The House of Favourite Newspapers

Fei Toto Kufungiwa na TFF Ikibainika Azam FC Wamemshawishi Kuvunja Mkataba

0
Feisal Salum ‘Fei Toto’

MWENYEKITI wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Said Sudi amesema ikibainika Azam FC wamemshawishi kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuvunja mkataba Yanga bila kufuata utaratibu wataifungia timu kusajili na mchezaji mwenyewe.

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu kamati hiyo ifanye kikao cha pamoja na pande mbili zikihusisha wamiliki wa mchezaji huyo na kiungo huyo ambaye aliandika barua ya kusitisha mkataba wake.

Katika kikao hicho, kamati hiyo ilijiridhisha kuwa kiungo huyo ni mali ya Yanga kutokana na kuwa na mkataba hadi mwaka 2024.

Akizungumza na moja ya kituo kikubwa cha radio nchini, Sudi alisema kuwa Azam ni kati ya klabu zilizokuza soka hapa nchini hivyo itakuwa inajishushia heshima kama itakuwa imehusika kwenye suala hilo.

 

Sudi alisema kuwa, hawana uhakika juu ya hilo, lakini wanaendelea na uchunguzi na kama ukikamilika na kujiridhisha katika hilo basi wataifungia Azam kusajili pamoja na kiungo huyo kumfungia kucheza soka.

“Sisi tunasikia kama wanavyosikia wengine kuwa Azam inahusika katika kumshawishi Fei Toto ambapo kimsingi ni kosa. Ikibainika Azam wamemshawishi kuvunja mkataba na Yanga bila kufuata utaratibu, basi tutaifungia timu hiyo kusajili na Fei Toto tutamfungia tukipata ushahidi wa kutosha hatutasita kufanya hivyo.

“Tulizifungia klabu mbili za Prisons na Singida Big Stars kwa makosa ya kuwashawishi wachezaji wa timu nyingine wakati wakiwa na mikataba wakaomba review, licha ya hivyo tukawakuta na hatia na tukawafungia.

“Shida ya wachezaji wengi huwa wanasaini mikataba baada ya kusoma ukurasa unaoonyesha mshahara watakaolipwa lakini hawapitii karatasi zenye vifungu vyenye masharti ya utekelezaji wa mkataba husika.

“Fei Toto alisimamia kifungu kimoja wakati mkataba huundwa kwa vipengele vingi, unapaswa uvisome vyote kwa pamoja.

“Mwanasheria wa Fei Toto aliomba mteja wake asihojiwe kwenye kamati, hatukumuhoji baadaye tulimuhoji ‘Off Record’ tukabaini kuwa Fei Toto na mwanasheria wake wanakinzana, mwanasheria aliiomba kamati imuachie Fei Toto aende timu nyingine, tulipomuhoji yeye akasema hataki kucheza mpira anataka kupumzika.

“Kwa hiyo uamuzi wa kamati ni kuwa Fei Toto ni mchezaji wa Yanga, na hakuna mkataba uliovunjika,” alisema Sudi.

STORI NA WILBERT MOLANDI, CHAMPIONI JUMATANO

EXCLUSIVE: ALI KAMWE AFUNGUKA USAJILI STRAIKA na BEKI wa KATI, SAKATA LA FEI TOTO UKWELI HUU HAPA

Leave A Reply