The House of Favourite Newspapers

Corona: Hakuna Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu

0

VIKAO vya Bunge la bajeti kuu vinavyoanza leo Machi 31, 2020, huku utaratibu mpya ukiwekwa juu ya tahadhari ya Corona ambapo wataruhusiwa kuingia wabunge 150 pekee ukumbini tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai alisema kutokana na tahadhari ya Ugonjwa unaotokana na virusi vya corona (COVID-19) idadi ya wabunge watakaokuwa wakiingia ukumbini ni wasiopungua 150 kati ya wabunge 393.

 

Amesema kwa kawaida vikao vya Bunge huhudhuriwa na zaidi ya watu 700 ukumbini ikijumuisha na watumishi wengine bungeni hivyo kutokana na tahadhari ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona wabunge wengine watakuwa wanafuatilia kupitia Mitandao na watagawanyika katika kumbi mbalimbali zilizopo bungeni.

 

Aidha, Ndugai alisema masaa ya vikao vya bunge yamepunguzwa ambapo vikao vyote vya bunge vitakuwa vinafanywa kwa masaa yasiyozidi manne kuanzia saa nane mchana hadi saa kumi jioni isipokuwa siku ya leo.

 

Kuhusu Maswali na Majibu bungeni, Ndugai alisema wabunge watakuwa wanapata fursa ya kuuliza maswali kupitia Mtandao wa Bunge hivyo hakutakuwa na Maswali ya ana kwa ana pia Maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri mkuu hayatakuwepo.

 

Katika kupiga kura za Ndiyo au Hapana kuhusu kupitisha bajeti, Ndugai amesema kura hizo zitapigiwa kupitia mtandaoni ambapo pia amebainisha kuwa Waziri mwenye dhamana husuka atalazimika kujibu swali akiwa anatumia kipaza sauti (mic) cha kwenye kiti alichokalia na hatolazimika kuchangia kipaza sauti kimoja kwa Mawaziri wengi kama ilivyokuwa awali.

 

Ikumbukwe kuwa katika bunge hili la Bajeti kuu Jumla ya Maswali 525 yatakuwepo ambapo mkutano huo unaanza Machi 31 ,2020 hadi Juni 30, 2020 Bunge litakapovunjwa kwa ajili ya Uchaguzi mkuu 2020.

Leave A Reply