The House of Favourite Newspapers

Niliolewa na mganga kwa tamaa ya cheo kazini-26

0

ILIPOISHIA:

Baada ya kufika kwenye hoteli iliyokuwa na hadhi ya nyota tatu, tulitafuta meza ya pembezoni na kukaa kisha tuliagiza chakula. Baada ya chakula kuletwa tulianza kula huku nikiwa na shauku ya kuujua huo ubuyu. Lakini Safia alinieleza nipunguze pupa, tule kwanza baada ya chakula tulikuwa na muda wa kutosha wa mazungumzo.

SASA ENDELEA…

Sikumbishia, tulikula kwa muda wa nusu saa kama ujuavyo ulaji wa kike, tunashika chakula kama tunakiogopa. Baadaye tulipata muda wa kuzungumza huku nikiwa na hamu ya kujua nini kimejiri ndani ya  mchakato wa kupata jina la mtu mmoja.

“Eflazia,” Safia aliniita huku akifuta midomo yake kwa kitambaa baada ya kumaliza kunywa funda la juisi.

“Abee,” niliitika huku nikikaa vizuri na kumtazama kama maneno yake yanaonekana kama sinema.

“Si unajua kuna ushindani mkubwa  katika uteuzi wa jina la kwenda kusoma?”

“Najua.”

“Unakumbuka nilikwambia nini kuhusiana na sifa za waombaji?”

“Ulinieleza hakuna anayenifikia sifa kama zangu na nafasi ile ni yangu.”

“Hiyo ilikuwa siku ya kwanza, baada ya hapo nilikueleza nini?”

“Uliniambia kuna binti mmoja aliye mkoani kwenye moja ya matawi yetu ameleta CV yake, lakini bado hakuwa na elimu kama yangu japokuwa alikuwa na elimu kuwashinda wote waliotangulia.”

“Sasa shoga kuna kitu nilikisia Jumatano, meneja wa kanda akizungumza na mkurugenzi  yalinitia mashaka.”

“Ulisikia nini?” nilijikuta nikishindwa kuvumilia.

“Yaani hawa wakubwa wana mambo ya kijinga sana.”

“Niambie shoga ulisikia nini?”

“Nilimsikia mkurugenzi akimwambia  meneja wa kanda kuwa mtu wake ajiandae kwa safari ambayo alitakiwa asafiri baada ya wiki tatu.”

“Safari! Safari gani?” nilimsikia lakini nilishindwa kumwelewa.

“Ya kwenda kusoma.”

“Kwenda kusoma! Wapi?” bado sikuelewa.

“Jamani kwani wewe ulikuwa unataka kwenda kusoma wapi?”

“Ha! Sasa nani anaenda ikiwa uteuzi haujafanywa?”

“Jambo likishikwa na wakubwa wadogo hawana nafasi.”

“Ina maana wamekaa lini na wamechagua ikiwa kikao ni Ijumaa?”

“Wakae wapi, nafasi ile wamepeana wenyewe kwa wenyewe.”

“Unamaanisha kikao hakitakuwepo?”

“Kitakuwepo kwa mujibu wa bodi lakini kila kitu kimekwisha, baada ya kunasa mazungumzo yale nilithibitisha siku iliyofuata  baada ya kuiona tiketi na viza ya yule msichana.”

“Mungu wangu,” nilihisi kama mapigo ya moyo yakienda kasi.

“Eflazia mbona hivyo?” Safia alishtuka baada ya kuona mabadiliko yangu.

“We acha tu, yaani nilivyoipania safari hiyo halafu kuna washenzi wachache wamenizunguka siamini,” nilisema kwa uchungu.

“Eflazia kwani mzee wako vipi?”

“Kwa kweli yupoyupo si kama zamani.”

“Nina imani ungemshirikisha nafasi ungeweza kuipata.”

“Yaani wee acha, pozi lote limeisha hata sijui itakuwaje?”

“Kivipi?”

“Sijui ofisi nitaionaje?”

“Eflazia isikuumize sana kwa vile nafasi bado zipo.”

“Sawa zipo lakini kwa upande wa kazi yangu hii ilikuwa ya juu, kinachoniuma zaidi kuchaguliwa kwenda msichana aliyenikuta kazini, nimemzidi kwa kila kitu.”

“Juzi ndiyo nimeelezwa kumbe yule msichana alikuwa aolewe na meneja hivi karibuni lakini safari ya kwenda kusoma imesogeza mambo mpaka atakaporudi ndipo harusi ifungwe.”

“Mmh! Sawa nashukuru kwa ubuyu wako uliogeuka shubiri.”

“Basi shoga ni hayo yaani kila kitu kimeisha kilichobaki danganya toto tu.”

“Sawa shoga nashukuru.”

Kwa vile muda ulikuwa umekwenda tulirudi ofisini, nilipofika sikukaa sana niliamua kuondoka kwa hasira nilikuwa tayari kwa lolote. Nikiwa nyumbani nilijikuta nikikumbuka, nilitakiwa kupeleka majina ya watu wanaokuwepo kwenye bodi ya uteuzi.

Leave A Reply