The House of Favourite Newspapers

Corona: Mwanri Aagiza Wanaofundisha ‘Tuisheni’ Wasakwe

0

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, ameagiza kuwasakwa kwa walimu ambao wamekuwa wakiwakusanya wanafunzi kwa ajili ya kufundisha tuisheni (masomo ya ziada) kwa kuwa wanapingana na kampeni ya kudhibiti na kupambana na ugonjwa wa Covid -19 unaotokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

 

Hatua hiyo inalenga kuzuia vitendo hatarishi vinavyoweza kuwepo na mazingira ya kupata virusi vya Corona.

 

Mwanri alitoa kauli hiyo wilayani Nzega wakati wa kukagua vituo na zahanati zilizoandaliwa kwa ajili ya washukiwa wa ugonjwa huo kama itatokea bahati wakaonekana mkoani humo.

 

Alisema ni marufuku kwa walimu kutumia janga la ugonjwa wa Covid -19 kujipatia maslahi kwani  kufanya hivyo ni kuvunja sheria kwa kisingizio kuwafundisha watoto masomo ya ziada.

 

Mwanri aliongeza kuwa baadhi ya wamiliki wa shule binafsi ndiyo wanasababisha walimu kujiingiza kwenye ufundishaji wa tuisheni baada ya kuambiwa kuwa hatawalipa mshahara kwa sababu hawakufundisha katika kipindi ambacho shule zimefungwa kutokana na Covid -19.

 

Alisema hilo halikubaliki na ndiyo linalowafanya baadhi yao kujiingiza katika ufundishaji wa tuisheni kinyume cha maagizo ya serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo. Aliongeza kwamba lazima walimu wote walipwe mishahara yao ili kutowaweka katika vishawishi vya kujiingiza katika kuvunja maagizo ya serikali ya kuzuia mikusanyiko kwa wanafunzi.

 

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Honaratha Rutatinisibwa, aliwataka wazazi kutowaruhusu watoto wao kuzuzura ovyo mitaani kwa kuwa vitendo hivyo vinaweza kuwasababisha kupata maambukizi ya virusi vya Corona.

 

Alisema kuna baadhi ya maeneo yanaonekana makundi ya watoto wakiwa wamekusanyika, jambo ambalo ni hatari kwao na kwa jamii zinazowazunguka, akaongeza kwamba ni vyema wanafunzi wakasisitizwa kubaki majumbani katika kipindi hiki ambacho mapambano dhidi ya Corona yakiendelea.

Leave A Reply