The House of Favourite Newspapers

Fisi Wakithiri Shinyanga, Serikali Kuwashughulikia

0

KUTOKANA na kukithiri kwa matukio ya fisi kushambulia wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga hususan watoto wadogo, serikali imeunda kikosi maalumu  kuwasaka.

 

Kwa takribani miezi sita sasa, kumekuwepo na matukio ya fisi kuonekana katika maeneo mbalimbali ya mji wa Shinyanga ambapo huwashambulia watu na kuwasababishia majeraha huku ikiripotiwa watoto wasiopungua wanne kufariki baada ya kushambuliwa na fisi hao.

 

Tukio la hivi karibuni lilitokea katika kitongoji cha Relini mtaa wa Nhelegani Manispaa ya Shinyanga, ambako mtoto aliyetambulika kwa jina la Kulwa Machiya (6) alikufa baada ya kujeruhiwa vibaya na Ffsi aliyewavamia na kumshambulia wakati wakitokea machungani pamoja na watoto wenzake.

 

Kutokana na hali hiyo, halmashauri hiyo  imelazimika kuunda kikosi maalumu ambacho kitaendesha operesheni ya kuwasaka fisi hao ili kuwaua na kuepusha wananchi kuendelea kuishi wa wasiwasi wa kushambuliwa.

 

Kiongozi wa kikosi hicho, Ezra Manjerenga,  amesema, operesheni hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya wataalamu wa Maliasili Kitengo cha Wanyamapori, Jeshi la Polisi, viongozi wa vijiji husika wakiwemo walinzi wa Jadi (Sungusungu).

 

Kwa mujibu wa maelezo ya kiongozi huyo, tayari operesheni hiyo imeanza leo saa 12 alfajiri kwa kufanya msako katika vichaka na mapori yote yaliyopo katika kijiji cha Nhelegani kwenye vitongoji vya Itogwanh’olo na Ibanza.

 

Hata hivyo kiongozi huyo ametoa wito kwa wakazi wote wa maeneo ambako oparesheni inafanyika, kutoa ushirikiano wao kwa kuelekeza maeneo ambayo fisi hao wamekuwa wakionekana mara kwa mara ili  kukabiliana nao.

 

Leave A Reply