The House of Favourite Newspapers

Dakika 450 za hatari Yanga

KIKOSI cha Yanga ambacho kimeanza Ligi Kuu Bara msimu huu kwa kichapo, kina dakika 450 mbele za hatari, ambazo ni sawa na mechi tano.

 

Yanga ambayo bado inaendelea na michuano ya kimataifa ikiiwakilisha Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika ina kibarua cha kupambana na Zesco ya Zambia katika hatua ya kwanza kusaka nafasi ya kutinga makundi lakini ikiwa na mechi nyingine za ligi zinafuatana.

 

Mechi hizo ni dhidi ya Zesco watakazocheza mbili, pamoja na tatu za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City, Prisons na Polisi Tanzania. Hizi ni mechi hatari kwa sababu, kwanza kati ya mechi tano, nne ni ugenini na zote Yanga haina rekodi nzuri kwao.

Ukiachana na mchezo wa Yanga na Zesco ambao wa kwanza utapigwa hapa nchini na mwingine ugenini, Yanga watakuwa na wakati mgumu watakapovaana na Polisi Tanzania ambayo inafundishwa na kocha Suleimani Matola, ambaye msimu uliopita katika mechi tatu Matola akiwa na Lipuli alishinda mbili na Yanga kushinda moja.

 

Hata hivyo, msimu huu tena Matola ameshakutana na Yanga kwenye mchezo wa kirafiki akiwa na Polisi na walishinda 2-0.

Pamoja na kwamba msimu uliopita Yanga walishinda dhidi ya Prisons na Mbeya City, lakini hii imekuwa michezo migumu sana kwa timu hiyo ya Jangwani. Yanga kwanza itaanza kuvaana na Zesco Septemba 14, hapa nyumbani ambapo watarudiana Septemba 28.

 

Pia itawavaa Mbeya City, Septemba 18, halafu itacheza na Prisons Septemba 21, baada ya hapo itakwenda Zambia kuwavaa Zesco Septemba 28, halafu Oktoba 20, itaivaa Polisi Tanzania.

Stori: Marco Mzumbe

Comments are closed.