The House of Favourite Newspapers

Chakula cha Kuzuia Kuzeeka Haraka

0

Na Nwandishi Wetu | Uwazi| YOU ARE WHAT YOU EAT

ILI kudumisha muonekano wa ujana kwa mwili wako unahitaji kuupa mahitaji yake yaliyobadilika. Kuzuia kuzeeka haraka unahitaji chakula chenye calcium ya kutosha kuipa mifupa yako nguvu na kupata chakula chenye collagen kwa wingi ili kuifanya ngozi yako isiwe na makunyanzi mwilini, kiashiria cha uzee.

Katika miaka ya 1950 Mmarekani mwanasayansi mtafiti, Denham Harman aligundua kuwepo uhusiano mkubwa kati ya mwili kuzeeka na uwepo wa kemikali ambazo hutengenezwa na mwili katika ufanyaji wake kazi wa kawaida katika mwili wa mtu, kitaalamu huitwa free radicals.

Mwili una uwezo wa kudhibiti madhara yanayotokana na uwepo wa free radicals kwa kiasi fulani, lakini idadi ikizidi mwili huzidiwa na madhara mengi hutokea, yakiwepo kuzeeka kwa mwili na magonjwa mengi kama kansa, magonjwa ya moyo, mifupa (arthritis), usahaulifu (Alzheimer’s), ugonjwa wa parkinson’s na kisukari.

Free radicals katika mwili huweza kuongezeka kwa kutumia vitu kutoka nje ya mwili. Sumu kutoka nje zinazozalisha free radicals katika mwili ni pamoja na hewa chafu hasa inayotoka kwenye viwanda, moshi wa sigara, na chakula chenye dawa za kuulia wadudu na utumiaji wa pombe kwa kiwango cha kuzidi kiwango.

Kiwango kidogo cha free radicals kinachozalishwa na mwili wenyewe kinaweza kikadhibitiwa vizuri na kemikali nyingine zinazoitwa antioxidants ambazo nazo pia huzalishwa na mwili.

Free radicals za ziada zinazozalishwa na vitu kutoka nje ya mwili zisipodhibitiwa kikamilifu husababisha madhara mengi pamoja na magonjwa yaliyotajwa hapo juu.

Hivyo basi tunahitaji kupata chakula chenye antioxidants kwa wingi ili kuisaidia miili yetu kupambana na kemikali hizi za ziada. Kuna aina nyingi za antioxidants zikiwemo vitamini C, vitamini E, flavonoids na polyphenols kwa kutaja tu bila kuingia kwa undani zaidi.

Baada ya utangulizi huo, sasa ni wakati wa kupitia chakula ambacho kikitumiwa kitakupa vitu tulivyovitaja hapo juu na kuufanya mwili wako kuwa na mwonekano wa ujana daima.

Vitamini C

Katika utafiti wa Mtafiti Herman uliofanywa kwenye kikundi cha wanawake wenye umri wa miaka zaidi ya 40 ulionyesha kwamba wanawake wanaotumia chakula chenye vitamini C zaidi walikuwa na makunyanzi zaidi na ngozi zao hazikuwa kavu ukilinganisha na wale ambao walitumia vitamini hiyo kidogo.

Hii ni kwa sababu vitamini C ni antioxidant yenye nguvu inayozuia uharibifu wa seli na DNA za seli hivyo kulinda uzalishaji wa collagen ambayo ndiyo nguzo muhimu ya kulinda ngozi yako.Unashauriwa basi upate angalau miligram 75 za vitamini hii kwa siku.

Kwa mfano unaweza kupata chungwa moja wakati wa kifungua kinywa na pilipili tano za njano ndani ya saladi kwenye mlo wako wa mchana. Chakula chenye vitamini C kwa wingi ni broccoli, strawberries, pilipili nyekundu, nyanya, tikitimaji n.k.

Chakula chenye protini

Tafiti zilionyesha kuwa wanawake waliotumia protini zaidi walikuwa na makunyanzi machache zaidi kwenye ngozi zao kuliko wale ambao walitumia protini kidogo, hii kwa sababu protini hutoa viungo muhimu katika ujenzi wa collagen.

Ili upate protini unashauriwa kula nyama ya kuku isiyo na ngozi, sehemu nyeupe ya mayai na samaki. Unapochagua kula nyama ya ng’ombe au mbuzi, pendelea kutumia ile isiyo na mafuta. Matumizi ya soya yameonyesha kusaidia kuondoa ile mistari myembamba kweye macho.

Samaki

Samaki wa baharini wenye mafuta wamebainika kuwa na kiwango kikubwa cha ‘omega-3 fatty acids’, kitu ambacho husaidia kuilinda ngozi yako kutokana na mionzi mibaya ya jua ambayo hudhoofisha collagen.

Nafaka

Utumiaji wa nafaka zisizokobolewa badala ya wali mweupe, mikate inayotokana na ngano isiyokobolewa (brown bread) na nafaka nyingine una faida nyingi. Moja ni kuzuia mwongezeko wa insulin katika mwili ambayo ina madhara ya kuharibu ngozi. Pia nafaka nzima ni chanzo cha madini ya selenium ambayo husaidia kuikinga ngozi yako kutokana na mionzi ya jua.

Unashauriwa kutumia mchele usiokobolewa (brown rice), shayiri na ngano isiyokobolewa ili uweze kupata madini haya yatakayokusaidia kulinda ngozi yako.

Green Tea

Green tea ni kinywaji chenye antioxidants nyingi. Unywaji wa vikombe viwili au vitatu kwa siku vya chai hii utaifanya ngozi yako kuwa nyororo na kutopata makunyanzi.

Hatuwezi kuorodhesha vyakula vyote ambavyo vinafaa katika kuzuia kuzeeka haraka katika nafasi hii, hivyo makala yetu inatoa mwongozo tu wa kula.

Leave A Reply