The House of Favourite Newspapers

Funga Mwaka 2021… Jini Mkata Kamba

0



BILA kupepesa kuna watu wengi hususan wale ambao ni mashabiki kindakindaki wa mastaa Bongo ambao mara nyingi wamekuwa wakiumizwa na kuachana kwa baadhi ya mastaa wao wanaowapenda na kuwasapoti kwenye kazi zao.

Hii itakuwa siyo mara ya kwanza kwa mastaa wakubwa Bongo kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi kisha baada ya muda mahaba yote yanaisha; wenyewe wanasema walipitiwa na jinni mkata kamba ambaye kazi yake huwa ni kutenhanisha wapendanao.

Uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA unakuletea ripoti ya mapenzi ya mastaa yaliyovunjika mwaka 2021 na sababu zilizofanya waachane;

 

HARMONIZE NA KAJALA

Miongoni mwa penzi ambalo lilitikisa vilivyo katika mitandao ya kijamii na kitaani ni pamoja na penzi la staa wa muziki wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ na mwanamama kiwango kutoka tasnia ya Bongo Movies, Frida Masanja ‘Kajala’.

Iliwachukua miezi kadhaa tu kabla ya jini mkata kamba kulipitia penzi hilo ambapo sababu kubwa inayotajwa ni kitendo cha Harmonize kutaka kula kuku na mayai yake (mama na mtoto) baada ya kudaiwa kumtaka kimapenzi Paula Kajala.

Bado jambo hilo limemfanya Kajala kutumbukia nyongo na kushindwa kabisa kumsamehe Konde Boy Mjeshi.

 

RAYVANNY NA FAHYMA

Penzi la Rayvanny na Fahyma ni moja ya mahusiano yaliyodumu kwa miaka kadhaa hadi wakafikia hatua ya kuzaa mtoto; kapo ambayo ilipendwa na watu wengi, lakini mwishowe jini mkata kamba naye alilipitia tena bila huruma, wawili hao wakaachana.

Pamoja na Rayvanny kuendelea na maisha na kutuliza mtima wake wa mrembo Paula Kajala, lakini habari za ndani zinaeleza kwamba, sababu kuu iliyowafanya wawili hao wakabwagana ni usaliti ambapo inadaiwa kuwa Fahyma ndiye aliyeanza kumsaliti Rayvany kwa kuchepuka na mwanaume mwingine.

 

HAMISA NA VUNJABEI

Baada ya kuachana na mzazi mwenzake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, mwanamitindo Hamisa Mobeto alijiingiza kwenye uhusiano wa kimapenzi na mfanyabiashara Fredi Vunjabei ambapo penzi lao lilidumu kwa siri ndani ya miezi kadhaa kisha na wao wakaachana.

Kwa sasa Hamisa anadaiwa kubanjuka na staa mkubwa wa muziki duniani, William Leonard Roberts ‘Rick Ross’.

Sababu ya kuachana na Hamisa na Vunjabei ni baada ya kubainika kwamba, jamaa huyo ana mkewe hivyo Hamisa akionekana mchepuko, jambo ambalo halikuwa jema.

 

RUBY NA KUSAH

Bila ubishi mwanamama Hellen George au Ruby ndiye staa wa kike mwenye sauti tamu ya kumtoa nyoka pangoni ukiachana na Zuchu, Nandy, Vanessa, Maua Sama na wengine.

Naye jini mkata kamba aliingilia penzi lake na msanii mwenzake, Kusah ambaye walikuwa wamejaaliwa mtoto mmoja aitwaye Aaliya.

Sababu ya kuvunjika kwa penzi hilo ni baada ya Kusah kubainika yupo kwenye mahaba mazito na mwanamama wa Bongo Movies, Aunt Ezekiel.

 

AUNT NA IYOBO

Aunt Ezekiel ni kati ya mastaa wa kike waliojizolea umaarufu mkubwa kutokana na kazi yake ya sanaa ambaye miaka kadhaa nyuma aliingia kwenye penzi zito na Dansa wa Diamond, Moses Iyobo ambaye walijaaliwa pamoja mtoto wa kike aitwaye Cookie.

Sababu kuu ya kuachana kwao ni usaliti ambapo hivi karibu Aunt alikiri kuanza uhusiano wa kimapenzi na Kusah ilihali analala kitanda kimoja na Iyobo; “Nilianza uhusiano mpya na Kusah wakati nipo na baba Cookie…”

 

ESMA NA MSIZWA

Achana na ile ndoa ya Aristote iliyotengeneza vichwa vingi vya habari mitandaoni; kuna ile ya dada wa msanii mkubwa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, Esma Khan na mfanyabiashara Msizwa ambayo ilifungwa miezi kadhaa iliyopita ikigharimu zaidi ya shilingi milioni 300 na kuacha mshangao mkubwa.

Hata hivyo, cha kushangaza ndoa hiyo haikudumu zaidi ya miezi mitatu baada ya kupitiwa na jini mkata kamba na sasa kila mtu anaendelea na maisha yake.

Sababu ya kuvunjika kwa ndoa ya Esma na Msizwa ni madai kwamba, mwanaume huyo alifuata umaarufu kwa mwanamama huyo na si kweli kwamba alikuwa na mapenzi ya dhati.

 

DARLEEN NA ISIHAKA

Miongoni mwa wapenzi waliotikisa Bongo ni pamoja na lile la dada wa Diamond, Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’ na Isihaka Mtoro ambao walidumu kwa kipindi cha miaka kadhaa kisha nao jini mkata kamba akaingilia kati ndoa yao na sasa hawapo pamoja.

Sababu inayotajwa iliyosababisha wawili hao kumwagana ni kutokana na chokochoko za Darleen na mke mkubwa wa Isihaka aitwaye Sabra.

 

HARMONIZE NA SARAH

Baada ya kuachana na mwigizaji Jacqueline Wolper, Harmonize Mjeshi aliamua kuanzisha mahaba mapya na mtoto wa Kiitaliano, Sarah Michelotti ambapo hata hivyo, ndoa yao haikudumu na hivi sasa staa huyo anatoka na mrembo mwingine aitwaye Briana; raia wa Australia.

Sababu ya Harmonize na Sarah kumwagana ni kutokana na usaliti ambapo mwanamama huyo alimtuhumu jamaa huyo kusaliti penzi lao na video vixen Nicole na Kajala.

 

NAI NA MONI

Video Vixen maarufu Bongo, Nairath Ramadhani ‘Nai’, mwaka huu haukuwa mzuri kwake baada ya kutengana na aliyekuwa mpenzi wake wa miaka mingi ambaye ni rapa Moni Centrozone.

Sababu ya Nai na Moni kuachana ni baada ya mrembo huyo kutuhumiwa kuchepuka na mfanyabiashara maarufu Bongo.

 

TUNDA NA WHOZU

Baada ya kusemwa kwa muda mrefu kuwa anapenda maisha ya bei ghali na siyo ‘wife material’ kwa sababu muda mwingi anajiachia na wanaume tofautitofauti mahotelini, hatimaye miaka kadhaa nyuma video vixen Annastazia Kimaro ‘Tunda’ aliingia kwenye mahaba mazito na msanii wa Bongo Fleva, Whozu.

Mtoto wa kike akatulia, mwishowe akabeba mimba na kufanikiwa kujifungua salama binti mrembo aitwaye Lola, lakini kama ilivyo kawaida, jini mkata kamba amewapitia na sasa inasemekana kuwa hawapo pamoja wamebaki kulea tu mtoto wao.

Sababu ya kuachana kwao ni kutokana na Tunda kupenda maisha ya mjini nab ado hayupo tayari kuwa mama bora wa familia.

 

S2KIZZY NA TUERN

Wakati mwaka 2021 unaingia, miongoni mwa kapo zilizozungumzwa ni pamoja na ile ya mtayarishaji wa muziki Bongo, S2Kizzy na mrembo Tuern; yule anayebana sauti kama mwigizaji Wema Sepetu.

Baadaye zilianza kuvuma stori kwamba, Tuern amemwagana na S2Kizzy na kutua kwa msanii Baddest.

Sababu ya kumwagana kwa wawili hao ilidaiwa ni kitendo cha Tuern kuwachanganya huku akidaiwa kuwa ni bendera fuata upepo kwa mastaa Bongo.

 

AMBER LULU NA BOTION

Awali zilikuwa ni stori tu kwamba, kuna jamaa aitwaye Emba Botion ambaye anatoka na msanii Amber Lulu.

Baadaye ilibainika kwamba, jamaa huyo naye ni msanii wa Bongo Fleva ambao katika uhusiano wao huo walijaaliwa mtoto mmoja wa kike aitwaye Ariana kabla ya kumwagana hivi karibuni na mwanamama huyo akaachia Wimbo wa Nimeachika.

Sababu ya kuachana kwao inatajwa ni kutokana na vipigo alivyokuwa akipokea Amber Lulu kutoka kwa jamaa huyo.

STORI: MEMORISE RICHARD, DAR

Leave A Reply