The House of Favourite Newspapers

Baba Diamond: Nikifa Diamond usinizike!

0

BABAD
Baba mzazi wa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Abdul Jumaa.

MAYASA MARIWATA NA CHANDE ABDALLAH

BABA mzazi wa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Abdul Jumaa amekuwa akisema mengi mazito juu ya mwanaye huyo lakini safari hii ni kama ‘yamemfika hapa’ kufuatia kauli yake kwamba, siku akifa staa huyo asimzike, Ijumaa limezungumza naye kwa takriban dakika 45.

Akizungumza kwa njia ya simu huku akionekana kutokuwa na matumaini ya mwanaye huyo kumsamehe, Mzee Abdul alieleza kuwa amefikia hatua ya kusema hayo kutokana na ukweli kwamba haoni faida ya kuwa na mtoto anayeitwa Diamond.

“Kwa anayonifanyia ni vyema ajihesabie tu kwamba hana baba, amenidhalilisha sana, sasa kama ameshindwa kunijali na kunisaidia nikiwa hai, nikifa kutakuwa na faida gani kuja kunizika?” alihoji mzee huyo.

diamond-23.jpgNasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

KUMBE SIYO DIAMOND TU

Mzee huyo ambaye kwa sasa afya yake si nzuri akisumbuliwa na miguu bila msaada wowote wa kimatibabu aliendelea kusema kuwa, siyo Diamond tu kwani hata mwanaye mwingine, Mwajuma Abdul ‘Queen Darleen’ ambaye naye ni msanii wa Bongo Fleva ameungana na kaka yake.

“Sioni faida ya watoto hawa ambao hawana msaada kwangu, hata Mwajuma (Queen Darleen) tangu apewe gari na kaka yake amezidi kunitupa, hivyo bora nikae nikijua sina watoto kuliko kuwa na watoto mastaa halafu hawana msaada kwangu.

“Kwa hiyo nasema nimechoka kabisa, sioni faida ya mtu kuja kunizika nitakapokufa wakati nipo hai hanijali, hakuna kitu kinachoniumiza kama pale ninaposikia Diamond anasaidia watu baki wakati mimi baba yake nateseka.

“Nimekuwa nikimtumia sms lakini hajali na hata nikimpigia hapokei, mbaya zaidi nikitembea watu wananinyooshea vidole kuwa baba fulani yule, nimechoka.

“Juzi nilimtumia sms Diamond nikamwambia ajihesabie kuwa hana baba kutokana na mateso ya mguu ninayoyapata na ugumu wa maisha.

“Lakini anashindwa kunipeleka kutibiwa! Sina shida ya kumlazimisha na pesa zake, nilimwambia anipeleke hospitali nitibiwe lakini kashindwa, cha ajabu nilivyomtumia hiyo sms juzi akanijibu: “Ahaa…baba upo… hujambo” na kuendelea kuuchuna.

 “Kama anasema kuna msaada ananipa mpigie mumuweke loud speaker aseme, mimi siwataki tena hao watoto watajijua wenyewe na maisha yao kwa sababu nimeshamwambia Diamond anipe pesa nifungue hata biashara ya mitumba lakini wapi hanijibu chochote.

“Hivi kuna kosa gani kubwa nililokosa mpaka nishindwe kusamehewa? Sioni kosa langu na kama lipo nini cha kumfanya mtu ashindwe kunisamehe nikae nateseka hivi? Siyo siri nateseka sana, mguu unanitesa na pesa ndiyo hivyo sina,” alimaliza kusema mzee huyo kwa uchungu.

MADHARA YA MANENO YAKE

Watu wenye busara waliozungumza na gazeti hili juu ya kauli ya mzee huyo walisema kuwa, kuna uwezekano mkubwa kama ikitokea akafariki dunia na Diamond akalisogelea jeneza lake yatamkuta makubwa.

“Unajua kwa maneno kama hayo endapo Diamond atakaidi, yanaweza kumkuta makubwa. Anachotakiwa kukaa chini na mzazi wake na kusameheana, kama mzazi anafikia hatua ya kusema hayo, basi yamemfika shingoni. Kwa maneno hayo makali lazima Diamond aishi akiwa na hofu,” alisema Mzee Shaban wa Sinza jijini Dar.

DIAMOND ANASEMAJE?

Kufuatia maneno hayo mazito, Ijumaa lilifanya jitihada za kumtafuta Diamond kupitia simu yake bila mafanikio lakini mara kadhaa anapoulizwa juu ya tofauti yake na mshua wake anasema, amemsamehe na maisha yanaendelea kama kawaida.

Leave A Reply