The House of Favourite Newspapers

Chongo!-19

0

Ilipoishia wiki iliyopita.

Ufunguaji wa mlango na jinsi Jerry alivyoingia uliwafanya waamini kabisa pale ndipo alipokuwa anaishi. Nao wakageuza pikipiki na kutokomea!

Sasa endelea…

Bata alirudi nyumbani kwake akiwa na mawazo mengi, alimfahamisha Elina kilichoendelea. Hadi wakati huo, msichana huyo hakuwa ameelewa ni kitu gani hasa mpenzi wake alikuwa amejiandaa kufanya.

“Sijajua, hivi unataka ufanye nini kwa hiyo ishu?” Elina alijikuta akimuuliza mpenzi wake, ambaye kwa mtu ambaye hakuwa anamfahamu, alikuwa na sura ya kutisha akiwa ametoa miwani yake ya jua kama alivyokuwa hivi sasa chumbani kwao.

“Hivi kwa sura hii waliyonipatia, wewe unafikiri naweza kufanya nini?” Bata alimjibu mpenzi wake huku akibadili chaneli ya televisheni, kwani kwa muda ule, alikuwa akipenda sana kuangalia tamthiliya ya Kaka na Dada iliyokuwa ikionyeshwa katika Amani Tv kila Alhamisi.

“Sasa mimi nitajuaje jamani, si ndiyo maana nimekuuliza?”

“Kiukweli hata mimi mwenyewe sijui nitafanyaje, lakini inabidi kwanza nipate uhakika kama dada yangu yupo,” Bata alijibu.

“Hivi ukimuona utamkumbuka?”

“Nadhani nitamkumbuka, kama niliweza kumkumbuka mpenzi wake?”

“Sidhani, labda kama utamuona akiwa katika mazingira ya hiyo nyumba unayosema umejua anapokaa,”

Baada ya majadiliano ya kina juu ya nini kinapaswa kufanyika katika kufuatilia hilo jambo, kazi sasa ikabakia kuwa ngumu kwa Bata, namna ya kuweza kujua kama dadake yupo katika ile nyumba au la.

Alichofanya Bata ni kuhamisha maskani ya biashara yake katika mitaa ile ya Masaki. Katika mtaa ule wenye nyumba aliyoingia Jerry, kulikuwa na maduka mawili makubwa, yaliyokuwa na kiambaza kirefu ambacho hakikuwa na kitu chochote zaidi ya baadhi ya vijana kugeuza maskani yao.

Akiwa amebeba nguo nzuri za mtumba za akina dada na viatu vyao pea mbili mkononi na zingine kwenye begi lake dogo la mgongoni, Bata alikaa sehemu hiyo, muda mwingi macho yake yakiwa katika nyumba aliyoingia Jerry.

Katika siku yake ya kwanza, hakuweza kumuona mtu yeyote akitoka hadi ilipofika saa kumi na mbili jioni, alipokuwa akijiandaa kuondoka. Lakini kama ilivyokuwa siku ya kwanza, Jerry aliwasili na kubonyeza kengele na muda mfupi baadaye alifunguliwa.

Ilikuwa ni siku ya tano tokea aanze mazoea ya kukaa katika kibaraza hicho, ndipo Bata alipomuona mtu akitoka ndani ya nyumba hiyo. Alikuwa ni binti aliyeonekana kama msaidizi wa kazi, kwani alitoka na mtoto mdogo ambaye muonekano wake ulimtofautisha naye.

“Huyu atakuwa ni hausigeli,” Bata alijisemea kimoyomoyo, wakati msichana huyo alipotoka akija upande wake hadi alipoingia katika moja ya maduka yale mawili. Ile ilikuwa ni ishara tosha kuwa kulikuwa na mwanamke anayeishi mle ndani, kwani umri wa mtoto aliyeandamana na hausigeli, haukuonyesha kama angeweza kuishi bila mama yake.

Hakutaka kufanya haraka na kitu kingine, katika kipindi cha siku hizo tano, tayari Bata alishaanza kuzoeleka miongoni mwa vijana wa eneo hilo. Kilichowavutia kwao ni utanashati wake na pia nguo na viatu vizuri alivyokuwa akiwauzia, kwani eneo hilo, walijua nini wanataka kuvaa.

Kwa hali hiyo, vijana wa kike na kiume, wa shuleni na wale wa nyumbani, walikuwa wakimuagizia aina ya nguo wanazotaka na kwa kuwa Bata alikuwa mjuzi sana wa kuchagua nguo nzuri, aliwaletea bila taabu.

Uzoefu wake katika kuchagua nguo za mitumba ulimfanya kujuana na wauzaji wakubwa waliokuwa wakikata mabalo katika maeneo mengi kama mtaa wa Kongo, soko la Karume, Ilala, Manzese, Mwenge, Magomeni, Makumbusho, Tandika hadi Mbagala na wote hao angeweza kuchukua kwa mali kauli bila matatizo.

Wiki mbili baada ya kuwa ameanza kufanya biashara zake katika mitaa hiyo, akiwa hajamuona mtu mwingine yoyote zaidi ya Jerry, yule msichana wa kazi na mtoto, alianza kutilia shaka kama kulikuwa na mtu mwingine ndani, kwani kwake ilikuwa ni jambo gumu mtu kukaa ndani kwa wiki mbili pasipo kutoka nje, labda kama ni mgonjwa kitandani.

Siku hiyo, majira ya saa tisa alasiri, wakati akiwa anazungumza na sista duu mmoja aliyetaka kununua kitop, akaona mlango wa ile nyumba unafunguliwa na mwanamke mmoja aliyejifunga kitambaa cheusi kichwani, kikificha sura, akajitokeza. Muda mchache baadaye, teksi ambayo haikujulikana ilikotoka, ikaja na kusimama nje ya nyumba hiyo na mwanamke huyo akaingia.

“Wewe bitozi mbona umeduwaa, unamjua huyo?” yule sista duu alimshtua Bata, ambaye alishtuka na kujisikia aibu flani kwa kushindwa kujidhibiti.

Je, ni nani aliyeingia kwenye ile teksi? Kitu gani Bata atafanya juu ya tukio hilo? Usikose kupata majibu katika toleo lijalo!

Leave A Reply