The House of Favourite Newspapers

DROO KUBWA SHINDA NYUMBA WASHINDI DINNER SET KICHEKO!

0
Kahabi Sulemani (kushoto) akikabidhiwa zawadi ya dinner set na Ofisa Usambazji wa Global Publishers, Jimmy Haroub.

WASHINDI watatu wa Dinner Set, waliopatikana wakati wa uchezeshaji wa droo kubwa ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, leo Jumatano wamepewa zawadi zao katika hafla fupi iliyofanyika katika ofisi za Global Publishers, zilizopo Sinza Mori jijini Dar es Salaam.

Washindi hao ni Melenia Swai, mkazi wa Mbezi Tangibovu, aliyekabidhiwa zawadi yake na Keffa Masaga ambaye ni mmoja wa maofisa wa Global Publishers, Kahabi Sulemani wa Vingunguti aliyepewa vifaa vyake hivyo na Jimmy Haroub huku Philemon Faustin wa Temeke Wailes ambaye akikabidhiwa mzigo wake na Mr Shinda Nyumba, Julius Charles.

Washindi wakiwa katika picha ya pamoja na timu ya usambazaji ya Global Publishers.

Wakizungumza wakati wa utoaji wa zawadi hiyo, washindi hao walitoa shukurani zao kwa waandaaji wa bahati nasibu hiyo, Global Publishers ambao wanafanya mambo makubwa kuliko kampuni zingine za magazeti.

Melania, ambaye hii ni mara yake ya pili kushiriki bahati nasibu hiyo, alisema alifurahi sana alipopata habari za ushindi wake, kwani awali, hakufanikiwa kwa sababu wakala aliyekuwa akimpa kuponi zake, anahisi hakuwa akimpelekea kuponi zake kwa wakati.

“Pale mwanzo kuna kaka mmoja hivi wakala nilikuwa nampa kuponi zangu, kila siku asubuhi nanunua na kukapa nampa, lakini nadhani alikuwa hapeleki kwa sababu siku moja nilivyoenda, nikakuta zimeanguka chini, nilipomuuliza mbona hakuzipeleka akawa anajiumauma tu.

 

Kutoka kushoto ni washindi, Merania Swai, Kahabi na Philemon Faustin wakiwa na zawadi zao.

“Safari hii nikaanza kujaza na kuzipeleka mimi mwenyewe, nimefurahi sana kuona nimeshinda hivi vitu japo sijashinda nyumba, lakini nawasihi wasomaji wenzangu ambao hawakupata zawadi kubwa kutokata tamaa, ipo siku tutafanikiwa.

“Mimi ni msomaji mzuri wa magazeti ya Ijumaa, Wikienda, Amani, Risasi na Uwazi na huwa ninavutiwa sana na hadithi za Shigongo (Eric) na machombezo mengine yanayoandikwa, pia hata habari za mastaa pia ninavutiwa nazo sana,” alisema mwanamama huyo.

Merania Swai akiwa na zawadi yake.

 Kwa upande wake, Kahabi ambaye awali alikuwa hapatikani kwenye simu yake, lakini akafanikiwa kupatikana Jumatano asubuhi, alisema awali hakuamini alipoambiwa ameshinda, kwani alijua ni mmoja wa watu wake wa karibu alikuwa akimtania.

“Halafu akaniambia ofisi zetu zimehama na leo ndiyo tunatoa zawadi, nikaona isiwe kesi, nikapanda gari breki ya kwanza kwenye ofisi za Global za zamani, nikakuta patupu hamna watu, nilipouliza nikaambiwa wamehama, ndipo nilipoamini kuwa ni kweli nimeshinda.

“Mimi bado kijana ndiyo kwanza ninaanza maisha, nitatumia vyombo hivi katika kujiweka sawa kwani vitanisaidia wakati huu ninapojiandaa kukabiliana na changamoto za maisha.

Merania Swai akikabidhiwa zawadi yake na Ofisa Usambazaji, Keffa masaga.

“Mimi ni msomaji mzuri wa gazeti la Championi, kila siku likitoka huwa silikosi, nimefurahi sana kupata zawadi hii kwani licha ya kusoma na kuburudika na habari, lakini leo ninapata nyongeza ya vyombo, hili ni jambo kubwa sana,” alisema kijana huyo aliyejiweka wazi kuwa yeye ni shabiki kindakindaki wa Wekundu wa Msimbazi, Simba.

Kwa upande wake, Philemon Faustin, ambaye pia ni shabiki wa Simba, alisema amefarijika sana kupata zawadi hiyo, kwani angalau imemfuta machozi kwa kutopata zawadi kubwa.

 

Philemon akielezea furaha yake wakati alipokuwa akihojiwa na mtangazaji, Isri Mohammmed.

“Ile mara ya kwanza nilikuwa nacheza lakini sikuwa siriaz, maana wakati mwingine nilikuwa natuma na mara zingine situmi, lakini tulipoanza mwaka huu tangu mwanzo nilikuwa nanunua kila Championi linapotoka, nashukuru sana kwa zawadi hii,” alisema Philemon.

Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili ambayo imechezeshwa kwa zaidi ya miezi sita, ilifikia tamati Septemba 27 mwaka huu kwa droo kubwa iliyofanyika katika viwanja vya Las Vegas, Mabibo jijini Dar es Salaam.

Mr. Shinda Nyumba akimkabidhi Philemon zawadi yake.

Katika droo hiyo, George Majaba wa Dodoma alishinda nyumba hiyo na sasa atakabidhiwa mwishoni mwa mwezi huu, shughuli ambayo itasindikizwa na hafla fupi ofisini na baadaye nyumbani kwake, Bunju B nje kidogo ya jiji.

Na Mwandishi Wetu.

Leave A Reply