The House of Favourite Newspapers

DROO KUBWA SHINDA NYUMBA MJENGO MPYA UPO BUNJU B

0
Nyumba aliyoshinda Nelly Mwangosi.

WAKATI siku ya kuchezesha droo kubwa ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili ikizidi kukaribia, imebainika kuwa mjengo ambao mshindi atapata, umejengwa maeneo ya Bunju B, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Ofisa Masoko wa Global Publishers, ambayo ndiyo inayoendesha bahati nasibu hiyo, Keffa Masanga, alisema jana kuwa nyumba hiyo ya kisasa, imejengwa eneo hilo, njia inayoelekea Mabwepande.

“Ni bonge la mjengo kwa kweli, mtu atakayebahatika kuupata, atakuwa amepata kitu kikubwa sana katika maisha yake,” alisema ofisa huyo.

Naye Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho aliwataka wasomaji wa magazeti ya Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Risasi, Amani, Championi na Uwazi kupeleka kuponi walizozikata kwa mawakala wa magazeti walio kila pembe ya nchi, sambamba na kupeleka katika ofi si zao zilizopo Bamaga, Mwenge jijini Dar es Salaam.

“Ninachoweza kuwaambia wasomaji wa magazeti yetu ni kuwa tumeshamaliza vikwazo vilivyokuwa vinatukabili, droo yetu kubwa itachezwa mwezi huu katika siku ambayo tutawaeleza hapo baadaye kidogo, tuendelee kufuatilia katika kurasa za magazeti yetu tutajua lini hii shughuli itafanyika,” alisema Mrisho.

Mrisho aliwataka wasomaji kuendelea kukata kuponi katika magazeti, zinazopatikana katika kurasa za ndani za kila gazeti la Global Publishers, ambayo huuzwa kwa shilingi mia tano tu ambayo ni Championi, Ijumaa Wikienda, Risasi, Amani na Uwazi na lile la Ijumaa ambalo huuzwa kwa shilingi elfu moja, lakini likiwa na kuponi mbili.

Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili inafanyika baada ya kuwepo kwa droo ndogo tano zilizochezeshwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ambako zaidi ya wasomaji 30 waliibuka na zawadi za aina mbalimbali zikiwemo pikipiki, televisheni kubwa, simu za kisasa za mikononi, dinner set na ving’amuzi.

Droo hizo ndogo zilifanyika katika maeneo ya Dar Live Mbagala, Manzese Bakhresa, CCM Mwinjuma Mwananyamala na Mabibo Soko la Ndizi, matukio ambayo yalihudhuriwa na mamia ya wasomaji.

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa kampuni hiyo kuchezesha bahati nasibu na kutoa zawadi ya nyumba baada ya mwaka jana kufanya hivyo ambapo mjasiriamali kutoka Iringa, Nelly Mwangosi alijipatia zawadi hiyo kubwa kabisa ambayo imebadili kabisa maisha yake ambayo sasa yamekuwa bora zaidi.

Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili imedhaminiwa na kampuni ya Premier Bet.

Leave A Reply