The House of Favourite Newspapers

Gonjwa Hili Ndilo Tishio Nchini

0

HOMA ya mapafu, usiichukulie poa! Ugonjwa huo ambao pia hujulikana kama nimonia au Pneumonia umeleta mtikisiko wa aina yake mwaka huu kwa kusababisha vifo vya watu maarufu na wasio maarufu ilhali jamii kubwa ya Watanzania ikiendelea kupigwa butwaa kuhusu athari zake.

 

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani zilizotolewa mwaka 2017, Nimonia ndio ugonjwa unaoongoza kwa kusababisha vifo 39,020 nchini.

 

Licha ya kwamba asilimia kubwa ya wananchi walidhani magonjwa kama vile kifua kikuu (TB), na VVU/Ukimwi ambayo ndio yanayoongoza kwa kushambulia Watanzania na kufuatiwa na nimonia, lakini cha ajabu ni kwamba nimonia ndio ya kwanza kwa kusababisha vifo nchini kwa asilimia 10.46 ya vifo vyote.

 

Nimonia ilizoeleka kuwaathiri watoto zaidi ambapo kati yao 2,500 wanafariki kila siku kutokana na maradhi hayo duniani, lakini sasa hali ni tofauti kwakuwa umelitikisa Taifa baada ya kuelezwa kwamba ndio uliosababisha kifo cha nguli wa biashara nchini Ali Mufuruki.

Mufuruki alifariki mapema, mwezi huu huko Afrika Kusini baada ya kuugua kwa muda mfupi hapa nchini.

 

Taarifa za kitengo cha serikali ya Marekani kinachoshughulika na magonjwa ya mapafu, inasema kuna visababishi zaidi ya 30 vya maradhi.

Ili kupata ufafanuzi wa kina kuhusu ugonjwa huo, UWAZI lilizungumza na Dk. Godfrey Chale kutoka hospitali ya Manispaa ya Temeke ambaye aliuelezea ugonjwa huo kama ifuatavyo.

 

“Homa ya mapafu au Pneumonia ni maambukizi katika viriba ya hewa katika pafu moja au mapafu yote. Viriba hivi vya hewa huweza kujaa maji au usaha na kusababisha mgonjwa kukohoa, homa kali na kupumua kwa shida. Pneumonia hubebwa na bakteria, virusi au fangasi.

 

“Pneumonia inaweza kuwa ya kawaida na ikapona lakini wakati mwingine huwa ni tishio kwa uhai na huweza kuleta kifo. Ugonjwa huu mara nyingi huwapata watoto wadogo au watu wenye umri zaidi ya miaka 65 lakini pia huweza kuwapata watu ambao mfumo wao wa kinga mwilini umeshambuliwa na magonjwa nyemelezi,” alisema.

 

Akieleza dalili za ugonjwa huo alisema ziko mbalimbali na hutofautiana toka dalili za awali hadi zile ambazo ni kubwa zaidi. Tofauti ya dalili wakati mwingine haisababishwi na muda tu ambao mgonjwa ameugua, bali pia nini kimesababisha, umri wa mgonjwa na kinga yake ya mwili kwa ujumla. Dalili za kati kawaida huwa kama za mafua au kikohozi lakini hudumu kwa muda mrefu.

 

“Dalili huweza kuwa maumivu ya kifua unapokohoa au kuhema, kuchanganyikiwa mambo (mental Confusion). Hii mara nyingi hutokea kwa watu ambao wana umri zaidi ya miaka 65, dalili nyingine ni kikohozi kizito, uchovu usioisha, homa, kutoka jasho na kutetemeka mwili, kichefuchefu, kutapika na kuharisha, pia kuishiwa pumzi.

 

Alisema watoto wachanga wanaweza wasionyeshe dalili zozote za maambukizi au wanaweza kutapika na kuwa na homa na kukohoa, kuishiwa nguvu na kushindwa kupumua au kula.

Alishauri kumuona daktari mara moja unapoona una shida ya kupumua, maumivu ya kifua na homa isiyoisha ya nyuzi joto za mwili 39 za Celcius au zaidi) au kukohoa kusikokoma.

 

Alisema ni vyema zaidi pia kwa watu wenye matatizo mengine ya afya na mfumo wa kinga ambao ni dhaifu na watu ambao wana saratani na wanapokea matibabu ya mionzi au dawa nyingine ambazo huweza kuleta tatizo kwa mfumo wa kinga mwilini.

 

Alisema sababu kubwa ya mtu kuugua ugonjwa huu ni bakteria ambao wako katika hewa tunayovuta kwani kila siku unavuta bakteria hawa lakini mwili unajilinda ili wasilete tatizo katika mapafu yako lakini wakati mwingine vimelea hivi huizidi nguvu kinga yako ya mwili hata kama afya yako ni nzuri.

 

Ili kujilinda daktari huyo alisema; pata chanjo, epuka sigara na uvutaji tumbaku, tunza mfumo wako wa kinga kwa kuzingatia kanuni za afya na watoto wapate chanjo.

 

HABARI; Gabriel Mushi

 

 

Leave A Reply