The House of Favourite Newspapers

Hamisa Mobeto Awashika Pabaya Watesi Wake

0

 

HIVI karibuni mwanamitindo  pia staa wa muziki wa Bongo Fleva, Hamisa Mobeto aliibukia kwenye miondoko ya Singeli.

 

Aliachia Remix ya Ngoma ya Ex Wangu akishirikiana na Seneta Kilaka na kuwashika pabaya watesi wake; wale waliosema hajui kuimba bora akabaki kwenye mitindo, filamu na kuuza nyago kwenye video za Bongo Fleva.

 

Hamisa alitanguliwa na msanii wawili kugeukia Singeli kwa wasanii wa kike Bongo; alianza Zuchu na Wimbo wa Nyumba Ndogo kisha akafuata Meninah aliyeibuka na Wimbo wa Nyumba Kubwa.

 

Akifichua jinsi Hamisa alivyoingia kwenye Singeli, Seneta Kilaka anasema kuwa, mwanamitindo huyo alimtafuta kwenye Mtandao wa Instagram baada ya kuupenda wimbo huo na kumpa namba ya meneja wake kisha wakakutana.

 

Baada ya makubaliano ya kibiashara kwa pande zote ndipo wakaingia studio na kurekodi remix ya wimbo huo.

 

“Huu ni mwaka wangu wa nne nipo kwenye muziki, nilishafanya kolabo na Dulla Makabila kwenye Singeli. Katika Bongo Fleva nilifanya na Gigy Money na bado sikutoka. Ila nyota yangu inaonekana alikuwa nayo Hamisa, tumefanya tu remix ya huu wimbo, kila mmoja sasa ananitambua na muziki wangu,” anasema Seneta.

 

Video ya wimbo huo imepata watazamaji zaidi ya milioni 3.7 kwenye Mtandao wa YouTube baada ya kuwekwa hewani hadi sasa.

Ngoma hiyo ni miongoni mwa video chache za Singeli zilizopata mapokezi makubwa ndani ya kipindi kifupi.

 

Seneta anasema kuwa, kufanya kazi na Hamisa kulikuwa na changamoto mbili kubwa; kwanza ni wakati wa kushuti video, pili walipokuwa wanarekodi Hamisa ilimbidi kujitoa zaidi ya hapo awali.

 

“Kwenye kufanya video ilikuwa ngumu kwa sababu kuna sehemu kama mbili nilitakiwa kucheza na Hamisa, nimshike kiuno, mara nimbambie, ilikuwa ni ngumu kwa sababu yule ni dada yangu na ni shemeji yetu. Ila aliniambia mdogo wangu usiogope wala usiwe na aibu tupo kazini, fanya chochote kinachohitajika kunogesha muziki wetu,” anasema Seneta huku akitabasamu.

 

“Wakati tunarekodi nilimwelekeza kwa sababu muziki wa Singeli unahitaji pumzi na nguvu kidogo, maneno yako uyatoe kwa hali ya mkazo, japokuwa ilikuwa ni ngumu kwake, lakini tulirekodi na unaona ngoma imetoka vizuri,” anasema Seneta.

 

Agosti, 2018 ndipo Hamisa aliachia ngoma yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la Madam Hero. Ngoma hiyo imeandikwa na msanii Foby na kusukwa na Prodyuza C9.

 

Kihistoria, kwa mara ya kwanza, Januari Mosi, 2019, Hamisa alitumbuiza jukwaani baada ya kuachia wimbo huo na mwingine uitwao Tunaendana ambao video yake ilifanyika nchini Marekani.

 

Aliwahi kuambiwa na baadhi ya watu kwamba hawezi kuimba, lakini yeye alijibu; “Mimi ni mtu ambaye huwa sikati tamaa, huwa naamini katika vision yangu mwenyewe, naamini ndoto zako ni za kwako ambazo umepewa na Mungu, kwenye haya maisha ukisikiliza watu wanachosema hutafika mbali, kama ulipangiwa kufika sehemu f’lani utafika tu.”

 

Mtangazaji wa E-FM Radio, Fido ambaye anatangaza Kipindi cha Genge kinadili na muziki Singeli pekee, anasema hiyo ni ishara kuwa muziki huo umezidi kukua na anategemea kuona wasanii wengi wa Bongo Fleva bila kujali jinsia wakiungana pamoja na kufanya mambo makubwa.

 

“Imeshakuwa biashara na mtaani ndiyo unahitajika sana, hivyo wasanii wa Bongo Fleva wanalazimika kufanya hivyo ili kuifikia mitaa, pia wanaona kwenye shoo jinsi wasanii wa miondoko hiyo wanavyoamsha.

“Hivyo basi wao wanajikuta hakuna namna zaidi ya kufanya muziki wa Singeli na ndiyo changamoto kubwa iliyoukumba muziki wa Bongo Fleva hivi sasa,” anasema Fido.

 

Kuhusu wasanii wa kike kutoka kwenye Bongo Fleva kuonesha muitiko zaidi upande wa Singeli kwa kipindi cha hivi karibuni, Fido anasema hiyo ni kutokana na muziki huo kutoa fursa ya mipasho, kitu ambacho wanawake wengi wanakipenda kama ilivyokuwa Taarab miaka ya nyuma.

 

“Unajua Singeli ni muziki wa Uswahilini kama Taarab huko nyuma, wanawake wengi wamehamasika kufanya kwa sababu unashabihiana na mipasho ya Pwanipwani, ni kama version mpya ya Taarab. Ndiyo maana wameupenda, unajua tena watoto wa kike wanapenda kuchambana na unawapendeza sana wanapoufanya,” anasema.

 

Kwa upande wa prodyuza wa muziki Bongo, Mocco Genius ambaye ametengeneza Wimbo wa Meninah wa Nyumba Kubwa wenye mahadhi ya Singeli pia. Anasema miondoko hiyo ni utambulisho wa muziki wa Kitanzania na ndiyo sababu unazidi kushika kasi na pia kila muziki una wakati wake.

 

“Kuna kipindi wasanii walikuwa wanashauriwa kuupa nguvu muziki wa Singeli kwa sababu ndiyo unaibeba asili yetu na ukisikiliza hamna nchi yoyote ambayo inaupiga,” anasema Mocco.

 

Aliongeza; “Sasa wakitoka wasanii wa Bongo Fleva wakafanya Singeli ni kwamba wanafanya muziki ambao unaweza kusikilizwa na mtu yeyote kutoka Taifa lolote, kwa hiyo kwangu ni kitu kizuri na waendelee kuufanya.”

 

Wasanii wenye majina makubwa waliofanya Singeli hadi sasa ni wengi; miongoni mwao ni Professa Jay, Harmonize, Ruby, Ben Pol, Snura, Lava Lava, Mr Blue, Rayvanny, Ibraah na wengine wengi ambao wameachia nyimbo zenye mahadhi hayo.

Makala: ELVAN STAMBULI

Leave A Reply