The House of Favourite Newspapers

Chongo!-20

0

Ilipoishia wiki iliyopita
Alimpiga pigo moja tu shingoni na Bonviek, akaanguka bila hata mwenye duka kujua kama kulikuwa na mtu ameanguka. Kisha akawakonyeza akina Jerry na kutoka taratibu na kutokomea. Kuona hivyo, kina Jerry nao wakainuka haraka na kutoka!
Sasa endelea…

Sekunde chache wakiwa wametoka eneo la duka hilo, wakarejewa na fahamu kuwa endapo wataondoka, mwenye duka atafahamu wao ndiyo wahusika wa tukio hilo, hivyo wakarudi haraka walipokuwa wamekaa na kama walioshtuka, wakapiga kelele za hatari.
Vomel, mwenye duka akashtuka. Alikuwa akipanga vinywaji kwenye kabati lenye ubaridi, akaacha na kutoka nje mara moja.

“Kuna nini?” aliuliza kwa lugha ya Kiafrikaner baada ya kumuona Bonviek akiwa ameanguka chini. Kama walioambiana, wapenzi wale wawili wakajikuta wakimwambia ukweli wa kilichotokea, kwani hawakuwa na namna tena.

“Watakuwa ni watu wake hao wa cocaine, ukute wameshadhulumiana, anapumua kwa mbali sana,” alisema Vomel, ambaye pia ni Kaburu, wakati akimtazama na kusikiliza alichoambiwa. Baadaye akapiga simu polisi, ambao walipokuja, walimchukua na kumkimbiza hospitalini.

Siku mbili baadaye taarifa zikaja kuwa Bonviek alifariki na tayari alishazikwa. Walishangaa jioni hiyo, Sule alipofika tena dukani hapo na kuwakuta Jerry na Ame wametulia wakila kinywaji chao taratibu.

Walimkumbuka vizuri kabisa, lakini walipata wasiwasi kama alikuwa akifahamiana na marehemu au alikuwa mmoja wa waafrika kusini weusi wengi wenye chuki na wazungu. Kama ni hivyo, walipata hofu ya mwenye duka na usalama wake. Alipokaa katika kiti chake, Sule alibaini hofu ya wenyeji machoni mwao.

“Iam a good guy, worry out,” (Mimi ni mtu mzuri, msiwe na wasiwasi) Sule aliwaambia, akionesha tabasamu usoni mwake, kisha akamwita mwenye duka na kuomba apewe Vodka chupa kubwa.

Ili kuwaaminisha kuwa yeye hakuwa mtu mbaya, alipofungua chupa ya kinywaji chake na kuweka katika glasi, kabla ya kunywa akawaambia;
“My name is Suleiman, Tanzanian,” (Naitwa Suleiman, ni Mtanzania) alisema kijana huyo huku akiiweka glasi yake mdomoni, alipoishusha, ilikuwa ni zamu ya Ame kuzungumza.

“Kama wewe ni Mbongo basi lazima utakuwa komandoo,”
Sule alionesha mshtuko wa dhahiri, hakutegemea kama wale wangekuwa ni watu wa kwao na kama angejua hivyo mapema, asingeweza kujitambulisha. Lakini kwa kuwa maji yalikuwa yameshamwagika, hakuwa na jinsi.

“Kivipi yaani,” aliuliza.
“Jinsi ulivyomzimisha yule nguruwe siku ile sikuamini,” Jerry alidakia na ghafla, wakajikuta wamezama katika mazungumzo yaliyowafanya watambulishane vizuri wanakoishi na kufanya kazi.

Wiki moja baadaye, wakafahamiana vizuri zaidi, Sule akijipambanua kuwa ni askari wa kikosi maalum cha kupambana na majambazi aliyekimbia kazi miaka sita iliyopita, baada ya kutoridhishwa na kipato alichokihitaji.

Kwa kuwa akina Jerry walikuwa wameanza kupata utajiri wa kuwaweka katika daraja la kati huko Afrika Kusini, wakakubaliana na Sule aendelee kufuata mzigo wa unga Brazil na faida ambayo ingepatikana, wagawane nusu kwa nusu!

Sule akawapa mchongo mzima juu ya biashara hiyo na kuahidi kuwaelekeza masoko yaliyo ndani ya Afrika Kusini. Akina Jerry wakafurahi sana, kwani moyoni mwao waliamini kwa kuongeza na biashara hiyo, mafanikio yao yangeenda haraka zaidi kuliko ilivyo sasa.

Walifanya hivyo, Sule alikwenda Brazil na kununua cocaine, zaidi ya mara nne. Ndani ya miezi miwili ya biashara hiyo, akina Jerry wakajikuta wenye fedha ya kutosha na wakaingiwa na tamaa. Kitu kimoja ambacho hawakuwa wanajua ni kuwa Sule alikuwa mkorofi, mgomvi na asiyekubali uonevu.

Siku hiyo wakiwa nyumbani kwao usiku wa saa nne, simu ya mkononi ya Jerry iliita, alipoitazama, alikuwa ni Sule, alipoipokea na kuuliza kunani, kijana huyo alimfahamisha kuwa alikuwa nje ya nyumba yao mlangoni, akisubiri kufunguliwa.

“Nimeua,” Sule alisema mara tu alipokaa kwenye sofa, sigara mkononi. Jerry na mpenzi wake wakashikwa na mshangao, lakini kabla hawajajua sababu ya kufanya hivyo, Sule mwenyewe akawaelezea kwa kirefu juu ya kilichotokea.

“Ndiyo hivyo, kitu tunachoweza kukifanya kwa sasa ni kurudi Bongo kwa muda, maana watanitafuta sana, sasa kwa kuwa niliyemuua anajulikana sana hapa, itatusumbua, wakinikamata mimi, nyinyi hamtapona,” Sule alihitimisha mazungumzo yake na kuomba kama anaweza kupatiwa Vodka!

Je, nini kilitokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo!

Leave A Reply