The House of Favourite Newspapers

Dkt. Biteko Ashiriki Misa Takatifu Ya Kumwombea Hayati Dkt. John Pombe Magufuli Chato

0
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko Machi 17, 2024 amejumuika na viongozi na wananchi mbalimbali katika misa Takatifu ya kumwombea Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mt. Yohana Maria Muzeyi, wilayani Chato mkoani Geita.

Akitoa Salaam za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Biteko amesema kuwa, Dkt. Samia na Serikali yake inaendelea kumkumbuka Hayati Dkt. John Pombe Magufuli si tu kama Rais katika Serikali Awamu ya Tano, bali pia kama kiongozi aliyeweka misingi mbalimbali ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuitekeleza.

Mjane wa Hayati Magufuli, Mama Janeth Magufuli.

Ametaja miradi mbalimbali ambayo ilianzishwa katika Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inaendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ni pamoja na mradi wa umeme wa Julius Nyerere ( JNHPP) ambao sasa umeshaanza kuzalisha megawati 235, mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam ambao tayari umeshaanza kufanyiwa majaribio na ujenzi wa Daraja kubwa la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza ambao umefikia asilimia 80.

Dkt. Biteko amewahakikishia Watanzania kuwa, masuala yaliyobuniwa na Hayati Magufuli yanaendelea na yataendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa na Serikali ya Awamu ya Sita ili kuendelea kumuenzi kwa vitendo.

“Hayati Magufuli anasifika kote duniani kwa uwezo wake wa kiongozi, karama ya kutatua matatizo ya wananchi, kuwasikiliza wananchi, kuondoa kero, uzembe, ubadhirifu, rushwa na kuhimiza uwajibikaji serikalini, nataka niwahakikishie kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayasukuma masuala yote hayo ili kutoa huduma kwa ufanisi kwa watanzania.” Amesisitiza Dkt. Biteko

Kwa upande wake, Mjane wa Hayati Magufuli, Mama Janeth Magufuli amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa pamoja na familia hiyo tangu kifo cha Hayati Magufuli ambapo pia amewashukuru viongozi waliojumuika na familia katika adhimisho hilo la misa Takatifu, akieleza kuwa hiyo ni alama ya upendo kwa familia hiyo.

MAGUFULI ALIJUA ATAFARIKI – ALIWAITA WACHUNGAJI WAMSALIE SALA ya MAREHEMU WODINI – MABEYO ASIMULIA

Leave A Reply