The House of Favourite Newspapers

DROO KUBWA SHINDA NYUMBA… KESHOPKUTWA MJENGO UNAMPATA MWENYEWE

0

ILE droo kubwa ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, sasa imebakiza saa 48 tu, kuweza kumpata mwenyewe katika tukio litakalofanyika keshokutwa Jumatano katika Viwanja vya Las Vegas vilivyopo Mabibo, mkabala na Soko la Ndizi jijini Dar es Salaam.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Global Publishers, Abdallah Mrisho ambayo ndiyo inaendesha zoezi hilo kubwa kabisa kufanywa na kampuni ya habari hapa nchini, alisema jana, kuwa, kila kitu kimekamilika na hivi sasa kilichobaki ni kusubiri siku tu ya tukio ifike ili mshindi wa mjengo huo uliopo Bunju B, Dar uweze kumpata mwenyewe.

Wasomaji wote ambao bado hawajawasilisha kuponi zao, wanatakiwa kufanya hivyo haraka iwezekanavyo, kwa kuzipeleka kwa mawakala wa Magazeti ya Global Publishers waliopo nchi nzima au kwa wakazi wa Dar es Salaam kuzipeleka moja kwa moja ofisini kwao, Bamaga Mwenge.

Nyumba hiyo ni ya kisasa yenye vyumba vitatu vya kulala, kikiwemo kimoja ambacho ni master bed room.

Licha ya vyumba hivyo vitatu, ndani ya mjengo huo pia kuna sebule, chumba cha maakuli, jiko na vyoo ndani, kitu ambacho kitamfanya mmiliki wake akiingia ndani, awe ameingia. Lakini kitu cha kufurahisha zaidi kuhusu nyumba hii ni kwamba mmiliki wake, ambaye atakuwa ni yule atakayeibuka mshindi katika droo kubwa ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, hatakuwa na sababu ya kuhangaika kuweka umeme, kwani atakuta umeingizwa tayari kwa matumizi.

“Lengo letu siku zote ni kurejesha faida kidogo tunayopata kwa jamii tunayofanya nayo kazi, ndiyo maana tumeingia gharama kubwa kuijenga nyumba hii iwe ya kisasa, ili mtu atakayebahatika kuipata, abadili kweli maisha yake na hiyo ndiyo kauli mbiu yetu, kubadili maisha ya watu.

“Ni nyumba ya kisasa kwa vigezo vyote, vyumba vitatu vya kulala, sebule kubwa, chumba cha chakula, jiko, choo na bafu, vyote hivyo vitapatikana ndani ya nyumba, mmiliki wake atakabidhiwa hati ya kiwanja na ataukuta umeme umeingia. Kazi yake itakuwa ni kuweka luku tu ili aendelee na huduma hiyo,” alisema Meneja Mrisho.

“Tumekamilisha kila kitu, kilichobakia sasa ni kuwaomba wasomaji wa magazeti yetu ya Ijumaa Wikienda, Amani, Uwazi, Risasi, Championi na

Ijumaa kukata kuponi zao za mwishomwisho na kuzituma kwetu haraka iwezekanavyo. Kwa wale wa mikoani, kuponi zao wazipeleke kwa wakala wetu ambao wako kila sehemu nchini.

“Kwa wale wa Dar, wazilete kuponi zao katika ofisi zetu zilizopo Bamaga-Mwenge, Dar na wazikabidhi kwa watu maalum wanaozipokea. Huu ni wakati wa kuhakikisha hawakosi nakala zao kwa vile muda umeshaisha. Wiki mbili zilizobaki wahakikishe hakuna mtu anayeziacha kuponi zake bila kuzileta kwetu, kwa sababu huenda ile utakayoiacha nyumbani, ndiyo iliyokuwa ya mshindi,” alisema Mrisho.

Nyumba hiyo ya kisasa imejengwa Bunju B, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwa na thamani ya mamilioni ya shilingi na itakuwa ni ya pili kutolewa na Global Publishers, kwani katika bahati nasibu ya kwanza iliyofanyika mwaka jana, mjengo wa aina hiyo ulitolewa.

Aliyeshinda katika bahati nasibu hiyo ya kwanza alikuwa ni mwanamama mjasiriamali, Nelly Mwangosi, mwenyeji wa mkoani Iringa ambaye mjengo wake upo eneo la Salasala, pia nje ya Jiji la Dar.

Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili inafanyika baada ya kuwepo kwa droo ndogo tano zilizochezeshwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ambako zaidi ya wasomaji 30 wa Magazeti ya Championi, Ijumaa, Risasi, Uwazi, Amani na Ijumaa Wikienda, waliibuka na zawadi za aina mbalimbali zikiwemo pikipiki, televisheni kubwa, simu za kisasa za mikononi, dinner set na ving’amuzi.

Shinda Nyumba; Washindi wa Pikipiki, Televisheni, Simu Kukabidhiwa

Leave A Reply