The House of Favourite Newspapers

Dk. Shein Aongoza hitma ya Kumuombea Dk. Badriya

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj, Dk. Ali Mohamed Shein ameongoza hitma ya kumuombea Dk. Badriya Abubakar Gurnal mke wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Sadala (Mabodi) iliyofanyika katika msikiti Maamur Upanga jijini Dar-es-Salaam.

 

Katika hitma hiyo, iliyohitimishwa na Sheikh Zain Sharif na dua yake kutolewa na Sheikh Ayoub Ali Seif wote wa msikiti Maamur, viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali walihudhuria pamoja na wana familia wakiwemo ndugu, jamaa na marafiki.

Baada ya hitma hiyo, akitoa neno la shukurani kwa niaba ya familia mjomba wa Marehemu alitoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein kwa ushiriki wake na kuungana pamoja na wanafamilia hao katika kisomo hicho.

 

Aidha, alitoa shukurani kwa wote waliohudhuria hitma hiyo na kutumia fursa hiyo kumuelezea Marehemu jinsi alvyokuwa mtu mwema, mwenye hikma na hulka aliyekuwa akifuata maadili ya Kiislamu sambamba na maadili ya kazi yake ya Udaktari.

Mapema Alhaj Dk. Shein akiwa na Mama Mwanamwema Shein walifika nyumbani kwao Marehemu Mikocheni jijini Dar-es-Salaam kwa ajili ya kutoa mkono wa pole kwa ndugu, jamaa watoto pamoja na mume wa Marehemu Dk. Badriya.

 

Akiwa nyumbani kwao Marehemu Rais Dk. Shein na Mama Mwanamwema Shein walitia saini kitabu cha Maombolezi kufuatia kifo cha Marehemu Badriya Gurnal.

Baada ya tukio hilo Rais Dk. Shein pamoja na Mama Mwanamwema Shein walitoa mkono wao wa pole huku Rais Dk. Shein akiwaomba wana familia wakiwemo ndugu, jamaa, watoto pamoja na mume wa marehemu kuwa na moyo wa subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba.

 

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alieleza jinsi alivyomfahamu Dk. Badriya katika maisha yake yote pamoja na utendaji wake wa kazi uliotukuka tokea Rais Dk. Shein akiwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya ambapo pia, aliwaomba wanafamilia kuzidi kuendelea kumuombea dua Marehemu.

Comments are closed.