The House of Favourite Newspapers

Fedha za Majini Zilivyoniendesha Puta-3

0

ILIPOISHIA

Nikamuacha atangulie mbele yangu. Njia tuliyokwenda ilikuwa ikielekea lilikokuwa shamba lake. Nikahisi tulikuwa tunakwenda shambani kwake. Lakini tulipolikaribia shamba hilo tuliliacha shamba upande wa kushoto tukashika njia ya upande wa kulia.

Kimoyomoyo nilikuwa nikijiuliza, baba alikuwa ananipeleka wapi usiku ule. Kwa mbali tulikuwa tukisikia milio ya fisi pamoja na ya wanayama wengine. Kile kitendo ch baba kuwa mbele yangu kilinizuia nisimuulize maswali mengi yaliyokuwa yakipita akilini mwangu.

Baada ya muda kidogo tukawa tumeingia kwenye njia iliyoelekea kwenye pori. Ilikuwa njia nyembamba ya kupita kwa miguu.

Sehemu yenyewe ilikuwa inatisha lakini baba alikuwa akitembea bila kuonesha wasiwasi wa aina yoyote. Mimi niliyekuwa nyuma yake nikiwa nimeshika sime mkononi, ndiye niliyekuwa nikitazama kila upande kwa wasiwasi.

SASA ENDELEA…

Wakati tunazidi kutokomea katika pori hilo, ghafla nilimuona baba akianza kusitasita. Kasi yake ya kutembea ilipungua. Mwisho akawa amesimama akielekeza mkono upande wangu kama aliyekuwa akihitaji msaada.

 Nikaushika mkono wake na kumuuliza.

 “Nini baba?”

 Nikamuona kama aliyekuwa anataka  kuanguka, nikamshika vizuri.

 Niliuona uso wake. Alikuwa kama aliyekuwa akisikia maumivu.

 Hakuweza kusema kitu hadi nilipomlaza chini kichalichali.

 Kwanza alinyoosha kidole chake kuelekea ule upande tuliokuwa tunakwenda.

“Kule mbele kuna mti wa mkuyu. Utakuta katika moja ya matawi yake nimening’iniza kitambaa chekundu na cheusi…utakata kushoto utakuta kichaka kikubwa. Ukiingia ndani ya kichaka hicho utakuta pango…” akaniambia lakini huo ulikuwa ndiyo mwisho wa maelezo yake.

 “Ni pango gani baba?” nikamuuliza haraka.

 “Safari yangu itaishia hapa…wewe nenda tu…” akaniambia.

 “Sijakuelewa baba. Unasema….?”

 Kabla hata sijamaliza kumuuliza nilichotaka kumuuliza alivuta pumzi ndefu kisha akazishusha. Akawa kimya. Hapo hapo nikajua kuwa baba yangu alikuwa ameshakufa.

 Alikuwa ameniacha njia panda. Sikujua baba alikuwa ananipeleka wapi huko alikoniambia kuna pango. Na pia sikujua alikuwa anakwenda kunionesha nini usiku ule.

 Nilichofanya hapo ni kumbeba begani na kurudi naye nyumbani. Kwa vile nilitembea naye mwendo mrefu, hadi tunafika nyumbani nilikuwa nimechoka.

Nilimuingiza chumbani kwake nikamlaza kitandani kisha nikammulika taa kumtazama usoni kwake. Kwa kweli mzee alikuwa ameshakufa!

 Likizo yangu ile ilikuwa ya balaa. Nilipofika tu hapo Manundu, Korogwe alikufa mwanangu, siku ile tena mzee wangu naye ananiaga katika mazingira ya kutatanisha.

 Baada ya kukaa na kuwaza nikiwa pembeni mwa kitanda nilichoulaza mwili wa baba, nikayakumbuka yale maneno ya baba aliyoniambia.

 “Cha kwanza ninachotaka kukwambia ni kuwa endapo nitafumba macho siku yoyote, urithi wako uko chini ya mvungu wa kitanda nilicholala.”

 Nikajiambia baba yangu alishajua kuwa atakufa leo ndiyo maana aliniita na kunieleza maneno hayo.

 Lakini shauku ya kutaka kujua kile alichoniambia ni urithi wangu kilichoko chini ya mvungu ikanipata. Nikachutama na kumulika taa chini ya mvungu wa kitanda chake.

 Nikaona mfuko wa ngozi kisha nikaona sanduku la chuma. Shauku yangu ikawa kwenye lile sanduku la chuma.

 Nikatia mkono mvunguni na kulivuta. Lilikuwa zito. Ikabidi nitumie mikono miwili, nikalitoa kwenye mvungu.

 Lilikuwa limefungwa kwa kufuli kubwa ya shaba. Nikafikiria niivunje ile kufuli ili nitazame kilichomo ndani lakini nikakumbuka baba yangu alikuwa na tabia ya kutembea na funguo nyingi anazozifunga kiunoni.

 Nikajua lazima kutakuwa na funguo ya kufuli ile.

 Nikainuka na kumtazama kiunoni. Nikaziona zile funguo alizozifunga kwenye mkanda wake. Nikazitoa.

 Zilikuwa karibu funguo tano. Nikawa natafuta ufunguo unaokubaliana na ile kufuli. Nikagundua funguo mbili. Kwa vile sikujua ni funguo ipi itakayofungua ile kufuli, nilizijaribu zote. Moja ilikataa hata kuingia kwenye tundu ya kufuli. Nyingine ikakubali na ndiyo iliyofungua kufuli hiyo.

 Kufuli ilipofunguka niliichomoa nikaufungua mlango wa sanduku hilo. Nilipotupa macho ndani nilishituka nikajiuliza kama kweli baba yangu alikuwa na utajiri wa kiasi kile!

 Noti nyekundu za elfu kumi kumi zilikuwa zimejaa ndani sanduku hilo hadi juu! Wakati ninazitazama niliona kama ninachanganyikiwa kwa sababu sikuwahi kuona fedha nyingi kiasi hicho.

 “Baba yangu alizipata wapi pesa hizi?” nikajiuliza kwa mshangao lakini sikupata jibu akilini mwangu.

 Nikaona nizitoe zile pesa na kuzihesabu. Nilifanya ile kazi usiku kucha! Mpaka kunaanza kupambazuka sikuwa nimemaliza kuzihesabu noti zote.

 Nikaona nizirudishe kwenye lile sanduku. Nikalifunga na kutia ile kufuli kisha nikalibeba na kwenda nalo katika chumba nilichokuwa ninalala. Nikalitia mvunguni.

 Nikarudi tena katika chumba cha baba. Nikaufunika mwili wake kwa shuka yake aliyokuwa akijifunika. Nikaamua nikae kwenye kiti nisubiri kuche ili nitoe taarifa kwa majirani kuwa mzazi wangu amefariki dunia usiku.

 Ilipofika saa kumi na mbili asubuhi nikampigia simu mke wangu na kumjulisha kuwa baba mkwe wake amefariki dunia usiku.

 Mke wangu alishituka sana akaniambia angefanyaje wakati baba yake naye alikuwa katika hali mbaya.

 “Wewe mshughulikie mzazi wako kwanza, huku tutazika tu,” nikamwambia.

 Akanipa pole nyingi na kuniambia kuwa alikuwa ananisikitikia hasa vile ambavyo nilikuwa peke yangu. Baada ya mazungumzo yetu nikakata simu na kuwapigia ndugu na jamaa waliokuwa pale Korogwe.

 Baada ya hapo nikatoka nje. Muda huo baadhi ya watu walikuwa wanakwenda mashambani na wanawake walikuwa wakifanya usafi nje ya nyumba zao.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia hapahapa Jumanne ijayo.

 

Kitabu changu cha “NILIVYOGEUZWA PAKA” sasa kipo mitaani. Kwa mawasiliano ya kukipata piga namba 0712 777737. Wasomaji wa Tanga wapige namba 0655 340572.

Leave A Reply