The House of Favourite Newspapers

Colin Powell; Jenerali wa Jeshi Aliyeiongoza Marekani Kumng’oa Saddam Hussein

0

-Aliweka rekodi ya kuwa Mmarekani mweusi wa kwanza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje

– Akakataa kugombea urais na kumpendekeza George Bush na baadaye akampigia debe Barrack Obama

– Vita ya Iraq ya kumng’oa Saddam Hussein ikaja kuichafua historia yake

Colin Powell amefariki dunia Oktoba 18, 2021 akiwa na umri wa miaka 84 kwa kile ambacho familia yake imeeleza kuwa ni maambukizi ya Virusi vya Corona.

Powell ni miongoni mwa Wamarekani weusi wa kwanza kuaminiwa na na serikali ya Marekani na kupata nafasi ya kuitumikia serikali na jeshi kwa miaka mingi, akishika nyadhifa mbalimbali za juu, kuanzia mshauri wa rais kuhusu masuala ya kijeshi, Mkuu wa Majeshi hadi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Historia inaonesha kwamba Collin Powell alizaliwa April 5, 1937 katika kitongoji maarufu cha Harlem jijini New York kutoka kwa  baba Luther Powell na mama Maud Powell ambao walikuwa ni wahamiaji kutoka nchini Cuba. Alikulia katika kitongoji kingine maarufu cha South Bronx jijini New York na alisomea katika Chuo cha City College of New York.

Baadaye alijiunga na mafunzo ya kijeshi ambapo katika moja ya mahojiano yake na Kituo cha Runinga cha CNN, Powell amewahi kunukuliwa akisema alikuwa akivutiwa mno na nidhamu iliyokuwepo ndani ya jeshi na alikuwa akijisikia ufahari kuvaa magwanda ya Jeshi la Marekani.

Alihitimu mafunzo ya kijeshi mwaka 1958 ambapo baada tu ya kuhitimu, Powell aliajiriwa rasmi na Jeshi la Marekani. Katika kipindi cha mwanzo cha utumishi wake jeshini, Powell alikuwa miongoni mwa wanajeshi wa Marekani waliopelekwa katika Vita ya Vietnam mwanzoni mwa miaka ya 1960.

Akiwa huko, alinusurika kupoteza maisha mara mbili, ambapo katika tukio la kwanza, alijeruhiwa vibaya wakati akiwaokoa wanajeshi wenzake wawili kufuatia helikopta yao ya kijeshi kupata ajali.

Baada ya kumalizika kwa vita hiyo, Powell alirejea nchini Marekani ambako aliendelea kulitumikia jeshi na baadaye, akajiunga tena na chuo cha kijeshi cha National War College. Uwezo mkubwa aliouonesha kuanzia jeshini mpaka vitani, ulimfanya apande vyeo harakaharaka hadi kufikia ngazi ya Brigedia Jenerali akiwa na nyota nne begani mwaka 1979.

Sifa hizo zilimvutia aliyekuwa rais wa wakati huo, Ronald Reagan ambaye alimteua kuwa mshauri wa rais wa masuala ya usalama kuanzia mwaka 1987 hadi 1989.

Wadhifa huo haukuwahi kushikiliwa na mtu mweusi kabla yake, akaingia kwenye rekodi ya kuwa Mmarekani mweusi wa kwanza kushikilia wadhifa huo.

Baada ya Rais Reagan kumaliza muda wake na kuingia Rais George H.W Bush au Bush mkubwa, mwaka 1989 alimteua Powell kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakuu wa Majeshi, Joint Chiefs of Staff, cheo ambacho pia hutafsiriwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Marekani mpaka mwaka 1993.

Akaweka rekodi nyingine ya kushika wadhifa huo akiwa na umri mdogo zaidi na kwa mara nyingine kuwa Mmarekani mweusi wa kwanza kushika wadhifa huo.

Akiwa Mkuu wa Majeshi, Powell aliiongoza Marekani kushinda katika vita mbalimbali. Ya kwanza ilikuwa ni Vita ya Panama mwaka 1989 iliyomuondoa madarakani Jenerali Manuel Norieg.

Vita nyingine kubwa, ilikuwa ni Vita ya Ghuba, Gulf War ambayo Marekani iliipa jina la Operation Desert Storm mwaka 1991. Katika vita hii, Iraq ilikuwa imeivamia Kuwait kimabavu na jukumu la Marekani likawa ni kwenda kumuondoa Saddam Hussein na majeshi yake ndani ya ardhi ya Kuwait, jambo ambalo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Baada ya kumalizika kwa vita hiyo, umaarufu wake uliongezeka mno nchini Marekani kiasi cha baadhi ya watu kuanza kutabiri kwamba huenda akaja kuwa rais wa kwanza mweusi wa Marekani.

Umahiri wake katika vita ya Ghuba, ulimfanya atunukiwe tuzo kadhaa za heshima na umaarufu wake ukazidi kuongezeka. Rais Bush alikuwa akimsifia mara kwa mara kutokana na ushindi uliopatikana kwenye vita hiyo na baadaye akatunukiwa tuzo ya heshima na rais huyo, ambaye alimsifu kwa jinsi alivyowaongoza wanajeshi wa Marekani vitani.

Powell aliendelea kulitumikia jeshi mpaka mwaka 1993 alipostaafu rasmi kutoka jeshini. Baada ya kustaafu utumishi wake jeshini, Powell alikuwa akitajwa kama mtu sahihi anayepaswa kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1996 kwa tiketi ya Chama cha Republican.

Hata hivyo, mwenyewe alikataa nafasi hiyo kwa kueleza kwamba hakuwa na wito wa kuitumikia Marekani katika nafasi ya kisiasa. Katika uchaguzi mkuu uliofuatia, mwaka 2000 bado hamu ya Wamarekani wengi ilikuwa ni kumuona akiwania urais lakini kama ilivyokuwa mwanzo, alikataa na badala yake, akapendekeza George Bush mdogo ndiyo agombee.

Mawazo yake hayo, yalipokelewa na wengi na akaendelea kumpigia kampeni Bush mdogo na hatimaye akashinda urais mwaka 2000. Kama shukrani kwake, baada tu ya kutangazwa kuwa Rais wa 43 wa Marekani, Bush mdogo alimteua Powell kuwa Waziri wa mambo ya Nje. Kwa mara nyingine tena akaweka rekodi ya kuwa Mmarekani mweusi wa kwanza kushika wadhifa huo.

Miezi michache tangu alipoingia madarakani, ndipo kwa mara ya kwanza Marekani ilipotingishwa na shambulio kubwa la kigaidi la Septemba 11, 2001.

Kutokana na uzoefu wake katika masuala ya diplomasia na masuala ya kijeshi, Rais Bush alimteua kuongoza vita dhidi ya ugaidi.

Ni Powell ndiye aliyekuwa ‘mastermind’ wa uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan kulisambaratisha Kundi la Al Qaeda na Taliban na kumsaka kinara wa shambulio hilo la kigaidi, Osama bin Laden.

Wakati vita dhidi ya ugaidi ikiendelea, ndipo lilipoibuka suala jingine la Iraq iliyokuwa ikiongozwa na Saddam Hussein, kudaiwa kuwa na silaha za maangamizi ya halaiki. Akihutubia Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa Februari 2003, Powell aliueleza ulimwengu kwamba Intelijensia za Marekani, zimethibitisha kwamba Sadam Hussein alikuwa na silaha hizo hatari.

Wiki sita baada ya hotuba hiyo ya Powell, ndipo majeshi ya Marekani yalipoivamia Iraq na kuisambaratisha Baghdad na hatimaye, Saddam Hussein akauawa.

Hata hivyo, miaka miwili baadaye ya majeshi ya Marekani kuivamia Iraq, ilikuja kuthibitika kwamba Saddam Hussein hakuwa na silaha za maangamizi ya halaiki na uvamizi huo haukuwa sahihi!

Hilo likawa doa kubwa kwa Collin Powell kwani ni yeye ndiye aliyeuaminisha ulimwengu kwamba Saddam Hussein alikuwa na silaha hizo. Inaelezwa kwamba, skendo hiyo, ndiyo iliyochochea Powell kuamua kujiuzulu wadhifa wake mwaka 2005.

Katika moja ya mahojiano aliyowahi kuyafanya baada ya kuondoka madarakani, Powell amewahi kunukuliwa akisema kwamba uamuzi wa kuivamia Iraq, ambao yeye ndiye aliyeutoa, ulikuwa ni doa kubwa kwenye historia ya maisha yake ambalo haliwezi kufutika.

Akizungumza na kituo cha runinga cha CNN katika mahojiano na mtangazaji Larry King mwaka 2010, Powell alinukuliwa akisema anajutia uamuzi wake huo kwa sababu haukuwa sahihi.

Baada ya kuondoka madarakani, Powell alirudi kuishi maisha yake ya kawaida na inaelezwa kwamba mwaka 2008, alibadili msimamo wake wa kukiunga mkono chama chake cha Republican na kuhamia chama cha Democrat ambacho Barack Obama alikuwa akiwania urais kupitia chama hicho.

Powell alimuunga mkono Obama kwa nguvu zote mpaka alipofanikiwa kuingia madarakani na kuwa rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo. Aliendelea kukiunga mkono Democrat hata baada ya Obama kuingia madarakani ambako katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2016, alikuwa akimuunga mkono mwanamama Hillary Clinton.

Baada ya mwanamama huyo kuangushwa na Donald Trump, Powell alionesha kukasirishwa sana na kitendo hicho na kueleza kwamab Trump hakuwa na sifa za kuiongoza Marekani, msimamo ambao alikuwa akiutoa hadharani.

Aliendelea kuwa mkosoaji mkubwa wa Trump katika kipindi chote cha utawala wake na katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, alikuwa akimuunga mkono rais wa sasa, Joe Bidden ambaye alifanikiwa kumwangusha Trump.

Marehemu Powell alifunga ndoa mwaka 1962 na Alma Vivian Johnson ambaye wamepata naye watoto watatu.

Na huyo ndiyo Collin Powell, jenerali wa jeshi aliyeiongoza Marekani kumng’oa Saddam Hussein.

Leave A Reply