The House of Favourite Newspapers

Gonjwa Tishio la Wanawake Latajwa

0
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Crispin Kahesa.

 

WAKATI Serikali ikiendelea kuwapatia chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi (HPV) mabinti wenye miaka tisa hadi 14; imebainika kuwa saratani hiyo ndio tishio zaidi kwa kusababisha vifo vya wanawake tisa kati ya 10 duniani.

 

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa Feruari mwaka huu ilieleza kuwa vifo hivyo hutokea zaidi kwa nchi zenye kipato cha chini na kipato cha kati ngazi ya chini ambako ndiko penye huduma duni za afya.

 

Ripoti hiyo imebainisha kuwa kati ya wagonjwa 570,000 wa saratani ya shingo ya kizazi, wagonjwa 311,000 hufariki dunia kila mwaka hali inayodhihirisha namna ugonjwa huo ulivyo hatari duniani.

 

Aidha, akifafanua kuhusu hali ya ugonjwa huo kwa upande wa Tanzania, Mkurugenzi wa Idara ya Kinga na Uchunguzi kutoka Taasisi ya magonjwa ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk. Crispin Kahesa alisema saratani ya shingo ya kizazi ndio saratani inayoongoza kwa kusababisha vifo nchini.

Alisema saratani hiyo ambayo inawaathiri zaidi akina mama, imechukua asilimia 36 ya saratani zote.

“Ni kubwa kwa sababu kati ya watu 100,000, watu 26,000 wameathirika licha ya kwamba saratani hii inaweza kuzuilika kabisa isitokee,” alisema.

Aidha, alisema idadi ya wagonjwa wa saratani imeongezeka kutoka 250 na 300 kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita hadi kufikia wagonjwa 900.

 

INAVYOZUILIKA KIRAHISI

Dk. Kahesa alisema saratani ya shingo ya kizazi ambayo ikigundulika mapema inatibika, husababishwa na kirusi cha ‘Human Pappiloma Virus’ na huambukizwa kwa njia ya kujamiiana.

Alisema ili kuzuia saratani hiyo ni muhimu watu kuelimishwa kuhusu saratani hiyo, pili ni kuhakikisha watoto wa kike wenye umri kuanzia miaka tisa hadi 14 wanapatiwa chanjo ya saratani hiyo inayoendelea kutolewa nchi nzima tangu mwaka jana.

 

“Lakini pia ni muhimu kwa wanawake kufanyiwa uchunguzi wa awali mara kwa mara kwa wale wenye umri kuanzia miaka 25 kwa sababu hii ni saratani ambayo ina matokeo mazuri sana kwenye tiba kama ukiiwahi.

“Tunawapatia chanjo watoto wa umri huo wa miaka 9-14 kwa sababu hawajaanza kukutana na visababishi. Saratani inasababishwa na kirusi ambacho kinapatikana kwa njia ya kujamiiana, kwa hiyo kwa mwanamke yeyote akishakutana nacho hakuna haja tena ya chanjo zaidi ya matibabu,” alisema.

 

WANAUME NAO HATARINI

Aidha, alisema saratani hiyo ya shingo ya kizazi licha ya kuwa tishio kwa wanawake zaidi, pia wanaume wachache wanaojihusisha na matendo ya kujamiiana kwa njia ya haja kubwa nao hupatwa na saratani hiyo.

“Wanaojamiiana kwa njia ya haja kubwa wanaweza kupata saratani kwenye huo mlango wa haja kubwa,” alisema.

 

TIBA MBIONI KUPATIKANA

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, taasisi mbalimbali zilizozungumza na UWAZI zimeeleza hatua mbalimbali za kutibu saratani hiyo.

Kwa upande wake Dk. Kahesa, alisema mbali na vyakula kumjengea kinga ya kawaida mtu, lakini haviwezi kuzuia maambukizi tiba ya saratani hiyo.

 

“Tiba ya saratani hutegemea makundi na aina ya saratani yenyewe. Ipo tiba ya kuchoma (cauterization) ambayo hutolewa kwa wagonjwa wenye matatizo ya shingo ya kizazi kabla hayajakuwa saratani ambapo hutumika joto kali, umeme na kemikali kuchoma sehemu iliyoathirika.

 

“Tiba ya dawa (Chemotherapy); hii hutumia dawa za saratani ambazo huua chembechembe au seli za saratani ya shingo ya kizazi. Dawa hizi hutolewa kwa mgonjwa ambae saratani imeshasambaa mwilini na inahusisha dawa moja pekee au mchanganyiko wa dawa zaidi ya moja ambazo mgonjwa hupewa kwa njia ya dripu au kumeza,” alisema.

 

Aidha, Mkurugenzi wa Tiba Asili katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dk. Joseph Otieno alisema tayari kuna dawa ambayo imefanyiwa utafiti na wanatarajia kuipeleka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ili kufanyiwa uhakiki zaidi.

 

“Tumeshatengeneza vidonge, tunatarajia kupeleka NIMR kwa ajili ya Clinical evaluation. Bado ipo katika hatua za mwanzo ambazo ni kupima hali ya sumu ambayo tutafanyia kwa wanyama.

“Kwa hiyo hali ya sumu ikishahakikiwa na kupita hatua hii (pre clinical evaluation) ndio utaratibu utafuata kufanyiwa majaribio kwa binadamu ambayo inaitwa -clinical evaluation,” alisema.

Alisema dawa hiyo imetokana na mimea ya asili ambayo ina uwezo wa kutibu saratani hiyo.

 

MSTAFELI WATAJWA KUWA KIBOKO YA SARATANI

Wakati hali ikiwa hivyo, Mtaalamu na Mtabibu Abdallah Mandai kutoka katika kituo cha Tiba cha Mandai Products alisema kuwa utafiti uliofanywa miaka ya hivi karibu katika Chuo Kikuu cha Purdue, Marekani, ulibaini uwezo mkubwa wa mstafeli katika kukabiliana na maradhi ya saratani.

 

Alisema chuo hicho kinachojihusisha na masuala ya dawa, kilibaini kuwa licha ya mizizi, majani na tunda kuwa ni msaada kwa wanaokabiliwa na saratani pia stafeli linasaidia wale wanaokabiliwa na tatizo la msongo wa mawazo na mfadhaiko.

“Tunda hili lenye rangi ya kijani hata likiwiva, lina virutubisho vingi ikiwamo asidi ya amino, vitamini C, madini ya chuma, phosphorus, calcium, carbohydrate na nyuzinyuzi zinazohitajika wakati wa tendo la mmeng’enyo wa chakula tumboni.

 

“Licha ya kuwa suala la stafeli kutibu saratani linaweza kuzua mjadala, lakini hakuna shaka kwa kuwa lina virutubisho vingi yenye uwezo wa kupambana na makali ya maradhi hayo,” alisema Mandai na kuongeza:

“Habari njema ni kwamba mmea huu ambao naweza kuuita ni wa ajabu kutokana na nguvu yake katika tiba, unapatikana nchi nzima kwa maana ya mijini na vijijini,” alisema.

 

Alisema zaidi ya majaribio 20 ya kimaabara yaliyofanywa katika Chuo Kikuu cha Purdue, Marekani kuhusu uwezo wa stafeli yamebaini kuwa huua chembechembe za aina 12 za saratani ikiwamo ya titi, mapafu, kongosho, kibofu na tumbo.

Alisema tafiti hizo zimefafanua kuwa stafeli lina uwezo wa kutibu saratani na magonjwa mengine kwa ubora wa karibu mara 10,000 ya matibabu ya kawaida.

 

“Mchanganyiko wa virutubisho vya annonaceous na acetonins vilivyomo kwenye stafeli vinaua seli zilizo athirika na saratani tu tofauti na dawa za kisasa ambazo zinaua zilizoathirika na nzima.

“Stafeli linadhibiti ukuaji wa seli za saratani bila kusababisha madhara mengine kama ilivyo kwa dawa za kisasa zina athari mbaya kwa mtumiaji na wakati mwingine zinaweza kumsababishia mtumiaji matatizo mengine ya kiafya,” alisema.

STORI: GABRIEL MUSHI

Leave A Reply