The House of Favourite Newspapers

Gamondi: Tutawapiga Al Ahly huko huko kwao

0

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema nyota wake wakiongeza umakini eneo la ushambuliaji na kuondoa makosa madogomadogo katika eneo la ulinzi itakuwa timu bora na tishio Afrika na ameitaka timu yake kwenda kuishangaza Al Ahly katika mechi yao ya mwisho ya Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika Machi 2.

Gamondi alisema hayo akiwa na furaha baada ya kuandika rekodi nyingine akiiongoza timu yake kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga CR Belouizdad mabao 4-0.

“Hongera Wananchi tumeandika historia nyingine licha ya wengine kukosa imani na sisi kutokana na namna tulivyoanza vibaya mchezo wetu wa kwanza wa hatua ya makundi, wachezaji wangu na benchi letu la ufundi tumefanya yaliyo bora;

“Wachezaji wangu wamefanya kazi nzuri na kubwa wameingia kwenye kitabu cha historia, licha ya ushindi huo na ubora waliouonyesha natamani kuona inabadilika maeneo mawili kwa kuwa imara zaidi ili iweze kuwa bora Afrika;

“Safu ya ushambuliaji ina upungufu, wanatengeneza nafasi nyingi wanatumia chache, pia eneo la ulinzi kuna makosa madogo madogo nikifanikiwa kurekebisha na wachezaji wakanielewa Yanga itakuwa timu bora Afrika kwa ushindani,” alisema.

Akizungumzia kutinga hatua ya robo fainali alisema anafuraha sana kufuzu hatua hiyo bila kujali nafasi aliyopo huku akikiri kuwa kuipeleka timu hiyo hatua ya makundi baada ya kuikosa kwa miaka 25, sasa amefika robo fainali na hiyo ni rekodi nzuri kwake.

“Nina furaha sana kuwa nafasi ya pili huku nikiwa nimeshafuzu hatua ya robo fainali bila kujali naenda kumaliza na timu gani lakini nina furaha sana na nitakwenda kucheza na mpinzani wangu kusaka pointi nyingine tatu ili nimalize nafasi ya kwanza;

“Nawafahamu Al Ahly vizuri kwasababu nimefundisha soka la Afrika kwa muda mrefu hivyo nafahamu aina ya uchezaji wao naandaa timu kwenda kucheza kwa ku-relax bila presha ili kuweza kupata matokeo pia kwenye mchezo huo na kuweza kuongoza kundi;

“Timu za Afrika miaka ya hivi karibuni zimekuwa bora na kuacha kuogopa Waarabu kama ilivyokuwa zamani ambapo hata wao walikuwa wanaamini Afrika ni sehemu ya wao kuchukua pointi sasa ni tofauti wanacheza soka la ushindani,” alisema.

Leave A Reply