The House of Favourite Newspapers

FAMILIA ZA WATU 1500 ZALIA: RAIS JPM, LUKUVI TUOKOENI

0
bomoa bomoa bagamoyo
Baadhi ya wananchi ambao nyumba zao zilivamiwa na kuchomwa moto.

Ni balaa kubwa! Wananchi wa kijiji cha Kwakonje, Kata ya Kibindu Wilaya ya Bagamoyo, wapatao 1500 wamemuomba Rais John Pombe Magufuli na Waziri wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wawaokoe, baada ya nyumba zao zaidi ya 160 kuchomwa moto na kubomolewa na watu wasiojulikana, Jumamosi iliyopita.

 

Licha ya kuchomwa kwa nyumba hizo, pia katika uvamizi huo, watu hao walichoma vitu vilivyokuwa ndani pamoja na mabanda ya mifugo hivyo kusababisha wananchi hao kutawanyika msituni na vichakani wasijue sehemu ya kuishi. Risasi Jumamosi ambalo lilifika kijijini hapo, lilishuhudia wakazi hao wakiwa wanyonge, huku vifaa vyao vichache vilivyonusurika, vikiwa vimekusanywa na mifugo ikiwa imesambaa vichakani.

bomoa bomoa bagamoyo

 

Akizungumza na waandishi wetu, mjumbe wa Kaya 300 wa eneo hilo, Wambura Ikwabe alisema yeye na wenzake walihamia eneo hilo zaidi ya miaka 25 iliyopita, wakiwa wameuziwa eneo hilo na uongozi wa kijiji hicho na kupewa nyaraka zinazowatambulisha kama wakazi halali.

 

Wambura alisema akiwa kijijini hapo na wakazi wengine, hivi karibuni walianza kupewa taarifa za kutakiwa kuhama eneo hilo na kuambiwa kuwa hiyo ni Hifadhi ya Uzigua na hakuna mtu anayeruhusiwa kuishi eneo hilo. Mjumbe huyo alisema baada ya kutangaziwa kuhama, ndani ya siku nne walianza kuvamiwa kwenye makazi yao na kubomolewa nyumba zao na kuchomwa moto huku kukiwa na mali za thamani ndani.

 

bomoa bomoa bagamoyo
Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli.

 

Inadaiwa wabomoaji hao waliwafanyia vitendo vya udhalilishaji akina mama na watoto. Katika tukio hilo, nyumba nne za ibada nazo ziliteketezwa huku Mchungaji wa Kanisa la EAGT Kwakonje, Joel Shabani akisema kitendo kilichofanywa hakikuwa cha kiungwana.

 

“Wametubomolea makanisa yetu, waumini wametawanyika hatujui tutawapata wapi ili tukusanyike na kulia kilio chetu, yaani hapa kila mtu amekuwa kama mnyama wa msituni na wengine wana watoto wachanga, tunamuomba Rais Magufuli na Waziri Lukuvi watuokoe katika balaa hili,” alisema. Diwani wa Kata hiyo, Ramadhani Mkufya ambaye alisema anafahamu matatizo yaliyowapata wananchi wake, alikemea unyanyasaji uliofanyika katika bomoabomoa hiyo.

 

“Hizo taarifa ninazo, lakini suala hilo ni la kisheria na wananchi hao walitakiwa kuhama kwenye eneo hilo ambalo ni Hifadhi ya Uzigua tangu mwaka 2015, lakini mimi niliwapigania mpaka wakabaki pale mpaka hivi sasa.

 

“Hivyo hakuna jinsi kinachotakiwa serikali iwafikirie wananchi hao kuendelea kuishi maeneo hayo kwa kuwa ardhi haipanuki lakini binadamu tunaongezeka, ni busara wananchi hao wangeachwa waendelee kukaa eneo hilo,” alisema diwani huyo.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP, Jonathan Shana alikataa kuzungumzia suala hilo, akisema mtu sahihi wa kufanya hivyo ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo. “Hilo sakata naomba umtafute DC wa eneo hilo ndiye alizungumzie, mimi siwezi kutoa ufafanuzi wowote maana yeye ndiye atakayekuwa akilijua vizuri sakata hilo,” alisema Kamanda Shana.

 

Mkuu wa wilaya hiyo, Majid Mwanga hakuweza kupatikana baada ya simu yake kuita bila kupokelewa kwa muda mrefu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi, hakujibu. Gazeti hili linaendelea kufuatilia tatizo hili lililowapata wananchi na kuona jinsi serikali itakavyowaangalia kwa jicho la huruma. Ili kuona laivu jinsi wananchi wa kijiji hicho wanavyosikitisha baada ya makazi yao hayo kuteketezwa, tembelea Global TV Online leo saa kumi jioni.

 

bomoa bomoa bagamoyo
Waziri wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

STORI: RICHARD BUKOS NA ISSA MNALLY| RISASI JUMAMOSI

Leave A Reply