The House of Favourite Newspapers

Exclusive: Makala Banda; Humwambii Kitu Kwa Kiba, Roma

0

 

MSAKATA kabumbu wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Banda aliyekuwa anaichezea Highlands Park inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Afrika Kusini (PSL) kwa mara ya kwanza ameelezea mahaba yake juu ya muziki mtamu wa Bongo Fleva.

Kwenye eneo hilo, Banda anakiri kwamba humwambii kitu mwanamuziki mkubwa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘Kin Kiba’ na rapa mkali Bongo, Ibrahim Mussa ‘Roma’.

Ikumbukwe Banda ni shemeji wa Kiba kwani amemuoa dada yake, Zabibu Kiba.

Gazeti la IJUMAA limefanya mahojiano maalum (exclusive interview) na Banda ambaye anafunguka mengi kuhusu maisha yake ya ndoa na vitu vingine vingi;

IJUMAA: Ni staa gani wa muziki wa Bongo Fleva ambaye unamkubali?

BANDA: Ninamkubali sana Ali (Kiba). Ndiye mwanamuziki ambaye mara nyingi ninamfuatilia na kusikiliza ngoma zake.

IJUMAA: Mbali na Kiba ni msanii gani mwingine ambaye huwa unamfuatilia zaidi?

BANDA: Mbali na Ali, msanii mwingine ambaye huwa ninamfuatilia ni Roma, napenda sana mashairi yake.

IJUMAA: Hivi karibuni Roma alizua taharuki mitandaoni baada ya kusema kuwa mwaka 2021 atasimama kwa muda kufanya muziki, hili ulilipokeaje?

BANDA: Nadhani ni meseji ambayo Watanzania hawakuielewa, sidhani kama Roma anaweza akaacha muziki wakati ndiyo kazi inayomuingizia kipato.

Mfano kama mimi leo hii nikuambie kuwa ninaacha kucheza mpira, ni kitu ambacho hakiwezekani. Roma alisema anaacha muziki labda ni meseji ambayo aliitoa ya wimbo huu wa mwisho, lakini Watanzania wasitegemee kwamba Roma anaweza kuacha muziki kirahisirahisi.

IJUMAA: Ni kitu gani ambacho huwa kinakuvutia kwa Zabibu?

BANDA: Kwanza ni mcheshi, ananisikiliza na ananipenda, lakini pia ni mwanamke ambaye amenivumilia kwa nyakati zote, watu wengi hawakijui hicho kitu, ameanza kunivumilia tangu nikiwa ninacheza Simba, kwa hiyo ananijua vizuri.

IJUMAA: Ni kitu gani unakizingatia sana kwenye fasheni?

BANDA: Mara nyingi huwa napenda kuvaa kawaida. Pia ni mtu ambaye ninafuatilia sana mambo ya fasheni, lakini pia hakuna mtu watu ambao wanapenda fasheni kama wachezaji, japokuwa kwa Tanzania sisi tunaona kama ni uongo lakini kwa nchi za wenzetu wachezaji ni watu wa fasheni sana, kwa hiyo binafsi mara nyingi huwa napenda kuangalia watu wa nje jinsi ambavyo wanavaa.

IJUMAA: Ni msanii gani Bongo ambaye mapigo yake yanakuvutia?

Banda: Jux ndiye huwa ananivutia, lakini pia Ali (Kiba) ni msanii ambaye anavaa kawaida, lakini anapendeza.

IJUMAA: Tangu uvae suti kwenye ndoa yako, uliivaa wapi tena na kwa sababu gani?

Banda: Mimi huwa sirudii suti.

IJUMAA: Kwa nini?

BANDA: Basi tu huwa sirudii, nikivaa suti kwenye interview, siwezi kuirudia, kwa hiyo hata nilivyovaa kwenye harusi, siwezi kurudia kuivaa sehemu yoyote.

IJUMAA: Kwa hiyo huwa unazipeleka wapi?

BANDA: Mara nyingi nampa mdogo wangu aliyenifuata kwa sababu naye ana mwili mkubwa. Siyo suti tu, hata vile viatu ambavyo nilivivaa siku ya harusi ambavyo nilinunua kwa Idris Sultan, bado vipo kwa hiyo hata Idris akivihitaji aje achukue, siwezi tena kuvivaa.

IJUMAA: Hiyo hali ya kutorudia nguo ni hata kwa nguo za kawaida au ni suti tu?

BANDA: Yaani nguo ambayo nilishawahi kuvaa kwenye event yoyote huwa sirudii, lakini hizi nguo za kawaida huwa narudia.

IJUMAA: Wewe ni ‘chizi’ wa nini?

BANDA: Mimi ni chizi wa nguo, napenda sana kuvaa, yaani hata kama kitu kiwe wapi, kama nina uwezo wa kukinunua, nanunua. Mfano wakati ninatoka Afrika Kusini kuja Tanzania, kuna kiatu kilitoka, lakini Afrika Kusini kilikuwa hakipo, kwa hiyo nimeagiza Uingereza na nimeambiwa viatu vimeshafika vipo Afrika Kusini, mimi nipo Tanzania, hivyo nitakaporejea Afrika Kusini nitavikuta kwa sababu nimeshavilipia.

IJUMAA: Mbali na mpira unapenda kitu gani kingine?

BANDA: Napenda kusikiliza muziki ila siyo kuimba.

IJUMAA: Haikusumbui kuishi muda mrefu Afrika Kusini na mke wako kuishi Tanzania?

BANDA: Kwanza nilimuoa siku ya Jumamosi, siku ya Jumapili nikasafiri naye kwenda Afrika Kusini ila kwa kuwa yeye alikuwa hana kibali cha kzi, alikuwa anakaa miezi mitatu kisha anarudi Tanzania.

Hivyo kitendo cha yeye kurudi Tanzania kwa mwezi mmoja kilikuwa hakinisumbui, ila kipindi cha Corona nilikaa zaidi ya miezi mitano bila kuonana naye, hiyo ndiyo ilinisumbua sana, lakini mwisho wa siku niliizoea.

IJUMAA: Kuna kipindi maneno yalisambaa mitandaoni kuwa wewe na mkeo mliachana, unaweza kutuambia ilikuwaje?

BANDA: Mimi na mke wangu siyo watu wa mitandao, hata picha ya familia yetu kuikuta mtandaoni ni kwa nadra sana, labda tunaweza tukaposti kwa mwezi mara moja. Kwa hiyo kipindi nikiwa Afrika Kusini kwa sababu ya Corona na mke wangu yupo huku (Tanzania) ndipo kila mtu akawa anaongea lake kuwa tumeachana, ila mwisho wa siku mimi na mke wangu hatujawahi kugombana na wala hatutegemei kuachana.

IJUMAA: Huwa husumbuliwi na na wasichana kwenye Instagram wakikuhitaji kimapenzi?

BANDA: Siwezi kusema kama ni usumbufu, kwa sababu mtu ana uhuru wa kuongea chochote anachojisikia moyoni mwake.

IJUMAA: Kitu gani ambacho huwa kinakukasirisha kwa mwanamke?

BANDA: (anaguna) yaani unaniuliza swali ambalo sina uzoefu nalo, kwa sababu mimi mke wangu hajawahi kunikasirisha.

IJUMAA: Umewahi kupitisha siku nzima bila kuwasiliana na mkeo?

BANDA: Hapana, haijawahi kutokea.

IJUMAA: Asilimia kubwa ya akina mama wanakuwa wasumbufu pindi wanapokuwa wajawazito, vipi mkeo Zabibu hakukusumbua kipindi cha ujauzito?

BANDA: Nashukuru Mungu kipindi akiwa mjamzito nilikuja kumuona wakati mimba yake ina miezi sita mpaka saba hivi, kwa hiyo kuanzia miezi hiyo mpaka anakuja kujifungua mimi nilikuwa Afrika Kusini hivyo usumbufu wake mimi sikuupata.

IJUMAA: Vipi mawasiliano ya simu yalikuwaje?

BANDA: Tulikuwa tunawasiliana, sema kuna muda tu alikuwa ananuna bila sababu, hivyo nilikuwa namuacha kwa sababu najua siyo yeye.

IJUMAA: Ni kitu gani ambacho huwezi kukisahau kwenye soka?

Banda: Unajua katika kitu ambacho sisi wachezaji hatukipendi katika mpira ni kuwa majeruhi, kwa hiyo kipindi nacheza Simba niliwahi kupata majeraha takriban miezi mitano, hicho ndicho kipindi ambacho sitakuja kukisahau kwenye soka langu.

Kingine ambacho sitakuja kukisahau na kimetokea hivi karibuni ni kufiwa na mlezi wangu ambaye alinichukua kutoka chini mpaka kuwa Banda huyu ambaye watu wanamjua, anaitwa Abdobrozmila.

Makala: Memorise Richard, Bongo

Leave A Reply