The House of Favourite Newspapers

Djuma: Tunalibeba, Andaeni Suti Za Ulaya

Kaimu kocha mkuu wa Simba, Masoud Djuma.

 

KAIMU kocha mkuu wa Simba, Masoud Djuma amesema kuwa kikosi alichonacho kinatosha sana kutwaa Kombe la SportPesa Super Cup bila hata msaada wa Emmanuel Okwi au John Bocco.

 

Mashabiki wa Simba wamekuwa wakihofia kutokuwepo kwa wachezaji hao pamoja na rekodi ya kutinga fainali bila kufunga bao lolote ndani ya muda wa kawaida wa mchezo.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Djuma amesema; “Ninashangazwa sana na watu kuendelea kuniuliza juu ya kikosi changu kama nitawaongeza kina Okwi na wengine wote ambao tuliwatumia kwenye ligi na sasa hawapo.”

 

“Naomba niwaambie kuwa kikosi hiki ni kipana na nina imani mazoezi ninayowapatia watashangaza wengi wakati tunanyanyua kombe na kulirudisha Tanzania.

 

“Tumejipanga kikamilifu kuonyesha maajabu hayo na ndio maana utaona wachezaji wangu wote wako na morali ya kutosha kwa ajili ya mchezo huo hivyo mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi,”anasisitiza Kocha huyo ambaye habari za ndani zinasema kwenye michuano ya Kagame ataiongoza timu akisaidiwa na nahodha wa heshima wa Simba, Seleman Matola.

 

Simba imeachana na Kocha wao, Mfaransa Pierre Lechantre ambaye Spoti Xtra lilikuwa la kwanza kufichua siri zinazomng’oa Msimbazi ambazo ni pamoja na kiburi cha kutotaka kuambiwa ukweli pamoja na kushinikiza mshahara wa Sh.milioni 90 kwa mwezi. Kwa uchambuzi wa kina soma ukurasa wa 22 na 23.

STORI NA MUSA MATEJA, NAKURU

 

Comments are closed.