The House of Favourite Newspapers

‘Dhuluma’ Ya Madam Rita! Tunajenga Taifa Linalochekelea Anguko La Watu

0

APRILI 8, mwaka huu ilikuwa siku mbaya mno kupata kutokea kwa Mkurugenzi wa Benchmark Productions, Rita Paulsen ‘Madam Rita’.

Ni siku ambayo mmoja wa washindi wa Shindano la Bongo Stars Search (BSS) 2019, Meshack Fukuta aliibuka na madai mazito kuwa hajalipwa shilingi milioni hamsini za ushindi wake.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza ndiye aliyesimamia shoo ya kumkaanga Madam Rita.

Ni kitendo cha kama dakika 45 tu, lakini kilitosha kabisa kuporomosha umalkia wa Madam Rita alioujenga kwa miaka 20.

Siku hiyo Waziri Shonza alifanya kazi kubwa mbili; moja kumpigania Fukuta kwa nguvu zote na pili kumshusha kileleni Madam Rita kwa nguvu zote.

Kila upande siku hiyo ulijua kuwa Waziri Shonza alifanya kazi kubwa kwake.

Fukuta akafukuta kweli hasa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ni shujaa aliyejitolea kuutafuna mfupa mgumu wa kusema ukweli kuhusu Shindano la BSS.

Madam Rita naye alionja machungu ya ‘udhulumati’ anaodaiwa kuufanya kwa Fukuta na hakika mwanamke huyo aligeuka kutoka shujaa hadi kuwa tapeli wa mjini.

Ukipita kwenye mitandao ya kijamii utaona jinsi ambavyo Madam Rita alivyodhalilika.

Ukijiuliza ndiyo iliyokuwa shabaha ya waziri huyo mdogo kwa Madam Rita ambaye mbali na kujihusisha na sanaa inayogusa jamii, bado ni mwanamke mwenzake ambaye amepambana miaka 20 kujenga nembo ya kampuni yake ya Benchmark Productions ambayo ndiyo ilikuja kuendesha Shindano la BSS.

Nafikiri Waziri Shonza hakulenga hivyo, kilichotokea baada ya kitendo chake cha kuwasilisha mauzauza ya BSS 2019, kilivuka malengo yake, tofauti na hapo waziri atakuwa na jambo lake kubwa zaidi ya alichokifanya na hilo nitamwachia mwenyewe.

Nitajadili hoja mbili; ya kwanza ni wajibu wake kama waziri kuhakikisha haki inatendeka kwa watu wote ikiwepo ya Fukuta kulipwa chake.

Kama waziri alichokifanya hakikuwa na makosa hata kidogo; shida ilikuwepo kwenye uwasilishaji wake, ulimbembesha dhambi kubwa Madam Rita.

Tafsiri yangu; ni kwamba aliua ili kutoa haki ya kijana mmoja ambaye ni Fukuta.

Je, Maadam Rita anastahili kifo ili Fukuta apate haki yake ya shilingi milioni hamsini?

Fukuta anafaa kuwa ALFA NA OMEGA wa vijana wote Tanzania? Hii ni hoja yangu ya pili ambayo nimepanga kuijadili kwenye makala haya.

Kwa herufi kubwa nasema NO! Fukuta si nembo ya vijana wa Tanzania, ni sehemu ndogo mno ya vipaji vya wasanii chipukizi kwenye nchi hii.

Sababu; Madam Rita amekuwa msaada kwenye tasnia ya muziki kwa wasanii wengi mno tangu alipoanzisha Benchmark Productions.

Ukikumbuka video nzuri ya mwanamuziki Profesa Jay iitwayo Zali la Mentali ya mwaka 2003; sifa mpe Madam Rita, kampuni yake ndiyo iliyotengeneza video hiyo ambayo hadi leo ukiitazama ina msisimko wa aina yake.

Hakuna ubishi kwamba Madam Rita amefanya kazi kubwa kwenye nchi hii, BSS imebadilisha maisha ya vijana wengi, imeamsha hamasa ya watu kuhusu muziki kwa mlango wa mbele au wa nyuma.

Inawezekanaje mema yote aliyoyafanya mwanamke huyu yakazimwa na tukio moja, tena ambalo amekiri kuwa Fukuta hajamlipa na kwamba anahaha kutafuta fedha ili ampe haki yake.

Ni Madam Rita huyuhuyu aliyeweza kumlipa mshindi wa BSS, Jumanne Idd mwaka 2006, Misoji Nkwabi (2008), Paschal Cassian (2009), Mariam Mohamed (2010) na Haji Ramadhani 2011.

Mwaka 2012 alimlipa Walter Chilambo haki yake, akampa zawadi yake Emmanuel Msuya 2013 na 2015 Kayumba Juma hakulalamika kutokulipwa.

Ni wazi linapojitokeza jambo baya kwa mwanamke huyu kuna akili ya tatu lazima itafute majibu ya ziada kuliko kuwahi kumlaumu na kumuona kama mtu asiyefaa kwenye jamii.

Tunafikisha ujumbe gani kwenye jamii yetu kuhusu watu wanaojitoa kusapoti jamii yetu na kuisadia Serikali kupanua uwanja wa ajira pale tunapokuwa wepesi kuzika mema 1000 kwa kosa moja?

Nafikiri siyo sawa, tunatakiwa kuwa Taifa linalofurahia zaidi mafanikio ya watu kuliko kuchekelea anguko lao!

Kasumba hii ndiyo ambayo inawafanya watu wengi wanaofanya mema mengi kwenye nchi hii kutothaminiwa na badala yake wanasubiriwa wafe au waanguke ndiyo igeuzwe kuwa agenda kwenye mitandao ya kijamii. Hii si sawa!

Fukuta alistahili kusaidiwa kupata haki yake na Madam Rita alitakuwa kusaidiwa kumlipa mshindi huyo bila kuvunja heshima yake mbele ya jamii.

Baada ya Fukuta bado Taifa linakwenda mbele, kuna vijana wengi wanahitaji kutoka kisanii kupitia BSS.

Wapo wasanii wengi nyota wanasubiri daraja la BSS ili waweze kuvuka kwenda kwenye mafanikio yao.

Kama jamii hatutakiwi kuua mashujaa kwa ajili ya kuwaponya waoga; kwa kauli hii nisitafsiriwe vibaya, imejaa falsafa ni wenye akili tu ndiyo wanaoweza kunielewa!

MAKALA: RICHARD MANYOTA, BONGO

Leave A Reply