The House of Favourite Newspapers

Haa! Dimpoz Unaanzaje Kutembea na Mama?

0
Ommy Dimpoz.

MUZIKI wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva hivi sasa ni kitu kikubwa barani Afrika. Ile shida ya waasisi wake na watu wengine wa burudani, kuona siku moja Tanzania inatajwa kwa sababu ya aina hii ya muziki imetimia.

Ni jambo la kufurahisha kwamba hivi sasa inakula sahani moja na Nigeria, Afrika Kusini, DRC Kongo na nchi nyingine barani Afrika ambazo zinafanya vizuri katika muziki, kitu ambacho awali kilisikika zaidi kwa vijana wa Ulaya na Marekani.

Hii haikuja kwa bahati mbaya, ilianza na kusukumwa na watu, kila mmoja kwa wakati wake, tokea enzi zile wakiimba nyimbo za majuu kwa kuzitafsiri kwa lugha yetu hadi pale baadhi yao walipoanza kuandika mashairi yao kwa Kiswahili na hatimaye kuanza kuelezea matatizo, raha au maono yao kwa ajili ya jamii yao.

Katika safari hii iliyochukua zaidi ya miaka 20, wasanii wamekuwa na uhusiano wa namna tofauti, baadhi wakisigana na kukwazana. Lakini si wao tu, bali wakati mwingine waliingia hadi wadau muhimu wakajenga uadui wa kimaslahi na wasanii na kuleta sintofahamu.

Ukiondoa lile tukio la aibu lililotokea miaka mingi iliyopita, wakati Godfrey Tumaini ‘Dudubaya’ alipompiga jukwaani Lucas Mkenda ‘Mr Nice’, Bongo Fleva haijawahi kushuhudia uhasama mkubwa na wa kijinga zaidi ya bifu za hapa na pale ambazo ni kawaida tu, kama ilivyo huko Ulaya na Marekani.

Wiki iliyopita umetokea ‘ujinga’ wa wasanii vijana wanaosumbua kwa sasa, kukoleza moto wa kile kinachotajwa kuwa ni uadui wao wa kugombea hatamu za muziki huo. Hata wanachopigania sijui ni kitu gani, maana kama ni ufalme wa enzi, mashabiki ndiyo wanajua, maana ukisema kila msanii ajiweke kwenye nafasi atakayo, atataka kuwa moja.

Pengine hayo yote yanaweza kuwa ya kawaida tu, maana wakati mwingine vijana hutaka wawe wanasemwa zaidi kuliko wenzao, au pengine ni katika kile baadhi ya wataalamu wa muziki wanachosema, kuna kitu kinatayarishwa, kwa hiyo haya ni mambo yanatengenezwa ili kuwapa watu ‘attention’ au kama wenyewe wanavyosema, kiki.

Lakini kuna jambo moja baya limejitokeza, ambalo hatuwezi kunyamaza kuliona linapita bila kupigiwa kelele, kwa sababu nguvu kubwa iliyotumika kuufikisha muziki huu hapa ulipofika, haiwezi kuwa sawa kuliona ni jambo dogo, la kawaida.

Ommy Dimpoz, yule kijana mwenye sauti nyororo, mmoja kati ya waimbaji wazuri, aliyeshirikishwa kuimba wimbo wa Nani kama Mama, akiwa na Christian Bella, amefanya jambo la kitoto na ambalo halikubaliki.

Aliposti picha akiwa na mama mzazi wa msanii mwenzake wanayelumbana, ambayo ni wazi kuwa waliipiga kwa nia njema kama ambavyo watoto marafiki wanavyoweza kupiga na mama wa mwenzake. Lakini kinachoudhi, ameitoa picha hiyo na kuandika maneno ya kidhalilishaji, kwanza akimdhalilisha mama huyo na isitoshe, akina mama wote wanaopiga picha na marafiki za watoto wao.

Akaandika na maneno yanayomaanisha kuwa yeye ni mpenzi wa mama huyo, hivyo kwamba kijana mwenzake huyo awe na adabu anapozungumza na baba yake.

Hapana! Tunaweza tukawa na uadui baina yetu kama vijana, tukatofautiana kwa vyovyote vile, lakini linapokuja suala la heshima, kwa mujibu wa maadili yetu, wazazi wanabaki kuwa tunu, wanaopaswa kuheshimiwa kwa asilimia zote.

Huu ni utovu mkubwa wa nidhamu na nitashangaa kama vyama vya wasanii vitakaa kimya kwa jambo hili. Kama tutaliacha hili na kuamini kuwa linawahusu wao, basi tusijeshangaa kama siku nyingine tena atatokea mtu atamtandika mwenzake risasi kama walivyofanya wale mahasimu wa kule Marekani, East na West Coast.

Mbona wana vitu vingi tu vya kusemana wao kwa wao ambavyo hata sisi tunavijua? Halafu hata kama ni kweli, hivi kijana wa miaka 30, unaona ufahari gani kuutangazia umma kuwa unatoka na mama mtu mzima wa miaka zaidi ya 50?

Hili limenikera hili na niseme tu kwamba, Dimpoz hebu shika adabu yako!

Usipitwe na Matukio, Install ===>Global Publishers App

Leave A Reply