The House of Favourite Newspapers

Chongo – 30

0

Ilipoishia wiki iliyopita
Naye alimchukulia Sule kama muuaji mwingine aliyestahili kufa sawa na Jerry. Alimtazama alipokuwa akitembea kulifuata jengo hilo na kupotelea ndani.
Sasa endelea..
Hakutaka kujishughulisha naye kwa sababu alijua anakoenda. Akiwa amesimama kwenye ngazi kusubiri lifti, mara macho yake yakamuona mtu akija kwa mbali ambaye alimfahamu, Twaha!
Twaha naye alimuona, kila mmoja akatoa tabasamu na walipokaribiana, wakakumbatiana na kushikana mikono kusalimiana.
“Eee bwana kwanza hebu njoo nikuoneshe kitu halafu tuendelee,” Twaha alimwambia Sule huku akimuongoza nje.
“Unamuona yule mshkaji?” Twaha alimwambia Sule huku akimuonesha Bata aliyekuwa amegeukia upande mwingine.
“Ndiyo nimemuona,” Sule alijibu huku akimshangaa mwenzake, ambaye alimuongoza tena kuingia ndani ili waendelee na shughuli zao!
“Huwezi kuamini, yule dogo ana historia ya kusisimua sana, pale unapomuona ni Mungu tu, ilibaki kiduchu afe. Kuna jamaa alishirikiana na dada yake walitaka wamuue ili wamdhulumu mali. Waliamini wamemuua, wakaenda kumtupa porini, lakini akapona aisee. Inasemekena anamsaka jamaa alipize kisasi,” Twaha alimwambia Sule.
Isingekuwa Sule aliwahi kuwa askari, tena wa idara maalum, Twaha angeweza kuona mshtuko mkubwa ndani ya mwili wake, lakini kazi hiyo ilimsaidia kuuficha mshtuko, ambao kwa kiwango kikubwa ulikuwa ni wa furaha, maana wamempata kirahisi mtu ambaye alipaswa kuondolewa duniani ili kuwafanya Jerry na mkewe waishi kwa amani.
Walibadilishana maneno mawili matatu na kuahidiana kuonana jioni maana alikuwa na safari ya kwenda pale walipokutana siku ile, kwani mwenyeji wake alishakubaliana naye.
Lakini kabla hawajaachana, Sule alimuuliza Twaha kama anamfahamu kwa kiwango kikubwa yule dogo, kwani simulizi yake imemvutia kiasi cha kutosha.

“Simjui kwa sana, maana pale alipo amepoteza kumbukumbu ya mambo mengi sana, sijui hata akimuona huyo jamaa aliyetaka kumuua kama atamkumbuka,” Twaha alisema, kitu kingine ambacho kilimfurahisha Sule, ambaye alimpa mkono, wakaagana, akapanda lifti hadi ofisini kwa Jerry.
Alipofika kwa Jerry, baada ya kusalimiana, alimshangaza alipomweleza kuwa amemuona na kumtambua kijana wanayemtafuta na hakuwa mbali kutoka pale walipo.
Moyo wa Jerry ukalipuka kwa hofu na kwa mshtuko, akajikuta ameinamia mezani kuupa mwili nguvu mpya. Kitendo cha kuambiwa kuwa adui yake alikuwa hatua chache kutoka pale alipo, kilimpa wakati mgumu sana na hakumwelewa Sule.
“No, usiwe na presha. Yupo nje anaendelea na shughuli zake na wala sidhani hata kama anajua upo hapa. Aliyeniambia na kunionyesha ni yuleyule mshkaji Twaha uliyenikutanisha naye kule Sinza.
“Mimi wakati nashuka hapo nje sijamuona, sasa nimeingia ndani natafuta lifti, kaniibukia na akanitoa nje na kunionesha hako ka bwa mdogo, kwa mujibu wa maelezo yake, dogo amepoteza kumbukumbu, naona kipigo ulichompa kilimharibu ubongo,” Sule alimwambia Jerry, kauli ambayo kwa mbali ilimshusha presha.
Bata akageuka kuwa ajenda, kikao chote kikawa kinamjadili yeye. Sule alipomtaka watoke nje ili amuone Bata, Jerry alimuonesha hofu ya dhahiri.
“Hapana Sule, leo hapana, wewe nenda kama utamuona uanze kazi mara moja, tunatakiwa kujua anakoishi na mazingira yake, ili ikibidi tumalize kazi mara moja,” Jerry alisema.
**
Bata alisubiri kwa dakika tano baada ya Sule kuingia ndani, kisha naye akatoweka eneo lile, akili yake ya ziada ilimuonya kuwa eneo lile halikuwa salama, akaondoka moja kwa moja hadi ofisini kwa mpenzi wake Ellina, pale katikati ya jiji.
Akiwa pale, akamwelezea jinsi alivyomuona Sule akiingia ofisini kwa Jerry. Akaonyesha pia hisia zake kuwa haoni kama eneo lile ni salama kwake, lakini Ellina akamtoa hofu kwamba isingekuwa rahisi kwao kumjua.

“Hapana, mimi naona tukutane na wadau wetu Jully na Mwani tupange namna ya kuifanya hii kazi haraka, maana naona kama tunaweza kuwahiwa, sina amani kabisa aisee,” Bata alimweleza mpenzi wake.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Leave A Reply