The House of Favourite Newspapers

Ewura Yatoa Ufafanuzi Kuhusu Kushuka Bei za Mafuta

0

KATIKA siku za hivi karibuni, kumekuwepo na taarifa katika mitandao ya kijamii kuhusu kushuka kwa bei ya mafuta ghafi nchini Marekani, hali iliyosababisha watu kuanza kuhoji kwanini bei za mafuta hapa nchini hazishuki kwa kiwango kinachoonekana kushuka katika soko la Marekani.

 

Ufafanuzi ni kwamba; bei za mafuta nchini Marekani zinazotangazwa kupungua kwa kiwango kikubwa ni zile za mafuta ghafi (crude oil) na siyo mafuta yaliyosafishwa (refined petroleum products). Punguzo hili la bei linatokana na kukosa mahali pa kuhifadhia mafuta hayo nchini Marekani.

 

Ni vyema ikafahamika kuwa hivi sasa, Tanzania haina mitambo ya kusafisha mafuta (refineries), hivyo mafuta yanayoingizwa nchini ni yale yaliyosafishwa tu. Pia hakuna Hifadhi ya Taifa ya kuhifadhi mafuta kwa wingi.

 

Maghala yote yaliyopo nchini ni ya kampuni binafsi na yanauwezo wa kuhifadhi mafuta kwa matumizi ya ndani kwa takribani siku miamoja ishirini (120). Hata hivyo, Kanuni zinazosimamia biashara ya mafuta zinamtaka kila mfanyabiashara wa mafuta kwa jumla awe na hifadhi ya mafuta kwa muda wa siku zisizopungua kuminatano (15) kulingana na hisa zake katika soko.

 

Hata hivyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) inafanya mchakato wa kujenga maghala ya kuhifadhi mafuta.

 

Vilevile, kwa taratibu zilizopo, mafuta yanaingizwa nchini na mshindi wa zabuni za uagizaji mafuta kwa pamoja, ambapo kwa kiasi kikubwa; mafuta yanayoletwa nchini hutokea nchi za Uarabuni. Hivyo basi, kushuka kwa bei za mafuta Marekani kunaweza kusilete unafuu katika soko la Tanzania, kwa kuwa mafuta yetu yananunuliwa Uarabuni.

 

Hata hivyo; ikiwa mafuta hayo yatashuka katika Soko la Dunia (Uarabuni), itachukua kipindi cha miezi miwili ndipo watanzania waone faida.

Imetolewa na:
MKURUGENZI MKUU
22 Aprili, 2020

Leave A Reply