The House of Favourite Newspapers

Exclusive: Kingwendu Autamani Ubunge Tena!

0

UKISIKIA; “Aluuu kukuruka mwanangu, helohelo, tupate raha duniani!”

Hii ni saini inayomtambulisha komediani mkongwe Bongo, Kingwendu Ngwendulile.

Jina lake halisi ni Rashidi Mwinshehe. Amejizolea umaarufu kutokana na kipaji chake cha kuchekesha alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

Kingwendu ameshiriki filamu nyingi za vichekesho na waigizaji wengi kama Said Gamba ‘Mzee Small’ na Amri Athuman ‘Majuto’ ambao wametangulia mbele ya haki.

Filamu kama Old is Gold, Mchakamchaka, Utanibeba, Nyama Choma, Lugha Mseto, Askari wa Bushi, Mbuzi wa Shughuli, Faza Hausi na nyingine kibao ambazo zimempa mafanikio kwenye maisha yake.

Ukiachilia mbali uigizaji, Kingwendu amefanya ngoma kama Mipango Siyo Matumizi, Mwanalumango na Mapepe.

Gazeti la RISASI MCHANGANYIKO, limekaa mezani kwenye mahojiano maalum (exclusive) na Kingwendu ambaye amefunguka ishu nyingi, kubwa ikiwa ni kurudi kugombea Ubunge katika uchaguzi wa mwaka huu kama alivyofanya kwenye Uchaguzi Mkuu 2015.

RISASI MCHANGANYIKO: Kingwendu umekuwa kimya kwa muda mrefu, shida ni nini?

KINGWENDU: Ni kweli nimekuwa kimya kwa sababu sijatoa kazi mpya kutokana na kusafiri sana, ila kwa sasa kazi zangu zipo 15 na zinarushwa Azam TV.

RISASI MCHANGANYIKO: Unaizungumziaje sanaa ya uchekeshaji ya sasa ukilinganisha na zamani?

KINGWENDU: Utofauti upo mkubwa sana kwa sababu zamani msanii ukionekana kwenye televisheni, haraka sana anapata jina, hususan akifanya vizuri. Sanaa ya sasa hata ufanye nini, ni vigumu sana kupata jina.

RISASI MCHANGANYIKO: Kwa nini unasema ni vigumu kupata jina?

KINGWENDU: Kwa sababu imekuwa ni nyepesi mno, imekuwa shaghalabaghala, kila mtu amekuwa msanii.

RISASI MCHANGANYIKO: Uliwahi kuwaza kubadili staili yako ya uigizaji?

KINGWENDU: Hicho kitu huwa nakiwaza sana, maana naweza kuigiza filamu za serious pia, japo nikipata pesa nitaandaa filamu yangu ambayo iko tofauti na uchekeshaji ambao mashabiki wamezoea kuniona.

RISASI MCHANGANYIKO: Vipi kuhusu kuifanya sanaa yako kimataifa zaidi?

KINGWENDU: Napenda sana kufanya uchekeshaji na watu wa nchi za nje kama Nigeria na Kenya. Hiyo ni ndoto ambayo naiota muda mrefu.

RISASI MCHANGANYIKO: Je, uliwahi kufanya utaratibu wowote? KINGWENDU: Niliwahi kwenda Kenya, nikakutana na Kingwendu wa Kenya ambaye tumepanga kufanya kazi ya pamoja.

RISASI MCHANGANYIKO: Ni changamoto zipi unazopitia kwenye kazi yako hii ya uchekeshaji?

KINGWENDU: Changamoto kubwa kwangu ni mapromota, wananiita kufanya kazi na halipi. Niliwahi kudhulumiwa pesa zangu nikiwa Afrika Kusini mwaka 2016.

RISASI MCHANGANYIKO: Mafanikio gani unayojivunia kwenye kazi yako ya sanaa?

KINGWENDU: Mafanikio makubwa kwangu ni kupata umaarufu mkubwa. Kila kona nikipita najulikana na watu wanakubali kazi zangu ninazofanya.

RISASI MCHANGANYIKO: Janga la Corona limekuathiri kiasi gani kwenye kazi zako?

KINGWENDU: Janga hili limeniathiri sana kwa sababu nilikuwa nimeshajipanga kuachia kazi zangu, ila kutokana na hili janga, nimeshindwa kufanya chochote, imebidi niache kwanza hadi pale mambo yatakapokaa sawa.

RISASI MCHANGANYIKO: Mwaka 2015 uligombea Ubunge katika Jimbo la Kisarawe mkoani Pwani kupitia tiketi ya Chama cha CUF. Je, mwaka huu umejipangaje?

KINGWENDU: Ni kweli niligombea japo sikufanikiwa kupita, mwaka huu kama kawaida, lazima nigombee mpaka kieleweke.

RISASI MCHANGANYIKO: Je, utagombea kupitia CUF au utabadili upepo?

KINGWENDU: Hapana, sibadili chama, ni kilekile cha CUF.

RISASI MCHANGANYIKO: Kingwendu ni jina kubwa na linafahamika. Je, una mpango wa kutumia jina lako kibiashara kwa maana ya kuwa na bidhaa za jina lako?

KINGWENDU: Zamani nilikuwa nachukulia kawaida sana kufungua kampuni au kuwa na bidhaa za jina langu, ila kwa sasa hivi nimewaza sana, nimeona umuhimu wa kufanya hivyo, lazima nitafungua kampuni yangu mwenyewe.

RISASI MCHANGANYIKO: Tofauti na kazi ya uigizaji, unajishughulisha na nini?

KINGWENDU: Kwa sasa mimi ni mtangazaji wa redio. Nafanya kazi E-FM.

RISASI MCHANGANYIKO: Neno kwa mashabiki wako.

KINGWENDU: Mashabiki wangu wasione nipo kimya, wakadhani nimeacha sanaa, bado nipo na mambo mazuri yapo njiani yanakuja.

 

MAKALA | Khadija Bakari, Bongo

Leave A Reply