The House of Favourite Newspapers

Chongo!-5

0

Ilipoishia wiki iliyopita

Hofu ya Bata ikapungua. Alikuwa anamfahamu shemeji yake, mpenzi wa dada yake Ame. Wakati anajiandaa kumsalimia, kitu kisicho cha kawaida kwake kikatokea!

Sasa endelea…

Jerry akatoa kisu, akiwa amekishika mkono wa kulia, ule wa kushoto kidole kikapita katikati ya mdomo, ishara ya kumtaka kukaa kimya. Mwili wa Bata ukafa ganzi na kama shemeji yake angetambua mapema, wala asingetumia nguvu kubwa kama alivyofanya.

Baada ya kujiridhisha na kazi yake, akauchukua mwili wa Bata na kuuingiza kwenye nyumba ile iliyokuwa inaendelea kujengwa, bahati nzuri kwake hadi wakati huo hakukuwa na mtu aliyemuona. Akammwaga kwenye kona, kisha akaondoka kumfuata Ame, aliyekuwa na wasiwasi mwingi nyumbani.

“Nimemaliza kazi, njoo na gari pale njiani tumbebe,” Jerry alimwambia Ame huku naye akiwa na wasiwasi mkubwa, akatoka na kutangulia kwenye ile nyumba na dakika tano baadaye, Ame aliegesha gari na kushuka. Wakaingia ndani na kuubeba mwili wa mdogo wake, wakauweka katika siti ya nyuma ya gari, wakaufunika shuka waliyokuwa nayo.

Jerry akarudi tena ndani ya nyumba, akatifuatifua mchanga ili kuchanganya damu iliyotapakaa, akarejea garini kisha wakaondoka zao taratibu kama wasio na hatia yoyote. Wakaingia barabarani, wakaingia kuelekea Bagamoyo, Ame akakanyaga mafuta, kasi ya gari ikamtisha hadi yeye mwenyewe!

Walipofika Bagamoyo, pale kwenye mzunguko, wakaingia barabara ya kushoto iendayo Msata. Waliendelea na kasi ileile hadi njia panda ya njia iendayo katika mbuga za wanyama ya Saadan, wakakata kulia kuifuata. Katika kijiji kimoja kinaitwa Makaani, wakaingia porini na kuutupa mwili wa Bata!

**

Noel na mkewe walikuwa nyumbani kwa mwenyekiti wa kijiji asubuhi asubuhi wakitaka aende akawaoneshe shamba lao, maana kila mara wamekuwa wakikosa nafasi ya kwenda kutokana na kutingwa na shughuli nyingi kazini kwao. Jumapili hiyo ilikuwa ndiyo fursa, wakaamua kuitumia vizuri.

Na kwa kuwa walishazungumza tangu jana yake, hakushangaa aliposikia watu wakibisha hodi asubuhi ile, akawafungulia mlango na kuwakaribisha, kisha akawaomba japo dakika tano apate kupiga mswaki. Alipomaliza, akaingia garini na kuongozana na wageni wake kuwaonesha walichohitaji.

Wakaingia njia nyembamba ya gari iliyokuwa ikipita katikati ya pori, wakaendesha kama dakika tano akawaambia wasimame.

“Sasa hili ndilo shamba lako bwana Noel, kuanzia hapa unakwenda upande huu ni hatua mia tatu hamsini, maana yake ni heka tano, na kwa kwenda huku mbele, ni hatua 140, yaani heka mbili. Unaweza kuweka alama au kama utalikumbuka basi kazi kwako,” mwenyekiti wa kijiji, Babu Masta alimweleza.

Noel alionesha tabasamu huku akimshika bega mkewe, halafu akampelekea mkono wa kumshukuru mwenyekiti, kwani siku zote alitamani sana apate shamba, angalau dogo, ili aweze kulima kuenzi kazi ambayo baba yake kule kijijini kwao alipenda sana kufanya.

Akauliza kama wangeweza kulizunguka kwa gari shamba hilo, akaambia haiwezekani, hivyo akamuomba mzee huyo apate kumzungusha kidogo ndani ya eneo lake, apate kuweka alama mbili tatu za kuweza kumkumbusha.

Katika miti mikubwa, Noel alipulizia rangi maalum aliyokuja nayo kwenye kichupa na kuandika herufi za jina lake na la mkewe, akafanya hivyo katika maeneo mengi na aliporidhika wakarejea ndani ya gari ili kuanza safari ya kurudi. Mwenyekiti akamweleza kuwa anaweza kuendelea mbele kwani ipo njia inayotokeza barabarani, ambako yeye akifika, atashuka na wao wataendelea na safari yao ya kurejea mjini.

Wakaingia garini na kuanza safari kidogo kidogo huku Noel akimwelezea mipango yake ya kuliendeleza shamba lake. Ghafla, Noel akashikwa bega na mwenyekiti.

“Hebu simama, mbona kama mtu yule, au?” Mwenyekiti huyo alimsemesha Noel huku akimuonesha kwa kidole eneo la pembeni kidogo ya barabara. Wote wakatumbua macho, wakashuka lakini mkewe Noel akakataa kusogea upande ule.

Noel na Babu Masta wakaanza kusogea taratibu, wakaona kama mtu aliyefunikwa shuka, wakasogelea na kubaini kuwa alikuwa ni mtu, lakini kijana mdogo. Ni Bata.

Damu zilikuwa zinavuja maeneo mbalimbali ya mwili wake. Kwa jinsi walivyomuangalia, walishindwa kujua kama amekufa au yu hai.

Bila kuambizana, wakambeba, wakamwingiza kwenye gari, wakamlaza kiti cha nyuma, wakaondoa gari hadi barabarani, wakakubaliana kumuacha mkewe Noel, ili Mzee Masta aongozane na Noel kuelekea Polisi.

Leave A Reply