The House of Favourite Newspapers

Meja Jenerali Msuya; Alivyokufa na Kufufuka – 04

0

MEJA ALIYEKUFA (2)

Meja Jenerali Mstaafu Msuya.

Ilipoishia wiki iliyopita
kulikuwa kumetokea uzembe kwa upande wa manesi kwani baada ya tukio la kwanza la kushuka kwa kisukari, wasingeondoka karibu ya kitanda changu.
Walipewa onyo kwa kitendo hicho. Kwa upande wa madaktari, utawala wa hospitali ulipaswa kuweka daktari wa zamu wa kuwahudumia watu waliokuwa wamelazwa hapo, na ninavyofahamu, huo ndiyo ulikuwa utaratibu wa siku zote.  Hata hivyo, upendo wa Mungu ulitawala.

Niliendelea kupata matibabu vyema hospitalini hapo na baada ya siku kumi niliomba nikatibiwe nyumbani, hivyo niliruhusiwa kuondoka hospitalini si kwa vile nilikuwa nimepata nafuu, bali kwa vile nilihisi ningepata matibabu mazuri zaidi nyumbani kuliko hospitalini.

mejaMeja Jenerali Mstaafu Msuya.

Nikiwa nyumbani, nilitafutiwa mtaalam makini kutoka Hospitali ya Muhimbili ambaye angejikita zaidi katika kutafuta chanzo na tiba ya uvimbe niliokuwa nao. Siku iliyofuata nilikwenda huko na kukutana na mwanaume mmoja mzee aliyekuwa amevalia vizuri.

Alinikaribisha katika maabara na kunifanyia kipimo kingine cha ‘Fine Needle Aspiration’ kwenye uvimbe mkubwa zaidi.  Matokeo yalipokuja, yakawa yaleyale, kwamba ‘uvimbe huo haukuwa na matatizo yoyote makubwa.’

Baada ya kupata matokeo hayo Hospitali ya Muhimbili, nilikwenda moja kwa moja Hospitali Kuu ya Kijeshi ya Lugalo kumwona Dk. Mwanjela, daktari wangu wa siku zote.  Tuliyajadili matokeo ya vipimo hivyo na tiba yangu kwa kina na kuamua kwamba nilipaswa kwenda kufanya kipimo cha MRI ambacho kingefichua zaidi picha halisi ya uvimbe huo.
Wakati huo, mwanangu mkubwa zaidi, Bisala, aliyekuwa Uingereza,  mdogo wake, Roderick, kutoka Tanga na dada yake, Annie, kutoka Marekani, walikuwa wamewasili nchini, hivyo nilikwenda nao Muhimbili.

Nilikuwa nimepata kundi kubwa la watu waliokuwa wakinitakia afya njema, wakiwemo wanangu wapendwa. Huko tulipokelewa na daktari yuleyule mzee mnadhifu.  Alitayarisha vifaa husika na baada ya maelekezo, aliniambia nilale katika mashine maalum kama kitanda chenye kusogea, akakiwasha kwa umeme.

Nilibakia katika mashine hiyo kwa muda mrefu, nafikiri niliweza hata kupitiwa usingizi kwa kuchoka, kisha akanitoa.
Baada ya kuzichunguza kwa makini picha nilizokuwa nimepigwa, aliniambia kwamba uvimbe huo haukuwa na madhara. Majibu hayo yalinikasirisha sana hivyo nikaamua kujichukulia mambo mkononi.
Kutoka Muhimbili tulikwenda moja kwa moja Makao Mkuu ya Wizara ya Ulinzi kumwona Mkuu wa Majeshi (CDF), Jenerali Davis Mwamunyange, nimweleze kuhusu maradhi yangu na kumwomba msaada.  Wakati huo alikuwa bado hajawasili ofisini kwake, hivyo tuliamua kukaa humo na kumsubiri.

Nilikuwa nimedhamiria kumweleza kila kitu kwa vile nilijua hali ilikuwa mbaya lakini majibu niliyokuwa napewa yalikuwa hayaendani na hali halisi.  Alipofika, aliniambia alikuwa hajajulishwa kwamba nilikuwa mgonjwa. Nilimjibu kwamba mfumo wa kumpasha habari ulikuwa na kasoro au nilikuwa nimepuuzwa kwa vile nilikuwa jenerali mstaafu.
Nilimwomba nikatibiwe nje ya nchi kwa kuwaruhusu madaktari wanielekeze nikatibiwe Uingereza ambako nilijua madaktari  wangenipatia huduma thabiti na bora zaidi.
Tulibishana kwa hoja kwa muda kidogo kwa vile alikuwa na mawazo kwamba India ingekuwa mahali bora zaidi kwangu na kwake kutokana na bajeti iliyokuwepo.    Nilisisitiza nikatibiwe Uingereza kwani niliwahi kuutembelea Ubalozi wa Tanzania huko nyuma mnamo miaka ya mwisho ya 1980, jambo ambalo lilinipa fursa ya kuwafahamu wataalam wengi bora wa magonjwa.  Kwa Upendo wa Mungu, alikubali na akafanya uamuzi huo mgumu.
Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi ijayo.

Leave A Reply