The House of Favourite Newspapers

Unanunaje kwa kosa dogo? Unamkata stimu bhana!

0

Mashosti za mwaka mpya, nimefurahi kuuona mwaka, huenda mambo yakawa mazuri kwani kila msimu una mambo yake, kungwi sizeeki ujuzi ingawa miaka inaenda.. kwa nini nizeeke ujuzi wakati ng’ombe hazeeki maini bwana, halooo.

Leo nina mada inayonikera shangingi miye, ambayo lazima niwaambie wanawake wenzangu na hata nyie wababa mnaotufanya tunajidai huku mjini.

Kususa na kununa kwa jambo dogo ambalo mngeweza kulimaliza na mkaendelea na starehe zenu, kunapunguza mapenzi asikwambie mtu.

Mada hii imetoka kwa shosti wangu ambaye nitamhifadhi jina kwa leo, yeye ana mpenzi wake wanapendana sana, kiasi kwamba watu wakiwaona wanaona hakuna kama wao.

Kikubwa kinachomkera kwa mpenzi wake huyo ni tabia yake ya kususa na kununa hata kwa jambo dogo tu ambalo halina maana, mbaya zaidi yeye anapenda asikilizwe yeye tu na pale anapomkosea mwenzake hakubaliane na yeye.

Niwaambie tu wasomaji wa safu hii hakuna kitu kibaya kama mtu kununanuna kila wakati, hasa mnapokuwa mnaishi nyumba moja itafikia wakati mkeo au mume anataka kukwambia jambo anashindwa kwa sababu tu ya kuogopa kununa kwako.

Lakini pia inapunguza mapenzi kabisa kwani wewe unakuwa ni kisirani tu kila wakati mwenzako akipata wa kumchekesha anahamia huko utabaki wewe na kisirani chako mwanzo mwisho.

Wanaume wanaopenda kununanuna na kususa wanawakosea sana wapenzi wao, kwani mwanamke ni rahisi kumchoka na kuvunjika moyo haraka hali ambayo ni rahisi kumfanya mtu aingie kwenye mazingira hatarishi ya uhusiano anaoona unamfaa.

Mwanamke akihamishia majeshi kwingine huwa ni mbaya sana kwa mwanaume kwani hujiona mnyonge na ni rahisi kumfanyia kitu mbaya yule aliyemsaliti.

Tabia hiyo ni mbaya ambayo kama usipojilazimisha kuiacha na kila jambo kuona dogo huwa inakuwa siku hadi siku sasa jiulize unakuwa hivyo, sasa hivi uko kijana ukiwa mzee je itakuwaje?

Uzee wako unaweza kuwa mbaya sana kwani hata watoto wanaweza kushindwa kukaa na wewe, kama unanisoma na kujiona una tabia hii acha mara moja kwani wakati mwingine tabia hujengwa na wanadamu wenyewe.

Kwa leo naishia hapa shangingi mie, mnaonunanuna muache, la mtabaki na kununa kwenu.

Leave A Reply