli ambayo niliwaambia kufunguliwa kesi ya mashtaka ya kubambikiza ya Ugaidi dhidi ya Mbowe, ni shambulio dhidi ya uhuru, haki na dhidi ya demokrasia.

 

“Nikawaasa kesi hii isichuliwe ni ya Mbowe pekee yake, isichukuliwe kama ni shambulio dhidi ya CHADEMA pekee kwa sababu madhara yake kwa nchi na wananchi yatakuwa makubwa kuliko shambulio dhidi ya Mbowe na CHADEMA, madhara yatakuwa kwenye uhuru, haki na demokrasia.

 

“Uamuzi wa jana na Jaji Kiongozi Mustapha Siyani, pamoja na kuitwa uamuzi mdogo kwenye shauri dogo madhara yake hayapo tu kwenye haki kwenye haki ya mwenyekiti Mbowe na wenzake kucheleweshwa au kuminywa kwa kuendelea kuwa gerezani leo siku ya 93 bali pia uamuzi uliofanyika.

 

“Jana umekwenda kutengeneza athari na madhara kwenye mfumo katika taifa letu kwa sababu maamuzi ya mahakama kuu hata kama yametolewa na Jaji mmoja, Mosi yana ushawishi kwa majaji wenzake wa mahakama kuu, pamoja na kuwa hayawalazimishi lakini pili na zaidi yanawaelekeza mahakama zingine zote za chini ya mahakama kuu juu ya maamuzi yake, ziwe ni mahakma za Hakimu Mkazi, Mahakama za wilaya na mahakama zingine.

“Hukumu ya Jana imekwenda kutoa mwanya na mwongozo usiokuwa halali kwa misingi ya haki na kisheria, Mosi, unatoa mwanya sasa kwa Polisi kwa kisingizio cha kutokukamilika kwa upelelezi, au kumsafirisha mtuhumiwa au kuna mtu mwingine wanamtafuta kama sehemu ya upelelezi.

“Kuwashikilia watuhumiwa kinyume cha haki na sheria zaidi ya masaa manne bila kuwaandikisha maelezo. Kama Jaji Kiongozi ameshindwa kutenda haki najiuliza huyo Jaji ambae atapangiwa kusikiliza kesi hii ataweza kweli kusimamia Haki?,” amesema Mnyika.

Leave A Reply