The House of Favourite Newspapers

Fedha za Majini Zilivyoniendesha Puta-07

0

ILIPOISHIA

Walikuwa hawawezi kunywa wenyewe. Walikuwa kama watu waliopooza. Ilibidi niwanyweshe. Uji ulikuwa moto lakini walikunywa hivyo hivyo kwa sababu ya njaa.

SASA ENDELEA

Kila mmoja alikunywa vikombe vinne. Sasa nikahisi kuwa walikuwa wakijsikia vyema. Hata hivyo, hawakuwa watu wa kuzungumza chochote. Walikuwa wameduwaa tu huku wakitoka ute.
Wakati nawatazama, machozi yalianza kunitoka. Nikajiuliza ni kwa nini baba yangu alikuwa katili kiasi kile. Hivi watu wanaodaiwa kumiliki pesa za majini wanakuwa katili kiasi hiki?
Nikaendelea kujiuliza kama kulikuwa na umuhimu wa kuendelea kuzifurahia zile pesa za marehemu baba yangu wakati zimekatisha uhai wa mama yangu na mwanangu wa pekee ambao sasa wamekuwa mazezeta wasiojielewa?
Sasa fikira zangu zikawa katika kuwaokoa viumbe hao waliokuwa katika mateso mazito. Sikuhitaji tena zile pesa ambazo kwa wakati ule niliziona kama sumu iliyokuwa inanyemelea kunimaliza mimi mwenyewe.
Nikawa nafikiria jinsi ya kuwaokoa viumbe hao ili warudi katika uhai wa kawaida na mimi mwenyewe niweze kuyanusuru maisha yangu.

Nikajiuliza nifanye nini wakati yule jini alishaniambia kuwa ni lazima nitii na nifuatishe maagizo yake kwa vile ndiyo makubaliano yake na marehemu baba yangu.
Upande mmoja wa akili yangu uliniambia kuwa hatua yoyote nitakayochukua kwenda kinyume na maagizo niliyopewa, inaweza kuyagharimu maisha yangu.
Nikaondoka katika lile pango nikiwa na chupa yangu niliyokuwa nimeitilia uji. Wakati natoka nilimuona mama yangu na mwanangu wakinitazama. Walikuwa wakinitazama bila kujielewa lakini nilihisi kama vile walikuwa wakiniambia nisiwaache pale lakini hawakuwa na uwezo wa kutamka maneno.

Nikatembea taratibu kurudi nyumbani huku nikiwaza. Picha ya mama yangu na mtoto wangu ilikuwa imekaa katika akili yangu wakati wote. Ilikuwa picha ambayo sikuipenda hata kidogo.
Nilipofika nyumbani niliketi kwenye kigoda huku nikiendelea kuwaza.
Wazo la kutolewa kafara kwa mke wangu nalo likanijia akilini. Nikaona kama sitaharakisha  kuchukua hatua stahiki, nitamkosa mke wangu ingawa sikujua ingekuwa ni lini.
Hapo nikapata wazo jingine la kwenda kwa mganga. Nikajiambia kwenda kwa mganga lilikuwa ndilo suala sahihi kwa matatizo yaliyokuwa yananikabili.

Sasa nikawa nafikiria niende kwa mganga gani. Kulikuwa na waganga kadhaa pale kijijini kwetu. Nikagundua kulikuwa na mganga mmoja aliyekuwa maarufu zaidi aliyekuwa akiishi kijiji cha pili. Nikaamua kwenda kwake nikiamini kwamba angeweza kulipatia ufumbuzi tatizo langu.
Nilipopata wazo hilo sikutaka kukaa tena, nikaondoka kwenye kigoda nikatoka na kufunga mlango. Nilikwenda kwenye kituo cha bodaboda. Nikapakiwa kwenye pikipiki na kuelekea katika hicho kijiji kilichokuwa na huyo mganga.
Kijana wa bodaboda alinishusha mbele ya nyumba ya mganga huyo. Uzuri wa waganga wa vijijini ni kwamba hata kama ni hodari kiasi gani huwezi kukuta msururu mrefu wa watu nyumbani kwake. Muda ule niliofika nilikuta watu watatu tu waliokuwa wakisubiri kuingia kwa mganga huyo.
Niliposhuka kwenye bodaboda nilikwenda barazani mwa nyumba hiyo nikawasalimia watu hao niliowakuta kisha nikakaa kwenye foleni.

Yalipita karibu masaa mawili hadi ilipofika zamu yangu. Niliingia kwenye ukumbi wa mganga huyo uliokuwa umetandikwa jamvi. Mganga mwenyewe alikuwa ameketi karibu na ukuta akiwa amevaa kaniki na shati jeupe.
Kando yake kulikuwa na chetezo kilichokuwa kinafuka moshi uliokuwa unanukia harufi ya udi.
Mbele yake kulikuwa na rundo la vitabu vilivyokuwa vimewekwa chini. Juu ya ukuta aliokuwa ameegemea kulikuwa na tunguri kadhaa zilizokuwa zimepachikwa.
“Karibu, kaa hapo,” mganga aliniambia huku akinionesha mahali pa kukaa. Nikakaa chini mbele yake.
“Naweza kukusaidia,” akaniambia.
“Nina shida. Naomba msaada wako.”
“Shida gani?”
Nikamueleza tatizo lililokuwa limenipeleka pale. Mganga akashtuka aliposikia kuwa ninamiliki sanduku la pesa za majini.

“Pesa za majini zina matatizo,” mganga akaniambia na kuongeza.
“Matatizo yake ni kama hayo. Mimi namfahamu baba yako lakini sikuwa nikijua kama alikuwa akimiliki pesa za majini. Kumbe alimtoa mhanga mke wake na mjukuu wake. Mwenyewe amekufa na siri imefichuka!”
“Sasa naomba msaada wako”
“Ulitaka nikusaidieje?”
“Kwanza uwaokoe mama yangu na mwanangu ambao wanateseka kule mapangoni. Na pili ninataka kuepukana na zile pesa. Mimi sizitaki tena.”
Mganga akacheka.

“Kwa nini huzitaki?”
“Masharti yake ni magumu kwangu. Yule jini aliniambia niende nikamzini makaburini. Sitaweza.”
“Lakini baba yako aliyaweza yote hayo!”
“Kosa alilofanya ni kunifanya mimi kuwa mrithi wake wa pesa zile na kwa hivyo ninatakiwa nimrithi na yule jini wake jambo ambalo sitaliweza. Baya zaidi ni kuwa ninatakiwa nimtoe kafara mke wangu ili mama yangu akifa pawepo na mtu mwingine.”
Itaendelea wiki ijayo
Itaendelea wiki ijayo
Kitabu changu cha “NILIVYOGEUZWA PAKA” sasa kipo mitaani. Kwa mawasiliano ya kukipata piga namba 0712 777737. Wasomaji wa Tanga wapige namba 0655 340572.

Leave A Reply