Chongo!-4

Ilipoishia wiki iliyopita

Alipoomba ufafanuzi zaidi, akaambiwa atoe maoni yake kama anadhani yeye mwenyewe anaweza kusimamia mali za marehemu baba yake, au ateuliwe mtu wa kuifanya kazi hiyo kusubiri wamalize masomo!

Songa nayo…

Ame aliwaambia ndugu zake waliokuwa katika kikao kuwa, angeomba ateuliwe mtu wa kuwasimamia kwa kuwa wakati huo wakiwa shuleni, watashindwa kuangalia mali zao na pia kuchanganya vitu viwili kwa wakati mmoja. Ndugu wakamuelewa, wakajadiliana na kumteua shangazi yao kuwa msimamizi wa mirathi.

Moja ya sifa za shangazi huyo ni kuwa alikuwa mtu wa karibu sana wa marehemu na isitoshe, mwenyewe pia alikuwa mjasiriamali, hivyo ikahisiwa kuwa angeweza kuzitunza mali hizo bila kuzifuja. Wiki moja baada ya mazishi, ndugu waliondoka nyumbani na kuwaacha Ame na mdogo wake, pamoja na ndugu wawili watatu waliobaki kwa ajili ya kuishi nao ili kuwapa kampani.

“Hivi unafikiri tutaendelea kuishi hivi hadi lini, nadhani hutaki tuoane.” Jerry alimwambia Ame, siku hiyo walipotoka kwa ajili ya chakula cha mchana, ufukweni mwa bahari, eneo la Coco.

Jerry alikuwa ni mpenzi wake wa muda mrefu, tangu akiwa kidato cha pili huku yeye akiwa hana kazi, baadaye mwanaume huyo alipata kazi halmashauri ya  manispaa na kufanikiwa kuwa na mshahara mzuri. Leo, Ame akiwa amemaliza kidato cha sita, Jerry alishajijenga, akiwa na nyumba eneo la Tabata akiendelea na kazi.

“Siyo kama sitaki Jerry, haya mambo yapo tu, una haraka gani? Kwani wewe hutaki na mimi nijijenge?” Ame alimjibu mwenziwe, miguu yao ikiwa inagusana.

“Ujijenge? Nadhani una mtu mwingine, mtu una mali zote hizo unasubiri ujijenge nini, si utaendeleza mali ya baba yako?” Jerry aliuliza akiwa amekasirika kidogo kutokana na maneno ya mpenzi wake, ambaye alimjibu kuwa asingeweza kutegemea urithi wa mali za baba yake kwa sababu hazikuwa zake peke yake, bali na ndugu yake.

“Oke! Nafikiri wewe endelea na kujijenga, mimi acha nitafute mwanamke mwingine, huwezi kunifanya mjinga,” Jerry alisema kwa hasira huku akisimama na kuondoka, akijua wazi lazima Ame angemfuata, kwani alimpenda sana.

Na kweli, saa mbili usiku simu ya Jerry iliita na alipotazama akaliona jina la Ame, alipopokea msichana huyo akaomba wakutane ili wajadili tena suala lao. Kijana akakubali na baada ya mabishano mengi hatimaye wakakubaliana kuwa wafanye jambo hilo lenye neema kwa muumba wao.

Wakapanga kulizungumza jambo hilo kwa ndugu zao siku chache kabla ya Sikukuu ya Krismasi, wakitegea kuwa siku hiyo ya kumbukumbu ya kuzaliwa Kristo, iwe ndiyo ya kuvishana pete ya uchumba ili kusubiri taratibu zingine muhimu ziendelee.

Habari hizo zilipokelewa kwa shangwe kubwa na ndugu wa pande zote mbili na waliamini wawili hao wakioana, watafanya jambo la msingi, kwani ni vijana wasomi, ambao ni wapenzi wa muda mrefu.

Siku tatu kabla ya Krismasi, Jerry alikuwa amekaa kwenye bustani na mpenzi wake maeneo ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Wakiwa wanakunywa juisi ya matunda, Jerry akavunja ukimya.

“Ame, kuna jambo moja muhimu nataka kukuambia, kukubali au kukataa kwako kutakuwa na maana mbili, kuharibu au kuboresha uhusiano wetu,” alisema huku akimtazama Ame, aliyeshtushwa na maneno hayo.

JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS UPATE HABARI KEMKEM ZA UCHAGUZI MKUU

globalbreakingnews.JPG


Loading...

Toa comment