The House of Favourite Newspapers

Dar: Watumishi Watatu wa Serikali Wakutwa na Dawa za Kulevya

0

TAARIFA YA KAMISHNA JENERALI WA MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA GERALD MUSABILA KUSAYA KWA WANAHABARI TAREHE 19 JUNI, 2021

OPERESHENI YA UKAMATAJI WA DAWA ZA KULEVYA KWA MWEZI JUNI

Ndugu Wanahabari
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!

 

Nimewaita leo tuzungumze kutokana na matukio yaliyojitokeza katika kipindi cha mwezi mmoja ulipita wa Juni mwaka huu, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama tumefanikiwa kukamata kilo 99.33 za dawa za kulevya katika matukio tofauti zikihusisha watu nane (8) kati yao watatu (3) wakiwa ni watumishi wa Serikali.

 

Mtakumbuka kuwa, tarehe 16 mwezi Juni, 2021 nilizungumza nanyi kuwataarifu juu ya kukamatwa kwa Kilo 88.27 za dawa za kulevya zikiwa ndani ya gari aina ya Toyota Prado namba T503 DHC ikiwa imetelekezwa barabarani katika eneo la Kimara Korogwe mkoani Dar es Salaam, na nikawaambia kuwa tunaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.

 

Ndugu wanahabari,
Kama nilivyo waahidi kuwa nitawataarifu juu ya matokeo ya uchunguzi; Katika uchunguzi uchunguzi wetu tulibaini kuwa, kati ya kilo 88.27 zilizokamatwa wakati ule kuna dawa nyingine ziliibiwa, na baadhi ya watumishi wasio waaminifu walishiriki kwenye uharifu huo.

 

Hivyo, tarehe 18 Juni, 2021 katika eneo la Mburahati Madoto NHC wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, tulifanikiwa kuwakamata mume na mke ambao ni JAMAL SAID NANGATUKILE (45) kabila Mmakonde, na MARIYAMU RASHID BACHA (28) kabila mburushi wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin yenye uzito wa gramu 494.52. Tarehe 19 Juni katika eneo la Bunju Beach tulimkamata aliyekuwa askari Polisi F.6763 CPL DEODATUS LEONID MASSARE (37) kabila Mrangi akiwa na kilo 1.04 ya dawa za kulevya aina ya heroin.

 

Aidha, tarehe 21 Juni 2021 katika maeneo ya Mivinjeni wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, tulimkamata Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ANDREW WAILES PAUL (45) kabila Muha, mkazi wa Kurasini na wenzake SAID RASHID MGOHA (45) maarufu kama Kindimu kazi yake fundi gereji kabila Mkwere mkazi wa mtoni kijichi, GEORGE DAVID MWAKANG’ATA (38) kabila Mnyakyusa, mfanyabiashara Mkazi wa Mtoni Kijichi, wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha kilo 1.02.

 

Terehe 23/06/2021, tulimkamata Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ALLY JUMA ALLY (32) kabila Mzaramo, mkazi wa Kinyerezi mkoani Dar es Salaam pamoja na ABUBAKAR JUMA ABDALL (28) kabila Mshiraz, mfanyabiashara wakiwa na dawa za kulevya aina ya Methamphetamine yenye uzito wa gramu 597.61, Aidha, katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwa ALLY maeneo ya Zimbili Kinyererezi, kulipatikana pesa taslimu Tsh. 82,043,000 na USD 5100.

 

Ndugu wanahabari,
Watuhumiwa wote wameshafikishwa mahakamani wakikabiliwa na makosa ya kujihusisha na usafirishaji na biashara ya dawa za Kulevya makosa ambayo ni Uhujumu Uchumi kwa Sheria za Nchi yetu. Pamoja na hatua hii tuliyofikia bado tunaendelea na uchunguzi ili kuwabaini waharifu wengine walioshiriki katika tukio hilo.

 

Natoa onyo wa wale wanaotaka kujaribu makali ya Serikali kwa kuendeleza au kujihusisha na biashara hii haramu, ninawaonya waachane na biashara hii na badala yake wajikite katika biashara na shughuli nyingine halali za kujiongezea kipato. Mamlaka tuko macho usiku na mchana, tutawakamata katika siku wasiyoijuana watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

 

Pia niwaombe ndugu zangu waandishi kuendelea kutumia kalamu zenu kuwapa elimu a watanzania na jamii kwa ujumla kuhusu madhara yatokanayo na biashara na matumizi ya dawa za kulevya, kwani janga hili tusipolighughulikia katika umoja wetu tutaua nguvu kazi ya taifa letu. ‘

Tuleteeni taarifa tu, sisi tutaifanyia kazi kikamilifu na kufanikiwa kuondokana na janga hili.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

Leave A Reply