The House of Favourite Newspapers

Chongo – 28

0

Ilipoishia wiki iliyopita
Bata alikuwa mitaa ya Gerezani, Kariakoo jijini Dar es Salaam nyumbani kwa kijana mmoja aliyeogopeka sana miongoni mwa watoto wa mjini, Gasto. Alipelekwa hapo na rafiki yake baada ya kumweleza lengo lake la kutaka kulipa kisasi, kwa mauaji ambayo hataki kumpa kazi hiyo mtu mwingine, lakini hataki atambulike.
Sasa endelea

Gasto, aliongoza genge lililoweza kuifanya kazi yoyote iliyo mbele yao, ikiwa ni pamoja na kuua, kuchoma moto majumba na viwanda, kusababisha ajali, kudhalilisha na kila aina ya adhabu ambazo zingelipiwa. Zaidi ya hayo pia, alitoa ushauri bure wa namna mteja wake anavyoweza kufanikisha lengo lake kwa mikono yake mwenyewe.
“Kwa jinsi ulivyonieleza, kazi hii unaweza kuifanya mwenyewe, tena kwa ulaini kabisa. Utatumia hii kitu,” alisema Gasto, akimwambia Bata aliyemtazama kwa utulivu, ndani ya miwani yake ya jua aliyovaa, wakati akiinuka na kulifuata kabati lililokuwa mbele yake.
Akafungua droo ya mlango wa chini, akatoa chupa ya dawa ya kupulizia wadudu, maarufu sana nchini ilifahamika kama OJ, iliyo na sifa ya kuua wadudu wote wanaotambaa na kuruka.
“Humu tunatia sumu yenye uwezo wa kufanya unachotaka, kuua, kupofua macho, kuuchanganya ubongo na kadhalika. Kwa hiyo unasema unachotaka mtu wako afanywe, sisi tunakutilia hiyo sumu kiufundi kabisa ndani ya hili kopo na popote unapotembea nalo, mtu anajua uko na OJ ya kuua wadudu,” Gasto alimwambia Bata, aliyekuwa anasikiliza kwa makini.
“Sawa bro, nadhani nimekuelewa vizuri sana, ngoja nirudi nikaratibu upya mpango wangu ili nijue nahitaji silaha ya namna gani katika maangamizi ninayopanga. Nitakuja tena kaka, nakushukuru sana kwa msaada wako,” Bata alimwambia Gasto, ambaye kwa kumuangalia, usingeweza kuamini kuwa alishatumika kutoa roho nyingi nchini.
***

Mwani alikuwa amekaa kwenye pub moja umbali mdogo kutoka nyumbani kwao, ambayo pia ilijumuisha vijana kadhaa wa mtaani kwao. Alikuwa hapo kwa ajili ya kusubiri simu ya Sule, ili apate kuungana naye katika sherehe iliyokuwa inafanyika nyumbani kwa mabosi wake, ambako yeye alikuwa na kazi ya ziada zaidi ya kumsindikiza mpenzi wake.
Hakutaka kulewa, hivyo mkononi mwake alikuwa na kinywaji Baltika, ambacho hakina kilevi kabisa. Kila mara aliitazama simu yake akiitazamia kuita au kuingia ujumbe kutoka kwa Sule, hasa baada ya kupita saa moja usiku, muda ambao aliambiwa atajulishwa.
Ni hadi ilipotimia saa mbili kasoro robo, ndipo simu ya Sule ilipoingia na alipopokea, aliambiwa gari lake, ambalo pia hulitumia kama teksi, itakuwa hapo dakika tano zijazo. Akajiweka sawa na muda huo ulipofika, mtu wake akawasili na kuegesha gari mbele kidogo, ambako Mwani alilifuata bila mtu mwingine kujua.
Ndani ya nyumba hiyo, uani, kulikuwa na matayarisho makubwa, kwani kulipambwa mapambo yaliyopafanya papendeze sana. Ingawa hakuwa ameingia katika nyumba hiyo kwa miaka mingi, lakini haikumzuia kutambua kuwa hakukuwa na tofauti yoyote na enzi zile. Kilichobadilika ni rangi tu, kwani hii ya sasa ilikuwa imepakwa upya.

Sehemu ile ambayo kulikuwa na chemba, kulikuwa kumepangwa spika, lakini pia kukiwa kumejengwa kibanda cha mabati, ambacho hakuelewa kilitumika kwa ajili ya kitu gani. Kibanda hicho, hata hivyo, kilionekana kuwa na faida kwao, kwani kilimfanya mtu atakayeibuka kutoonekana wakati akiinua mfuniko wake.
Macho ya Mwani yalifanya ziara katika ua huo kwa umahiri mkubwa, akilitazama dirisha linaloangalia uani hapo na jinsi mlango wa kuingilia sebuleni ulivyokuwa. Mlango mkubwa wa kuingia getini, haukuonesha kama kulikuwa na kibanda cha mlinzi. Katika wageni wachache waliokuwa wameingia hadi wakati huo, alibaini kuwa kulikuwa na wenyeji wasiopungua watano, kwa jinsi walivyokuwa wakijishughulisha.
“Mbona uko kimya sana, naona unazungusha kichwa tu, vipi?” Sule alimshtua mpenzi wake wakiwa wamekaa pembeni ya ua huo, wamejitenga na wengine, mwanaume huyo akinywa bia na Mwani akiendelea na kinywaji chake.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Leave A Reply